|
Elimu ina nafasi kubwa ya kukomboa mwanamke
2008-03-18 10:07:33
Na Sharon Sauwa
Mgawanyo wa raslimali fedha kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, ni msingi wa maendeleo ndio kauli mbiu ya siku ya wanawake mwaka huu.
Katika makala hii inayoandikwa na Mwandishi Wetu Sharon Sauwa inaelezea jinsi wanawake wanaoweza kufikia katika hali hiyo.
Harakati za kudai usawa wa kijinsia zilianza miaka mingi iliyopita lakini hadi hivi leo bado harakati hizo hazijaweza kuzaa matunda ya kuridhisha hasa hapa nchini ambapo wanawake hasa wale wa vijijini wameendelea kutaabika kwa kazi ngumu, mila na desturi potofu na mfumo dume.
Lakini aluta kontinua ipo siku tunaweza tukimuona mwanamke akiondokana na matatizo hayo endapo jitihada hizi zitaendelea katika kila kona.
Hata hivyo, hatua ya mgawanyo wa raslimali fedha kijinsia na uwezeshaji wanawake inatakiwa kuzingatiwa ili kulisaidia kundi hili kupiga hatua zaidi.
Moja ya jitihada hizo ni wanawake kuwa na siku yao maalum ya kujadili na kutafakari mambo mbalimbali yanayowahusu wao wenyewe.
Chimbuko la siku ya wanawake duniani linatokana na na harakati za wanawake nchini Marekani.
Kwa mujibu wa kumbukumbu mbalimbali duniani inaonyesha siku hii inatokana na wanawake wafanyakazi viwandani nchini Marekani kuamua kuandamana kupinga maovu mbalimbali yaliyokuwa yakifanywa na waajiri wao.
Miongoni mwa maovu hayo ni pamoja na kulipwa ujira mdogo, kufanyishwa kazi ngumu kwa saa nyingi, kukosekana kwa huduma za kijamii, ubaguzi na upungufu mwingine.
Mwaka 1910 nchi hiyo ya Marekani ikakubali kupitisha siku maalum kwa wanawake ili kutafakari haki zao za binadamu hivyo kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo yalifanyika mwaka 1911.
Kwa Kuenzi harakati hizo Umoja wa mataifa ulipoanzishwa mwaka 1945 ulipitisha machi 8 kuwa siku ya kimataifa ya wanawake.
Kwa upande wa Tanzania mwaka 2005, Serikali ilitoa agizo kuwa siku hiyo itakuwa ikiadhimishwa katika ngazi ya kitaifa katika kila baada ya miaka mitano, lengo likiwa ni kutoa muda wa kutosha wa utekelezaji wa maazimio na mipango mbalimbali ya kitaifa.
Kwa muda wa miaka mitatu mfululizo sasa maadhimisho hayo yamekuwa yakifanyika katika ngazi ya kimkoa na kiwilaya ambapo wanawake wamekuwa wakipata fursa ya kujadiliana mambo mbalimbali yanayowahusu.
Mwaka huu suala la mgawanyo wa raslimali fedha kijinsia na uwezeshaji wa wanawake; ni msingi wa maendeleo limepewa nafasi kubwa katika maadhimisho hayo na hivyo kubeba kauli mbiu ya mwaka huu.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Magreth Sitta anasema kauli mbiu hiyo ni muhimu sana kwa kuzingatia hali halisi iliyopo katia jamii ya kitanzania.
Umuhimu huo unaonekana katika maeneo mbalimbali ambapo kundi hilo linalobeba asilimia 51 ya Watanzania wote, limeachwa nyuma katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.
\"Kama hali iko hivyo, kwa nini kundi hili liwe limeachwa nyuma katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.
Anasema wanawake wanakabiliwa na tatizo la elimu na afya duni na vifo vya akinamama na watoto wakati wa kujifungua.
Takwimu za sekta ya afya mwaka jana zinaonyesha kuwa wanawake 578 kwa kila 100,000 wanakufa kwa vifo vya uzazi.
Anasema pia uhaba wa ajira umekuwa tatizo sugu ambapo takwimu za mwaka jana zinaonuyesha kuwa wanawake asilimia 12 na wanaume asilimia 9 hawana ajira.
Kati ya wanawake milioni tatu na nne wapo katika sekta isiyo rasmi yenye mitaji na tija ya chini, mazingira ya kazi hatarishi na kutokupata huduma za kibiashara.
Waziri huyo anazitaka asasi za kifedha ziwanufaishe wanawake na wanaume bila kujali tofauti za kijinsia na mahusiano ya kijamii ya wanawake na wanaume.
Anasema katika kufanikisha hii hakuna budi kufanya uchambuzi wa kijinsia wa kina kwa kutumia takwimu sahihi za wanaume kutokana na tofauti za mahitaji yao.
``Hapa msisitizo ni kwa kiasi gani bajeti za programu, miradi au shughuli zinazingatia mahitaji tofauti ya wanawake, wanaume, watoto wa kike na wa kiume katika ngazi zote,`` anasema Waziri huyo.
Anasema kuwa wizara yake katika mwaka huu itaweka msisitizo katika maeneo matatu ikiwa ni miongoni mwa mambo ambayo Tanzania inaendelea kuyashughulikia kati ya 12 yaliyoainishwa katika Mkutano Mkuu uliofanyika Beijing mwaka 1995.
Anayataja miongoni mwa uwezeshaji wa wanawake ikiwa ni pamoja na elimu na upatikanaji wa mitaji ili kuimarisha ujasiriamali,kuongeza usawa katika vyombo vya maamuzi ikiwa ni pamoja na vile vya uwakilishi na uongozi wa ngazi zote na kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike na kiume.
Anasema suala la upatikanaji wa usawa kati ya wanaume na wanawake utatokana na mgawanyiko sawia wa raslimali fedha kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika ngazi zote za utekelezaji.
Hata hivyo, anasema mgawanyo wa raslimali fedha kijinsia na uwezeshaji wa wanawake bado linakabiliwa na changamoto nyingi.
``Tafiti zinaonyesha kuwa utekelezaji wa sera, mikakati na programu mbalimbali kwa muda mrefu unakabiliwa na changamoto ya wanawake kuendelea kubaki nyumba kiuchumi, kijinsia na kisiasa,``anaasema.
Kwa kupigana kwa pamoja katika mambo mbalimbali tunaweza kuona harakati za mwanamke katika kujikomboa zinafanikiwa.
|