27 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Walimu wazingatie maadili
 
2008-02-27 08:42:38
Na Haji Mbaruku

Moja ya matatizo yanayochangia kwa kiasi kikubwa kushusha taaluma ya elimu ya msingi hapa nchini ni suala la utovu wa nidhamu unaofanywa na baadhi ya walimu.

Sijui kwanini walimu wetu wamefikia hatua hii.

Zamani haikuwa kazi rahisi kusikia mwalimu amempa mimba mwanafunzi ama ameachishwa kazi kwa ulevi.

Pamoja na mazingira magumu waliyokuwa nayo wakati ule, bado walimu wetu waliheshimu kazi zao.

Wakati ule walimu waliipenda kazi yao na walichukulia kufaulu kwa mwanafunzi kama kipimo cha uwezo wao wa kufundisha mashuleni.

Mwalimu wa zamani alijisikia raha sana kuona mwanafunzi wake amefaulu bila kujali kama alipata maslahi mazuri kazini ama la.

Alichukulia kufaulu kwa mwanafunzi shuleni kama moja ya mafanikio yake maishani mwake.

Hata mwanafunzi mwenyewe alimuogopa mwalimu, alimheshimu na kumnyenyekea kama mzazi wake.

Mwanafunzi alipokuwa akimuona mwalimu, alishikwa na hofu na hata nidhamu ya kutosha .

Sasa hivi ni tofauti kabisa ambapo mwanafunzi wa shule ya msingi hamuogopi mwalimu, mwanafunzi anaweza kujibizana na mwalimu wake.

Lakini sio sasa hivi ambapo uchunguzi unaonyesha kuwa wengi wanakimbilia kwenye ualimu kwa vile hawana jinsi.

Kutokana na ukosefu wa ajira hapa nchini, baadhi ya watu wanaona ualimu ndio sehemu ya kukimbilia.

Jaribu kufuatilia, wengi wanaoingia kwenye vyuo vya ualimu kusomea ualimu ngazi za chini wanakuwa na matokeo mabaya mashuleni.

Sijaona mtu mwenye daraja la kwanza ama la pili akaenda kusomea ualimu ili akafundishe shule ya msingi.

Hata hivyo, hiyo sio mbaya.Mbaya zaidi ni pale elimu inapogeuzwa kuwa mradi.

Hivi sasa baadhi ya walimu wamegeuza taaluma hiyo kama mradi.

Tangu serikali ilipopiga marufuku tuisheni basi walimu wetu wakishirikiana na kamati za shule, wamebuni njia nyingine mbadala wa tuisheni.

Hivi sasa shule nyingi za msingi hapa nchini kwa kushirikiana na kamati za shule, zimeweka utaratibu kuwa wanafunzi wote watake wasitake, watasoma masomo ya ziada mara baada ya kumalizika kwa masomo ya kawaida.

Wenyewe hata hivyo wanasisitiza kuwa hiyo sio tuisheni.

Kwa mfano, kama masomo ya kawaida yatamalizika saa 8.00 mchana, masomo ya ziada yataanza saa 8.30 mchana hadi saa 12.00 jioni.

Na katika masomo hayo, kila mwanafunzi anapaswa kulipia shilingi 500 kwa siku ama kwa mwezi shilingi 5,000.

Yaani michango imekuwa mingi kupita kiasi katika shule za msingi.

Baadhi ya wazazi wanasema kuwa elimu ya msingi sasa hivi imekuwa na gharama sana ukilinganisha na elimu ya sekondari.

Mzazi mmoja anayesomesha mtoto wake katika shule moja ya msingi pale Yombo analalamikia kuhusu mwenendo wa shule hiyo.

Anasema kuwa, shule hiyo ina kawaida ya kumaliza masomo kuanzia saa 5.00 asubuhi ambapo wanafunzi wote wanatakiwa warudi majumbani mwao na baadae saa 8.00 mchana wanarudi tena kuanza masomo ya ziada ambayo ni lazima mwanafunzi alipie shilingi 500 ama 5000 kwa mwezi.

Mzazi huyo anakiita kitendo hicho kuwa ni mradi akihoji kwanini masomo hayo ya ziada yasifundishwe kwenye muda wa kawaida.

Katika hali kama hiyo mtoto au ndugu yako anapomaliza shule unashukuru kutokana na ukweli kuwa michango ni mingi katika shule hizo na wakati mwingine unashindwa kumudu.

Wanafunzi wanatozwa kulipia pesa za masomo ya ziada bila kujali uwezo wa wazazi wao.

Mzazi atapata wapi shilingi 500 ya kila siku katika kipindi hiki ambacho taifa limegubikwa na tatizo la mfumuko wa bei ambapo upatikanaji wa mahitaji mengi ni taabu tupu.

Ni hivi majuzi tu imeelezwa kuwa kumekuwepo na malalamiko mbalimbali katika tume ya utumishi wa umma dhidi ya utovu wa nidhamu unaofanywa na baadhi ya walimu.

Katibu mkuu wa utumishi wa umma, Bi.Thecla Shangali anasema kuwa tume imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali dhidi ya uvunjaji wa maadili kwa walimu.

Anasema kuwa, tume yake imepokea jumla ya mashauri 35 kutoka idara ya walimu kuhusu makosa ya kinidhamu yanayofanywa na baadhi ya walimu ambayo yanaendelea kuchunguzwa.

Sasa kama walimu wetu ambao tumewapa dhamana ya kuhakikisha watoto wetu wanakuwa na nidhamu kumbe wao ndio wanaoongoza kwa utovu wa nidhamu, tutegemee nini watanzania?

Walimu wanatakiwa wawe mfano bora wa kuigwa na jamii, sasa inashangaza kuona wao ndio watovu wakubwa wa nidhamu.
Taifa linapokuwa na wasomi wazuri kama vile wachumi, wahasibu, wahandisi, wakandarasi ni matokeo ya walimu wetu.

Sasa kama walimu wetu sasa hivi wanashindwa kuzingatia maadili, ni vigumu kwa watoto wetu kufanikiwa katika masomo yao.

Ni vyema kwa maofisa wa elimu kufanya ukaguzi mashuleni kubaini vitendo hivi kabla mambo hajaharibika zaidi.

Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa inachunguza tabia za walimu kabla haijafikia hatua ya kuwaajiri ili wasije wakawaharibu watoto wetu.

Vile vile iangalie mradi huu unaofanywa na walimu kwa kushirikiana na kamati za shule ambao unaumiza sana wazazi mashuleni.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.