|
Elimu ya uzalendo itapunguza mafisadi
2008-03-19 08:51:23
Na Joseph Mwendapole
Elimu ya uzalendo na watu kufundishwa kuipenda nchi yao kunaweza kupunguza idadi ya mafisadi na wala rushwa.
Uzalendo ni neno dogo lakini maana yake ni kubwa kwa tafsiri ya kawaida.
Unapozungumzia uzalendo unaongelea juu ya watu kuipenda nchi yao na kuweka maslahi ya taifa mbele kuliko maslahi binafsi.
Ni kutokana na umuhimu huo suala la elimu ya uzalendo linapaswa kuanza kupewa umuhimu wake katika kuwajenga wananchi.
Mtoto anapozaliwa akalelewa katika misingi ya kuipenda nchi yake ni dhahiri atakua na mtazamo wa kuipenda nchi yake.
Tuanze kuwafundisha watoto nini maslahi ya Taifa wakiwa wadogo, wafundishwe kuwa wajenga nchi ni wananchi wenyewe. Pengine inaweza kupunguza idadi ya mafisadi na wala rushwa tulio nao.
Watu wakiipenda na kuithamini nchi yao hawawezi kuitafuna kama ambavyo imebainika hivi karibuni.
Ingawa haiwezekani wakakosekana wachache ambao ni akina haambiliki lakini tunaweza kusaidia kujenga kizazi cha wapenda nchi yao kwa dhati.
Waswahili wanasema msafara wa mamba kenge nao wamo.
Kashfa ya hivi karibuni ya wizi wa Sh bilioni 133 BoT ni matokeo ya watu kukosa uzalendo na kuweka maslahi yao binafsi mbele.
Na wizi uliotokea BoT ni robo ya uvundo ulioko serikali ambako imekuwa ikiripotiwa katika vyombo vya habari mara kwa mara.
Imekuwa ikisikita kuwa kiasi fulani cha fedha kimetoweka wizara fulani na zimekuwa zikipotelea matumboni mwa watu wachache.
Kashfa ya Richomnd iliyopelekea baadhi ya vigogo kuondoka madarakani ni kielelezo cha kukosekana uzalendo.
Endapo watanzania wanaamua kwa makusudi kula njama na kuipa tenda kampuni hewa isiyo na ofisi wala ujuzi ni dhahiri uzalendo haupo.
Watu wanaamua kuliingiza taifa katika hasara kubwa ya kuilipa kampuni hewa mabilioni ya shilingi kwa manufaa yao binafsi.
Enzi za utawala wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere yasingeweza kutokea yaliyotokea.
Alikuwa mkali na hakuwa na mzaha na wala rushwa hivyo kutokana na msimamo wake watu wenye uchu na rushwa walilitambua.
Walijua kuwa ukila rushwa na mwalimu akabaini umekwenda na maji.
Vivyo hivyo viongozi wa sasa Rais Jakaya Kikwete na Waziri wake Mkuu Mizengo Pinda wafuate nyayo hizo.
Viongozi wetu wasiwe na mzaha, wawe wakali kama Nyerere kwani hali imekuwa mbaya na watu wanakula rushwa hadharani.
Elimu itolewe kwa nguvu kuhusu uzalendo na wasio sikia washughulikiwe kwa kutumia nguvu zao dola.
Uzalendo pia uende mbali kwa watanzania kuanza kuzipenda bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Kuna dhana potofu kudhani kuwa kitu chochote kizuri kinatoka nje.
Kutokana na dhana hiyo watu wamekuwa wakiacha kununua bidhaa bora zinazotengenezwa hapa nchini na kukimbilia za nje.
Wanasahau kuwa kwa kununua bidhaa za nje unajenga uchumi wa nchi za nje, unaongeza ajira nje na kuimarisha taifa la nje.
Baadhi ya nchi wameligundua hilo mapema, wakawaelimisha na kuwahamasisha wananchi wao kununua bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.
Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Deodorus Kamala, anasema katika baadhi ya nchi uzalendo uko juu.
Anatoa mfano wa nchi jirani ya Kenya kuwa wananchi wake wanapendelea zaidi bidhaa zinazozalishwa kwao.
Anasema kuna wakati alikwenda nchini Kenya na alipokaa katika baa moja akaagiza bia moja ya nje.
Anasema alishangaa kusikia kuwa bia hiyo haiuzwi Kenya na inayopatikana kwa wingi ni bia aina ya Tusker inayozalishwa nchini humo.
Dk. Kamala anasema aliwauliza kwanini hawauzi hiyo ambayo nchini Tanzania ukiinywa unaonekana mwenye hadhi,wakasema wanajenga nchi yao, wanataka kuongeza ajira kwa wananchi wa Kenya.
Pengine hali hiyo inaweza kutufumbua macho, inapofikia watu wanaacha kuuza bidhaa za nje na kuuza zinazozalishwa nchini mwao.
Huo ni uzalendo wa hali ya juu na ndio huenda umewafikisha wakenya hapo walipo.
Uchumi wa Kenya uko juu sana ukulinganisha na nchi za Tanzania na Uganda.
Bajeti ya nchi hiyo haitegemei wahisani, Tanzania tukianza sasa hatujachelewa, tuwaelimishe watanzania umuhimu wa kuipenda nchi yao.
Wazalishaji wa ndani nao wanatakiwa kuongezea ubora bidhaa wanazozalisha ili kuwavutia walaji.
Baadhi yao wamekuwa wakiongezea ubora bidhaa wanazouza nje na zile za ndani kuziacha katika hali ya kawaida.
Hali hiyo imekuwa kwa kiasi kikubwa ikichangia kuwakatisha tamaa Watanzania kununua bidhaa hizo.
|