02 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Halmashauri ziimarishe kudhibiti ubadhirifu
 
2008-05-02 08:50:54
Na Mhariri

Ndani ya gazeti hili kwenye toleo letu la jana tuliandika habari zilizohusu Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani ambao waligoma kupitisha bajeti ya Sh. milioni 75 kwa ajili ya ununuzi wa gari la Mkurugenzi wa halmashauri hiyo na kuazimia badala yake fedha hizo zinunue matrekta kwa ajili ya kuwasaidia kilimo wananchi.

Taarifa zinasema kwamba madiwani hao walifikia maamuzi hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye alikuwa miongoni mwa wageni wa kikao hicho kilichokuwa kikijadili bajeti ya halmashauri hiyo.

Hakika, hata katika taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG), ilibainika kwamba, ubadhirifu ndiyo chanzo kikubwa kinachokwamisha utendaji madhubuti wa idara za serikali.

Ilibainika kwamba ununuzi wa vifaa mbalimbali katika idara za serikali umekuwa hauzingatii taratibu na kanuni za kifedha au bajeti zilizowekwa.

Pamoja na madiwani hao kuzuia kupitisha bajeti hiyo inayohusu gari la kifahari, ni vizuri viongozi hao ambao wanawawakilisha wananchi wakapitia kasma nyinginezo ambazo pia hukithiri kwa ubadhirifu mkubwa.

Baadhi ya maeneo ambayo halmashauri hizi zinatuhumiwa kuhusika na ufujaji wa fedha ni misaada ya fedha zitolewazo na wahisani, maandalizi ya semina, warsha, mikutano na safari za kikazi zisizokuwa na ulazima pamoja na shughuli hewa.

Kwa upande wa pili ni lazima katika halmashaurui hizi pia kukaangaliwa hata baadhi ya madiwani ambao pia hujihusisha na kuzihujumu halmashauri wanazozisimamia.

Tumekuwa tukipata taarifa za baadhi ya madiwani kumiliki kampuni zitoazo huduma katika idara zilizo chini ya halmashauri zao, jambo ambalo ni rahisi kujitokeza mgongano wa maslahi.

Inakuwa si rahisi zabuni akapewa mzabuni asiyekuwa diwani hata kama huduma zake ni bora endapo miongoni mwa madiwani kuna ambaye ameomba apewe zabuni iliyotangazwa.

Halikadhalika, tunadhani, badala ya kulaumu kuhusu utendaji wa Wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali nchini, ni vizuri madiwani nao wakajitathmini utendaji wao wa kazi katika kufuatilia masuala yanayohusu halmashauri zao.

Mfano unaohusu halmashauri hiyohiyo ya Kibaha ni uzembe ambao uliwahi kufanywa na Halmashauri kushindwa kuchukua fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo hadi kufikia kipindi ambacho ilistahili zirejeshwe serikalini.

Halmashauri ya Kibaha ilikuwa ni miongoni mwa halmashauri kadhaa nchini ambazo zilithibitika kuzembea kuchukua ruzuku hizo, madiwani wakiwa wanahusika moja kwa moja.

Hata hivyo, wakati madiwani wakijitahidi kufuatilia utendaji kazi wa watumishi wa halmashauri, ni vyema nao wakahakikisha kwamba nao wanafanya kazi zao kivitendo kwa maslahi ya wananchi na siyo kutoa lawama pasipo kuonyesha njia za kuondokana na kero zilizopo.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.