02 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wanavijiji bado hawajaweza kutambua, kutumia fursa zilizopo kiuchumi
 
2008-05-02 08:53:12
Na LUSEKELO PHILEMON

Vijiji vingi hapa nchini vina rasilimali nyingi ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuwakomboa kutoka kwenye lindi la umaskini.

Viongozi wa vijiji, kata, wilaya na Mikoa bado hawajaweza kufanya kazi yao ya kuwashirikisha wananchi wao kuibua, kuainisha na kutumia fursa zao kiuchumi.

Wananchi wengi bado wanaendelea kuishi maisha duni na hali ni mbaya zaidi kwa wakazi wa vijijini kwani wengi wao wamekuwa wakiishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa matope na kuezekwa kwa nyasi.

Wengi wanaoishi maisha hayo siyo kuwa wametaka hali iwe hivyo ila umaskini wa kipato, mtazamo wa kiakili umechangia hali hiyo.

Hali hii imewafanya vijana wengi kukimbilia mijini kwa matumaini ya kupata maisha bora.

Lakini kwa sababu ya kukosa ujuzi vijana wengi wamejikuta wakiishi pia maisha magumu kwa kukosa kazi za kufanya wawapo mijini.

Mipango ya Serikali kama vile MKUKUTA na MKURABITA haijaweza kutoa msukumo wa kutosha kuwakwamua Watanzania kutoka kwenye lindi la umaskini.

Hamasa haijaweza kutolewa vya kutosha ili watu mahali walipo waweze kuzibadilisha rasilimali walizonazo ziweze kuwaletea Maendeleo ya kiuchumi na hatmaye kuondokana na umaskini.

Umaskini ni gonjwa ndugu ambalo linaendelea kuwatafuna Watanzania siku hadi siku.

Matatizo mengi ya kijamii hapa nchini yanatokana na umaskini uliokithiri ukasababishwa na Ukimwi na magonjwa mengine yanayofanana na hayo.

Ni kutokana na ukweli huo, Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) limeamua kupanua wigo wa majukumu yake na kuisaidia jamii ya Watanzania waishio vijijini.

Baraza hilo likiwatumia wakuu wa Mikoa, Wilaya, kata na vijiji linataka wananchi katika maeneo yao kuainisha fursa zilizopo ili ziweze kutumika kwa uwekezaji utakao leta tija kwa jamii nzima ya kila eneo husika.

Kutokana na hatua hiyo baraza hilo linawataka wakuu wa mikoa na wilaya zote nchini kuwashirikisha wananchi kikamilifu katika kuzitambua fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao kwa kuwasilisha mawazo na maoni yao katika ngazi ya Taifa, lengo likiwa ni kuongeza ajira na kuwaondoa wananchi hao katika umasikini walionao.

Akizungumza hivi karibuni na wakuu wa Mikoa na Wilaya kanda ya Pwani kuhusu uwezeshaji wa kiuchumi nchini, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Bw. Dunstan Mrutu anasema , Baraza lake limejiandaa kuhakikisha azma hiyo inafikia lengo.

``Hii ni sehemu ya mkakati wa Baraza kuzikutanisha sekta binafsi na serikali katika majadiliano yenye lengo la kuboresha mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji yatakayopelekea kuongeza ajira kwa wananchi kwa kutumia rasilimali zilizopo ili kuondokana na umasikini,`` anasema.

Bw. Mrutu anawataka wakuu hao wa wilaya kufanya midahalo ya mara kwa mara na vikundi vya kijamii ambavyo vitakuwa vinawakilisha maoni na mawazo ya wananchi kuhusu kuzitambua fursa hizo za kiuchumi.

Anavitaja vikundi hivyo kuwa ni pamoja na vya wafanyabiashara, wakulima, wafugaji, wavuvi, vijana, wasomi, wanahabari na vinginevyo ambavyo wakuu hao wa wilaya wanatakiwa kuvitambua kutokana na rasilimali zilizopo katika maeneo yao.

``Ninyi mnatakiwa kuwa ni wawakilishi wa wananchi wenu, kuleta mawazo yao kuhusu nini kifanyike, wanataka nini na namna gani tuwahudumie,`` anasema katibu huyo.

Katika hilo wakuu hao wa wilaya na mikoa nao wanataja changamoto mbalimbali zilizopo mbele yao kuwa ni pamoja na baadhi ya viongozi kutokuwa wawajibikaji na watendaji wa mipango mbalimbali inayoibuliwa na serikali kwa lengo la kupunguza umasikini na kukuza ajira.

Kwa mfano, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Abbas Kandoro anasema kuwa kwa muda mrefu sasa mipango imekuwa ikianzishwa kwa lengo la kuondoa umasikini wa wananchi lakini matokeo yake imekuwa ikiishia kwenye makabrasha.

Anafafanua kuwa hivi sasa viongozi wa ngazi za chini wanatakiwa kubadilika kiutendaji ili azma hiyo ya kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi ifikie malengo.

``Mimi naona kuna tatizo katika uwajibikaji. Mambo mengi yamekuwa yakianzishwa kwa madhumuni mazuri tu lakini yamekuwa yakiishia vitabuni. Naomba tutakapokuwa na mjadala wa kitaifa jambo hili lizungumzwe.`` anafafanua Bw. Kandoro.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Said Saddick analitaka Baraza hilo kuangalia namna ya kuwasaidia wakulima hasa wa zao la korosho katika mikoa ya kusini katika upande wa masoko ili wawe na ari ya kuzalisha zao hilo kwa wingi.

Bw. Saddick anasema kuwa wakulima wengi wanapofikia katika uuzaji wa mazao yao, soko huwa ni la shida kwao na hivyo kupunguza ari ya kuendelea kulima zao hilo kwa wingi.

``Wananchi bado wanaendelea kukaa na kuishi katika nyumba za nyasi, hawana maendeleo yoyote. Naomba sasa hili la uwezeshaji kiuchumi wananchi liwe la manufaa kwao,`` anasema Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Bi. Hawa Mchope.

Bi. Mchope anatoa changamoto kwa Serikali kuhakikisha mpango wa kuwawezesha wananchi kiuchumi unafanikiwa badala ya kuwa ni kitendawili kwa wananchi akitolea mfano wa MKURABITA na MKUKUTA.

Anasema kuwa mipango mingi ilianzishwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi kiuchumi, lakini bado hali za wananchi walio wengi kiuchumi si za kuridhisha.

Hata hivyo, akitolea majibu hoja hizo Bw. Mrutu anasema awali mipango hii ilikuwa ikitolewa maamuzi na ngazi za juu pasipo kuwashirikisha wananchi jambo ambalo limepelekea kutofikia malengo yaliyokusudiwa.

Bw. Mrutu anasema kuwa kwa kuliona hili, Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) limeamua kuwashirikisha wananchi kikamilifu katika kuzijadili na kuzitambua fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao, ili uwezeshaji uelekezwe moja kwa moja katika fursa zilizoainishwa na wananchi hao.

``Na ndio maana sasa TNBC tukaamua kuwepo haya majadiliano kwa kuzikutanisha sekta binafsi na zile za serikali,`` Bw. Mrutu anafafanua.

Katika mada yake kuhusu uwezeshaji wa kiuchumi, mshauri wa mambo ya uchumi wa TNBC, Profesa Lucian Msambichaka anaishauri serikali kuimarisha baadhi ya sheria zake ili uwezeshaji wa kiuchumi uweze kufanikiwa hapa nchini.

Anasema kuna baadhi ya sheria ambazo bado ni kikwazo na kukwamisha juhudi za wananchi kujikwaamua kiuchumi.

Profesa Msambichaka anaeleza kuwa ili kuhakikisha azma ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, ni vema vikwazo vya kiuchumi vikawekwa bayana ili wananchi wasiwe na mashaka yanayopelekea kuhoji kuhusu vikwazo hivyo.

Mtaalamu huyo anasema imekuwa vigumu pia kwa suala la rasilimali fedha kushindwa kuwafikia walengwa hasa wale waishio vijijini. Anasema matokeo yake fedha hizo hushindwa kuleta maendeleo ya sehemu hizo kama ilivyokuwa imekusudiwa na kufanya suala la mabadiliko ya kiuchumi kuwa ni kitendawili siku zote.

Kwa mujibu wa Profesa Msambichaka, baadhi ya vikwazo vya kiuchumi vilivyopo kwa wananchi wengi wa vijijini na kupelekea kutopata maendeleo ni pamoja na elimu duni, kutokuwepo kwa mahusiano ya karibu baina ya sekta binafsi na serikali, tatizo vifo vinavyotokana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi pamoja na tatizo la uwekezaji.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.