|
Operesheni ondoa ombaomba iwe ya kudumu
2008-03-18 10:08:15
Na Mhariri
Moja ya kero ambazo zinaonekana kukua kwa kasi kila siku, hasa katika maeneo ya mijini ni ongezeko la watu wanaoamua kuendesha maisha yao kwa kuomba pesa.
Ombaomba hawa wamegawanyika katika jinsia na rika tofauti kama vile wazee, wanawake, wasichana na watoto wadogo ambao umri wao ni chini ya miaka 10.
Cha ajabu ni kwamba, ombaomba wengi walio na umri zaidi ya miaka 18 ni watu wazima, ikiwa ni pamoja na wasichana wadogo ambao huonekana wakiwa wamebeba watoto wachanga.
Itakumbukwa kwamba manispaa mbalimbali nchini hasa Dar es Salaam na Morogoro zimewahi kuendesha operesheni maalumu ambazo zililenga kuwaondoa ombaomba mijini na kuwarudisha makwao, kwani licha ya kero ya kuomba, pia wana tabia ya kuchafua mazingira kwa kujisaidia hovyo.
Zoezi hili limekuwa likifanyika kama `zimamoto` ambapo baada ya kuwakamata na kuwasafirisha makwao, mamlaka husika za miji hutulia bila kuweka mikakati ya kuwazuia wasirejee tena mijini.
Imefikia sasa ombaomba wengi wameigeuza hali hiyo kama ajira rasmi ambapo hata watu wenye viungo kamilifu, bila aibu huonekana na mifuko ya `rambo` wakipita duka hadi duka au baa hadi sehemu nyinginezo za starehe kwa ajili ya kuomba pesa.
Sisi kimsingi hatupingi suala la watu wanaoishi katika mazingira magumu kupewa misaada, alimradi misaada hiyo ikusanywe na kutolewa katika taratibu rasmi.
Wakazi wengi wa Dar es Salaam watamkumbuka ombaomba maarufu aliyekuwa na maskani yake katika mtaa wa Samora, aliyejulikana kama `Matonya` ambaye shughuli ya kuomba aliifanya kama kazi rasmi.
Halikadhalika, kumejitokeza hata baadhi ya watu watanashati, wanawake kwa wanaume ambao hujifanya kama wana matatizo, kumbe ni matapeli wakubwa.
Lakini hali sasa imekuwa mbaya ambapo hata watoto wadogo huingizwa kufanya shughuli hiyo ya kuomba pesa na hivyo kuwanyima fursa hata ya kupata elimu au huduma nyinginezo za jamii.
Tunaelezwa kwamba, baadhi ya wasichana wadogo ambao ni ombaomba hushirikishwa vitendo vichafu vya ngono na hivyo kuwahatarishia afya zao.
Tunajua kwamba mifarakano ya wazazi pamoja na gonjwa la ukimwi vinachangia ongezeko la ombaomba watoto mitaani, lakini jamii haiwezi kukaa kimya bila kuchukua hatua ya kukaa na watoto hawa, kujua matatizo yao na kuwatafutia ufumbuzi wa maisha muafaka ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kwenye vituo husika.
Tufikie mahali tukahoji idadi ya watoto ambao Tanzania inawapoteza kila mwaka wakiachwa kuwa ombaomba huku hata mamlaka husika zikifumbia macho.
Tunadhani kwamba sasa ni wakati ambapo utatuzi wa suala hili uanzie katika jamii ambako ombaomba hao wanatoka ambapo serikali za mitaa zina wajibu wa kuwaeleza wakazi wao waliopo vijijini kwamba mijini siyo sehemu pekee ya kujipatia riziki.
Halikadhalika, jamii ijue kwamba kitendo cha kumpa ombaomba Shilingi 50 au 100 siyo jawabu kamili la kumuondolea kadhia hiyo ila kila mmoja atumie fursa hiyo kuwapa ushauri nasaha kwamba tabia hiyo ni aibu kwao na taifa kwa ujumla.
Ni wazi kwamba, kama unafanyika utafiti wa kutosha inaweza kubainika kwamba wengi wa wale wanaojiita ombaomba wanazo familia zao ambazo zingeweza kuwahudumia kwa mahitaji yao muhimu isipokuwa wameshaathirika kwa kutaka kupata pesa bila kufanya kazi.
Halikadhalika, baadhi yao ni watu ambao wanaweza kujishughulisha na uzalishaji mali kama kilimo na hivyo kuweza kujitegemea.
Bila shaka kuna haja kwa manispaa zote mijini kuweka sheria ndogondogo ambazo zitawabana zaidi ombaomba.
Ombaomba ambao wataonekana sugu kubadilika wakusanywe na kupelekwa katika makambi yenye usimamizi ili wajihusishe na kufanya kazi.
Vinginevyo miji yetu itaendelea kuwa na ongezeko kubwa la watu wasiokuwa na faida yoyote, huku wakijitengenezea mazingira magumu wenyewe.
|