27 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Walimu sasa walipwe haraka
 
2008-02-27 08:40:57
Na Mhariri

Bila shaka walimu wengi wana kila sababu ya kutekeleza majukumu yao kwa furaha kutokana na habari zilizotangazwa na serikali juzi kwamba watalipwa zaidi ya sh. bilioni nane ikiwa ni malimbikizo ya madai yao ya siku nyingi.

Madeni hayo ni yale yanayohusu likizo, matibabu, uhamisho na posho nyingine.

Mapema mwezi huu walimu kupitia Chama cha Walimu Tanzania (CWT) walitishia kuitisha mgomo nchi nzima katika kuishinikiza serikali kuwalipa mbalimbikizo yao.

Walimu hao walikuwa wametishia kugoma ifikapo Mei Mosi mwaka huu.

Tunaipongeza serikali kwa dhati kwa kuitikia kilio cha walimu wetu kwa kutenga kiasi hicho cha fedha kuwalipa mafao yao.

Kwa kweli kilio cha walimu kimekuwa ni cha siku nyingi,lakini wamekuwa wakipigwa danadana na kupewa visingizio ambavyo hakika vilikuwa na maudhi.

Wakati tunaipongeza serikali ni vizuri tukaliangalia upya na kwa undani zaidi suala zima lililofanya malimbikizo hayo yakafikia mabilioni ya fedha.

Suala linalojitokeza moja kwa moja ni kwamba bajeti inayotengwa kwa ajili ya maslahi ya walimu ama haitoshi au inatumika kwa ajili ya shughuli nyingine.

Tuchukue mfano wa posho ya likizo na ya uhamisho.

Inakuwaje mwalimu aende likizo, ambayo inaeleweka na siyo dharura, asipewe fedha za likizo?

Au inakuwaje mwalimu, kwa mfano, ahamishwe kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine bila kulipwa fedha za uhamisho?

Huyu mwalimu tunamtazamia afanye kazi zake kwa uadilifu wakati serikali haimtendei haki?

Katika nchi yetu walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana.

Shule nyingi, hasa za msingi,zimejengwa vijijini ambako mawasiliano ya barabara na mengineyo ni magumu. Hulazimika kutembea mwendo mrefu kwenda na kurudi mashuleni.

Na pale shuleni mazingira ya baadhi ya shule zetu ni ya kukatisha tamaa.

Baadhi ya madarasa hayana madawati na mengine hayana hata madirisha. Mvua ikinyesha inaingia ndani na pa kujificha hakuna.

Baadhi ya shule hazina hata ofisi kwa ajili ya walimu. Ama wanaamua kukaa darasani wanakofundisha, au chini ya mti kusahihisha madaftari.

Lakini wengi wao wanajituma kufundisha watoto wetu kwa bidii zote.

Katika baadhi ya shule matunda ya bidii zao yanaonekana wazi kwa jinsi ambavyo watoto wanafanya vizuri katika masomo yao.

Tunachukua nafasi hii kuwapongeza walimu nchini kote kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwaelimisha watoto wetu.

Tunatoa pongezi za pekee kwa wale waliokuwa wamepunjwa maslahi yao kwa uvumilivu wao wa muda mrefu.

Hata hivyo, tungependa kutoa tahadhari kwa wale watakaokabidhiwa dhamana ya kugawa fedha hizi.

Tunaambiwa kwamba kwa upande wa walimu wa sekondari watalipwa kupitia makao makuu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Kwa upande wa walimu wa shule za msingi watalipwa kupitia halmashauri za wilaya.

Uzoefu unaonyesha kuwa fedha zilizotengwa kwa jambo fulani zimetumika kwa ajili ya jambo jingine.

Tatizo hili liko zaidi katika baadhi ya halmashauri za wilaya.

Katika hili tungependa kutahadharisha mapema kwamba ni lazima utaratibu ulio wazi uwekwe kuhakikisha kwamba fedha za malimbikizo ya madeni ya walimu zinawafikia walengwa mapema iwezekanavyo.

Serikali imeshatenga fedha kulingana na idadi ya walimu wanaodai maslahi yao.

Kwa hiyo orodha kamili ipo na kiasi wanachodai kinaonekana wazi katika orodha hiyo.

Watakaokabidhiwa dhamana ya kuwalipa, walipe, tena haraka sana.

Tunajua urasimu uliopo huko wilayani lakini usitumike kama kisingizio cha kuchelewesha kuwalipa walimu malimbikizo yao ya muda mrefu. Tusiwakere tena kwa kuwaambia ``nenda njoo kesho``.

Tuna hakika walimu wakifanya kazi yao kwa furaha watoto wetu nao watasoma kwa furaha na kuafanya vizuri katika masomo yao

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.