|
Mamlaka za maji ziweke mikakati endelevu
2008-03-19 08:49:54
Na Mhariri
Hii ni Wiki ya Maji nchini pote ambapo idadi kubwa ya Watanzania wanatarajia kuwa, lengo kubwa litakuwa ni kuwahakikishia wananchi mipango madhubuti ya kuwapatia maji yaliyo salama katika maeneo wanayoishi.
Hakuna asiyefahamu umuhimu wa maji kwa binadamu, mifugo na hata mimea kupata maji yaliyo salama kwa ajili ya matumizi muhimu.
Bila kuwepo upatikanaji wa maji salama ya kutosha katika makazi yoyote ya binadamu, ni rahisi kabisa kuibuka kwa magonjwa ya milipuko kama kipindupindu au kuhara damu.
Licha ya juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na mamlaka mbalimbali za maji nchini, bado upatikanaji wa maji salama, hauridhishi katika maeneo mbalimbali ya mijini na vijijini.
Katika baadhi ya maeneo ya mijini, mathalani katika jiji la Dar es Salaam, bado wakazi wake wanaendelea kutumia maji ya visima ambapo nyakati za mvua kubwa, huathiriwa na maji machafu yanayofunguliwa kutoka katika chemba za maji machafu zinazomilikiwa na wakazi wengine.
Kwa wakazi wa Dar es Salaam ambao wanaishi katika maeneo ya mabondeni, jambo hili siyo la ajabu hata kidogo, na ndiko ambako milipuko mikubwa ya magonjwa kama kipindupindu husambaa kwa haraka.
Kuna habari kuwa, hata baadhi ya miundombinu ya mabomba, huungana na yale yanayosafirisha maji machafu.
Tunafahamu kwamba, mamlaka hizi wakati mwingine zinakabiliwa na vikwazo katika utekelezaji wa mipango yao, japokuwa tunadhani kuwa pia zinakosa mikakati ambayo inaweza kufanywa bila hata kupata misaada nje ya taasisi zao.
Ndani ya gazeti hili leo kwa mfano, tumeandika habari kuwa, Kata ya Igoma iliyopo mjini Mwanza, bado inaongoza kwa kuwa na matukio mengi ya wizi wa mita za maji yanayozalishwa kupitia ofisi ya Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka (MWAUWASA).
Hayo yalisemwa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Bw. Justus Rwetabula wakati akisoma taarifa ya Mamlaka hiyo kwenye uzinduzi wa Wiki ya Maji, sherehe ambazo zilifanyika katika Kata ya Butimba.
Mkurugenzi huyo aliyataja maeneo mengine yenye matukio mengi ya wizi wa mita za maji kuwa ni Mabatini, Bugarika, Igogo pamoja na Nyegezi.
Kata ya Igoma pia mwaka Jana, ilitajwa na mkurugenzi huyo kwamba inaongoza kwa wizi wa mita za maji jijini humo.
Bw. Rwetabula alisema tatizo la wizi wa mita za maji bado ni kubwa katika maeneo hayo licha ya kwamba ofisi yake imetangaza na tayari imeanza kutoa zawadi kwa watu wanaotoa taarifa za siri dhidi ya wananchi wanaoihujumu mamlaka.
Tatizo la wizi wa mita za maji halipo Mwanza pekee, bali ni kitu ambacho kimesambaa nchi nzima.
Lakini pamoja kuwepo kwa wizi wa mita, kuna uzembe ambao unatokana na mamlaka hizo kutokuwa makini katika kudhibiti maji yanayopotea kufuatia mabomba yanayoharibika au kuharibiwa na watu wasiokuwa waaminifu.
Tunazo taarifa kwamba, waunganishaji wakubwa wa mabomba yanayotumia maji ya wizi ni `vishoka` wanaoshirikiana kwa karibu na mamlaka husika za maji.
Watumishi hao hao wasiokuwa waaminifu, ndio ambao wamekuwa wakiwapa taarifa wezi wa maji kila kunapotaka kuendeshwa operesheni maalumu za kuwanasa wahalifu hao.
Tunadhani kwamba, kuna kila sababu kwa mamlaka zenyewe kuanza kuwachunguza watumishi wao jinsi wanavyojihusisha na uhalifu kama huo.
Hali kadhalika, kumekuwepo na urasimu usiokuwa wa lazima wa kuwaunganishia maji wateja, hata kama tayari wameshalipia gharama zote za uunganishaji, mazingira ambayo yanaashiria rushwa.
Tunapenda kutoa wito kwamba maadhimisho ya wiki ya maji mwaka huu, yadhamirie kutafuta dawa ya kasoro zote zinazokwamisha upatikanaji wa maji salama nchini Tanzania.
Hali kadhalika, ni vyema kipindi kama hiki, Wizara ya Maji na Umwagiliaji ziweke mikakati madhubuti ya kuwashirikisha wadau binafsi ili nao waweze kushiriki katika usambazaji maji, tukiamini kwamba kwa namna hiyo kutazipunguzia mzigo taasisi za umma kuhimili jukumu hilo muhimu peke yao.
|