30 Apr 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kila tuhuma ya ufisadi isipuuzwe ukweli utafutwe
 
2008-04-30 08:53:11
Na Dunstan Bahai

Katika historia ya Tanzania, hakukuwa na tabia ya wananchi au viongozi kwa viongozi kupakana matope, lakini sasa kumeibuka tabia ya watu aidha kuchafua tabaka fulani au kueleza ukweli juu ya tabaka hilo.

Mmoja wa watu ambao wanaheshimika sana katika umma wa Watanzania ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Samuel Sitta, ambaye ameibuliwa kashfa nzito za matumizi mabaya ya fedha za chombo hicho.

Mhe Sitta ametuhumiwa kujiongezea masurufu ya safari na kwamba anadaiwa na ofisi ya Bunge zaidi ya Sh. milioni 60.

Tuhuma hizo nzito ziliwastua watu wengi kwani Bw. Sitta amejitahidi kulifanya Bunge kuwa na heshima kubwa. mara baada ya kukabidhiwa uongozi wa taasisi hiyo alisema kuwa litakuwa la kisasa lenye spidi na viwango.

Bunge kama mhimili wa tatu wa nchi, na yeye kama msimamizi mkuu wa mhimili huo, watu walioamua ama kuibua tuhuma hizo chafu dhidi yake, si wajinga kwani ni watu wenye elimu zao na wanajua ni chombo gani wakikitumia wanaweza kufikisha ujumbe huo kikamilifu.

Wakachagua kutumia njia mitandao ya intaneti na kusambaza huku na huko ndani na nje ya nchi ili watu wapate fursa ya kusoma kikamilifu na kujenga mashaka makubwa kwa kiongozi huyo.

Kwa namna yoyote ile, Bw. Sitta ni mmoja wa viongozi nchini ambao kutokana na michango yao wamekubalika aidha kwa viongozi wenzao au kwa wananchi kwamba wanajitahidi kutimiza wajibu wao kikamilifu.

Kwa hiyo, kama tuhuma zilizopo mbele yake hazina chembe ya ukweli kwa kiasi kikubwa zitakuwa zimefanikiwa kuwashawishi vinginevyo watu wasio makini na kumshushia hadhi kubwa na hata wananchi watakuwa njia panda kuamua kama ukweli spika wanayemfahamu kumbe na yeye ni kundi la wale wale.

Kuvurumishiana tuhuma nzito kama hizo,endapo hazina chembe ya ukweli, zikiwa zimelenga kuendeleza ile hali ya kuchafuana, zisiposhughulikiwa mapema zinaweza kumuweka pabaya mbele ya macho ya wananchi wao na hasa wapiga kura wake.

Lakini kuenea kwa tuhuma hizo, mbaya zaidi ni kwamba familia zao nazo zitatengwa na jamii inayowazunguka huku zikiwanyooshea vidole vya shari.

Kama itafikia mahali chombo kikuu cha kutunga sheria za nchi kama Bunge, mahali panapotolewa maelekezo muhimu kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa nchi, iwapo wananchi wanakosa imani nacho, kuna kila dalili za wazi kuwa inaweza ikafikia mahali chombo hicho na wabunge wake wakadharauliwa na wananchi kwamba hawako makini na maslahi ya wananchi zaidi ya kuzingatia maslahi yao binafsi hata kutilia shaka michango na maamuzi yao wanayoyatoa kutoheshimika.

Zipo hatua mbalimbali za kuweza kumpangusa matope Spika wetu, endapo kweli hahusiki kabiasa na tuhuma hizo.

Njia ya kwanza ni kama ile ambayo tayari ameichukua ya kutoa ufafanuzi bungeni kuhusu suala hilo nyeti, ili kuwafahamisha waheshimiwa wabunge namna gani anazipokea taarifa hizo ikiwa pamoja na wananchi kupata fursa ya kumsikia kwa kinywa chake akijaribu kujisafisha.

Njia nyingine ni kuundwa kwa Kamati huru ya Bunge kuchunguza tuhuma hizo, kama kanuni zinavyoruhusu kwa wabunge wengine kufanyiwa uchunguzi anapokabiliwa na tuhuma ili kuoana ukweli wa mamabo kama itabainika kuwa hakuna uweli wowote ni kwamba waliozushatuhuma hizo watakuwa wamefanikiwa kumjenga zaidi spika kuwa ni mtu muadilifu badala ya kumbomoa na hivyo jamii kuwa na imani naye kubwa.

Aidha, njia ya tatu ambayo hiyo ni muhimu zaidi, ni kutafuta mkaguzi wa hesabu wa kujitegemea, kama ilivyofanywa na Benki Kuu ili afanye kazi kwa kuchunguza kwa makini mahesabu ya taasisi hiyo ikiwa pamoja na yale yanayoidhinishwa binafsi na kiongozi huyo.

Kimsingi kuchukua uamuzi huo kutasaidia sana kujua sio tu matumizi ya spika ni pamoja na mwenendo wa fedha wa Bunge lote katika kipindi ambacho mheshimiwa Sitta amekuwa madarakani.

Wakati ufumbuzi wa suala hilo unatafutwa ili ukweli ubainike na kuondoa mashaka yaliyopo, ni muhimu sana juhudi zikafanyika kuwabaini au kumbaini mtu anayesambaza taarifa hizo kama ni muongo ili aweze kudhibitiwa ipasavyo na kama ni mkweli aweze kupongezwa kwa kuonyesha uzalendo wa hali ya juu wa kuonyesha kuwa mali ya umma imekabidhiwa kwa mtu au watu ambao si waadilifui aslani.

Hatua hiyo inatakiwa ifanywe kwa uangalifu na umakini sana katika kuhakikisha kuwa ni yule tu anayehusika anafikiwa hata kama amejificha wapi na katika mazingira gani ili awe mfano kwa watu wengine wenye malengo kama yake.

Hata hivyo, ipo haja ya kutafuta watu wanaosambaza tuhuma hizo na kuwachukulia hatua kali, lakini kama tuhuma hizo zinagundulika kuwa za kweli, basi wapongezwe watu walioziibua.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.