|
Mazao ya kilimo hai yana uhakika wa soko
2008-02-28 10:21:33
Na Sharon Sauwa
Kwa muda mrefu sasa wakulima wengi wamekuwa wakihamasishwa kulima kilimo Hai (kisichotumia kemikali) nia ikiwa ni kulinda afya za walaji. Katika makala hii Mwandishi Wetu Sharon Sauwa anaelezea zaidi kama alivyozungumza na Asasi ya Kilimo Hai Tanzania (TANCET)
WENGI wa wakulima nchini wamekuwa wakitumia mbolea za viwandani katika kilimo, hali inayotokana na watu kutoelewa madhara ya kilimo hicho.
Madhara haya hayaishii kwa wakulima tu, bali hata kwa walaji ambao huathirika kiafya kutokana na kemikali zilizotumika katika kukuza mimea hiyo ama kuzuia wadudu waharibifu mashambani.
Bi. Hawa Kimolo ni mjumbe wa Asasi ya Kuendeleza Kilimo Hai nchini (TANCET) ambaye pia ni mkulima katika eneo la Kibaha mkoani Pwani.
Anasema anajivunia kilimo hicho kwa kuwa sasa anaweza kunufaika na familia yake kwa kula matunda, mbogamboga na kuku ambazo hazijazalishwa kwa kutumia kemikali.
Lakini unapododosa ni kwanini aliamua kujiunga na kilimo hicho anasema, kinamwezesha kupata mazao ambayo hayana athari kwa afya ya binadamu na pia kinamwezesha kuwa na kilimo endelevu katika ardhi anayoitumia.
Bi. Hawa Kimolo anasema hicho ni kinyume na ardhi ambayo imewekwa kemikali (mbolea) kwa ajili ya kukuzia.
``Wakati unaanza kilimo hiki cha kutotumia kemikali unaona kuwa uzalishaji unakuwa mdogo lakini kwa kadri unavyoendelea uzalishaji unakuwa mkubwa,``anasema Bi. Hawa.
Anasema kujikita katika kilimo hicho ambacho anasema mwanzoni unaweza kukiona kuwa hakina manufaa, kumemwezesha kuwa na uhakika wakupata mbogamboga, matunda na hata mayai yasiyo na kemikali.
Anasema kilimo hai ni chaguo la wakulima wengi, kutokana na kuwashirikishi, kuhofia gharama kubwa na kutojua matumizi ya kemikali mbalimbali zinazotumika mashambani.
Pia anasema ni kilimo cha asili toka enzi za mababu ambapo kutokana na kutopatikana kirahisi mbolea hizo na madawa, walikuwa wakilima kwa mfumo wa kilimo hai.
Anasema kilimo hicho hakina wakulima wakubwa bali kinalimwa na wakulima wadogo wadogo hapa nchini.
Anasema tayari wameanza uhamasishaji katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya wilaya za Mkuranga na Kibaha mkoani Pwani.
Bi. Hawa anasema mfumo maalum ulioandaliwa unaojulikana kama PGS, ni mfumo rahisi ambao umeandaliwa kwa ajili ya kurahisisha ukaguaji wa kilimo hicho.
Katika mfumo huo jirani yako ndio anakuwa mkaguzi wa kwanza na baadaye mkaguzi kutoka nje.
Anabainisha kuwa hatua hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo lugha yao inakuwa moja kwa wakulima kuhusiana na aina ya mfumo wa kilimo wanaotaka kutumia.
``Hapa hakuna kudanganyana wote lazima mtasema katika lugha moja katika kilimo hiki hai ili muweze kuendelea nacho,``anasema Bi. Hawa.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TANCET, Bw. Jordan Gama, anasema makampuni 23 yameingia mkataba wa kuzalisha mazao yanayotokana na kilimo hai.
Anasema makampuni hayo yanafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la watu wa Sweden, (SIDA), chini ya mradi unaojulikana kama EPOPAR ambao ulianza mwaka 1998.
Anasema makampuni hayo, yameingia mkataba wa kuzalisha mazao aina ya kakao, pamba, kahawa, karanga, ufuta na kwamba mafanikio yamejionyesha ambapo makampuni hayo yameanza kuuza mazao hayo nje ya nchi.
Anasema soko la uhakika lipo katika nchi za Marekani, Japan na Ujerumani na bado tunafanya jitihada za kupanua soko.
``Hitaji la soko ni kubwa sana, bado hatujaweza kulimudu, tumekuwa tukipokea email kutoka nchini Marekani, Japan na Ujerumani zikitaka mazao haya lakini tumeshindwa kuwatimizia mahitaji yao,``anasema Bw. Gama.
Anasema bado wakulima nchini hawajaweza kuzalisha bidhaa zinazotosheleza, hali ambayo inaleta ugumu katika suala zima la kumudu mahitaji.
Anawahamasisha wakulima kulima kilimo hicho ili waweze kupata soko ya mazao yao na kuondokana na tatizo la ukosefu wa soko.
Anasema wao kama TANCET wana miadi moja wilayani Karagwe mkoani Kagera.
Anasema baadhi ya wawekezaji wamekuja kuwekeza katika kilimo hicho hai ambapo mkoani Morogoro wanashamba linalojulikana kama KIMANGO, linalolima mchachai, choya aukwa jina lingine rosella (kinywaji cha kuongeza damu).
Lakini anasema pamoja na juhudi hizo wamekuwa wakishiriki katika maonyesho mbalimbali ya bidhaa hizo, hatua ambayo inalenga kwenye kupanua soko.
Anasema kwa sasa hivi wanapigania soko la Latin Amerika na Asia na kwamba soko hilo linakua kwa kati ya asilimia 15 na 20 kila mwaka.
``Tutashiriki katika maonyesho mbalimbali na Februari mwaka huu tunaelekea nchini Ujerumani kuonyesha bidhaa zetu,``anasema.
Watanzania hao wanapeleka katika maonyesho hayo viungo mbalimbali kutoka visiwani Zanzibar pamoja na Vanila inayolimwa mkoani Kagera.
Anasema bidhaa nyingi wanazopeleka ni za kukausha lakini zinatokana na kilimo hai.
Anasema hatua hiyo inalenga katika kuhakikisha kuwa wanapata soko katika nchi za Latin Amerika na Asia.
Bw. Gama anasema maonyesho ya mwaka huu ni tofauti na yaliyotangulia kwani Afrika nzima itaweza kushiriki katika banda moja.
Awali anasema Afrika ilikuwa ikionyesha katika mabanda tofauti. katika mabanda ya nchi nyingine.
Anaongeza kuwa Tanzania imetoa washiriki 24 kutoka makampuni 14 na kwamba wote hao watakwenda kuonyesha bidhaa za kilimo hai ambazo ziko katika mfumo wa kukaushwa na kadhalika.
Hata hivyo Bi. Hawa anasema bado soko la ndani lina mahitaji makubwa na kwamba yeye amekuwa akisambaza bidhaa zake anazozalisha katika soko la ndani.
Ingawa ni ukweli usiopingika kuwa katika nchini zinazozalisha kwa wingi vyakula, hutumia kemikali mbalimbali lakini afya ya mlaji ni jambo muhimu.
Changamoto iliyopo nchini ni kuhakikisha kuwa wakulima wanalima kwa kutumia mfumo wa kilimo hai, sambamba na kufanikiwa kuzalisha mazao mengi yenye ubora.
Lakini kama elimu ikitolewa katika maeneo mbalimbali na wakulima kunufaika na mfumo huo, suala la kutumia kemikali litapungua na hatimaye kutokomea.
|