28 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kibaki, Odinga leteni amani sasa
 
2008-02-28 10:22:26
Na Mhariri

Katika gazeti hili kuna habari zinazoonekaa ni njema kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, ambaye amekaririwa akisema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika usuluhishi wa mgogoro wa kisiasa nchini Kenya.

Rais Kikwete yuko nchini Kenya katika kuongeza nguvu za kumaliza mgogoro huo wa kisiasa ambao pia ulichukua sura ya kikabila.

Katika mgogoro huo, zaidi ya watu 1,000 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 300,000 kukimbia makazi yao.

Aidha, mzozo huo umerudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi ya nchi hiyo na kuathiri pia nchi za jirani tukiwemo sisi Tanzania katika baadhi ya sekta ikiwemo utalii.

Habari nyingine ya kufurahisha ni kwamba chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM) jana kimesitisha maandamano ya nchi nzima yaliyotakiwa kufanyika leo.

Kwa wiki nzima ODM ilisema itafanya maandamano hayo kama itafika leo bila muafaka wa mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa mataifa, Kofi Annan.

Mpaka sasa inaelezwa kuwa mambo makubwa ya msingi yameshakubaliwa na pande zote mbili, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa cheo cha Waziri Mkuu kilichokuwa kinadaiwa sana na wapinzani.

Kinachogomba kwa sasa ni madaraka atakayokuwa nayo waziri mkuu kikatiba ambaye bila shaka anatakiwa awe Bw. Raila Odinga.

Kingine ambacho pande mbili katika mzozo huo hazijakubaliana sawasawa ni idadi ya mawaziri ambayo kila upande unatakiwa kutoa.

Halikadhalika suala la kurudiwa uchaguzi endapo serikali ya mseto itakayoundwa itashindwa kufanya kazi ni jambo jingine ambalo halijapatiwa ufumbuzi.

Kwa kifupi, Kenya wanakwenda vyema lakini masuala hayo matatu yanahitaji maamuzi magumu na wahusika wakuu ni Odinga na Kibaki.

Tunajua kwamba viongozi hawa wawili wamekuwa wakipata miito mingi ya ndani na nje ya kuwataka wafikie mwafaka haraka. Tunazishukuru nchi za Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya ambazo zimekuwa msitari wa mbele kuhakikisha Kenya inarudisha amani yake.

Sisi tunawaomba Kibaki na Odinga wahakikishe kwamba wanaikoa Kenya isitumbukie tena katika ghasia na vita kwa kuendelea na misimamo yao mikali.

Kusuluhishwa kunamaanisha kukubaliana hata kama hujaridhika au hata ikibidi kupoteza maslahi yako binafsi na ya chama chako na kikubwa zaidi ni kuangalia maslahi ya watu na nchi yako.

Hili ndilo ambalo wawili hawa, Mabwana Mwai Kibaki na Raila Odinga wanatakiwa kukikubali kwa kuwa yanayotafutwa ni maslahi ya Wakenya na si ya mtu mmoja mmoja.

Ikumbukwe haina maana kuwa na mazungumzo ya upatanishi kwa muda mrefu bila kuwa na ufumbuzi wa haraka.

Wakati umefika wa kuwa na maridhiano kwa ajili ya kudumisha umoja wa kitaifa na kulinda mali na maisha ya raia ambao ndiyo wapiga kura badala ya kung`ang`ania hoja zinazoonekana ni za maslahi binafsi.

Tunampongeza Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN) Dk. Kofi Annan na washirika wengine, Rais mstaafu Bw. Benjamin Mkapa na mke wa Rais wa Afrika Kusini, Bi. Graca Machel kwa kazi nzito iliyofanyika.

Tunatarajia jitahadi za Mwenyekiti wa AU na washirika wengine wa usuluhishi zifungue sura mpya ya Kenya badala ya kuendelea kusikia taarifa kuwa mazungumzo ya usuluhishi yanaendelea bila kuuona ukomo ama yamesimama.

Tunaliona suala la Kenya kwamba si kubwa na la kuhofia kama uasi na vurumai za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, si gumu kama lilivyo la Sudan ya Kusini wala halifanani na mgogoro sugu wa Somalia na hivyo ni imani yetu kwamba amani itakuja kwa majirani zetu na sisi wa Afrika Mashariki tufurahie uhusiano na amani iliyokuwepo kabla ya uchaguzi wa Desemba mwaka jana.

Kazi kwenu Odinga na Kibaki. Ufunguo wa amani mnao nyiye.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.