|
Utoaji wa elimu ujengewe mstakabali mpya
2008-02-26 09:59:06
Na Mwandosha Mfanga
Kuna usemi ambao umekuwa ukitumika sana katika masuala ya elimu; nao ni unasema, ``Kama unadhani kuwa elimu ni aghali, basi jaribu ujinga,`` Ukitanzama mizania ya matumizi ya kila Mtanzania leo hii utaona kuwa usemi huu haupo mbali na hali halisi kwa miaka kadhaa sasa.
Wananchi, na hasa wazazi pamoja na serikali wamekuwa wakipambana na ujinga kila siku kwa kutumia njia za kila aina wakiwa wanajua kuwa ujinga ni moja kati ya matatizo yanayoikabili nchi na watu wake lakini haielekei kuonyesha kuwa kuna kazi yoyote kubwa iliyofanyika.
Bado ujinga upo katika kiwango cha juu sana katika nchi hii, hata miongoni mwa waliokwenda shule na elimu bado inaendelea kuwa aghali zaidi hususan kutokana na taasisi mbalimbali za elimu kupandisha gharama kila kukicha.
Ni wazi kuwa ukitazama suala la elimu utaona kuwa muelekeo wa utoaji wa elimu katika nchi hii unaonyesha kuwa umepogoka kwa kiwango kikubwa.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mathalani, kilitangaza juma lililopita kuwa kinaongeza gharama za elimu kwa asilimia 80 kuanzia mwaka wa elimu unaoanzia Septemba hii.
Kwa mujibu wa mapendekezo yaliyotolewa Kenya vyombo vya habari, ada itapanda kutoka Shillingi 722,000 zinazolipwa sasa kwa daraja la chini na kufikia Shillingi 1.3 milioni, wakakti ambapo kwa daraja la juu inapendekezwa kuwa zipande kutoka kiwango cha sasa cha Shillingi 1.22m/- na kufikia Shillingi 2.52m/- kwa mwaka.
Hakuna shaka kuwa kuongezeka kwa ada katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutafanya ada za masomo katika vyuo vingine vya Serikali kuongeza ada kwa vile tayari vitakuwa vimeshaona mfano kutoka chuo hicho.
Ni wazi pia kuwa vyuo vinavyomilikiwa na watu binafsi vitafuata kutokana na ya le yanayojiri katika vyuo vya umma kwa kuongeza ada katika vyuo hivyo licha ya kwamba tayari vilikuwa vimeshaongeza mwanzo wa mwaka uliopita na vingine katikati ya mwaka.
Haiyumikini kama nyongeza hizi za ada zitaishia kwenye uwanja wa elimu tu, na hususani elimu ya juu au zitasambaa katika uchumi wote kwa ujumla na kusababisha ongezeko la mfumoko wa bei.
Hii ni moja kati ya hofu zisizoweza kuepukika ambazo zinautanza uchumi wetu kwa sasa, na hakuna anayeelewa kuwa hatima ya hili litakuwa nini.
Hata hivyo ni wazi kuwa kuongezeka kwa ada za mamsomo hakutaathiri mambo kama vile matumizi katika maeneo kama vile matumizi ya familia ya chakula, nyumba, nguo, abayo bila shaka yatakuwa juu zaidi.
Mfano mzuri unaonekana kwa wanafunzi wanaosoma katika shule binafsi za awali, msingi na sekondari ambapo ada za masomo na matumizi mengine zimekuwa zikiongezeka kila mwaka na kuwa juu sana tofauti na kwa wale wanaosoma katika shule za serikali ambapo gharama ni ndogo.
Kusema ukweli ni kuwa kuna tofauti kubwa kati ya ada za masomo kwa wanafunzi wanaosoma katika shule za watu na taasisi binafsi na wale wanaosoma katika shule zinazomilikiwa na Serikali.
Pengine tatizo la elimu inayotolewa na shule za serikali ni kuwa wakati mwingi ni ya kiwango cha chini, hususani kutokana na kukosekana kwa nyenzo na vifaa na walimu wa kutosha.
Lakini kama kikwazo hiki kingeondolewaa, shule za Serikali zingekuwa mahali pazuri sana pa kuwapeleka watoto wetu na sio katika shule zinazomilikiwa na watu na taasisi binafsi ambapo nyingine ni za ubabaishaji.
Ingawa Wizara ya Elimu na Mafunzo imeweka kiwango cha Shillingi 380,000 kwa mwanafunzi kwa mwaka katika shule za sekondari, wamiliki wa shule binafsi wameshavuka kiwango hiki zaidi ya mara tatu au nne.
Nyingi ya shule zinazomilikiwa na watu na taasisi binafsi, hata kama zinatoa elimu duni kiasi gani, zinatoza ada zaidi ya mara mbili au tatu ya kiwango hicho cha juu kilichoidhinishwa na Serikali, na pengine ni kutokana na hili Naibu Waziri wa Elimu na Ufundi Stadi, Mwantumu Mahiza, aliwaambia wazazi wakatae shule zinazotoza ada kubwa.
Hata hivyo hakukuwa na hata mzazi mmoja aliyekubaliana na ushauri huo. Shule zilizo nyingi hivi sasa hudai ada kwa mamilioni, ziwe ni za awali, msingi au sekondari, na hivvyo kufanya tofauti kati ya shule na vyuo kuonekana kuwa hazipo kabisa.
Yatosha tu kusema kuwa elimu nchini Tanzania ni aghali sana tena sana kuliko hata katika nchi jirani, hii ikiwa ni sababu moja kubwa kwa baadhi ya wazazi kupeleka watoto wao huko kusoma.
Lakini hilo sio tatizo pekee. Pengine athari kubwa kitaifa kwa ada za elimu kuwa kubwa ni kuwa Watanzania walio wengi ambao wanaotaka kusoma watakwazwa na kigezo cha gharama licha ya kuwa nia wanayo.
Hii itakuwa ni kikwazo kikubwa sana katika kulikomboa taifa dhidi ya ujinga-moja ya matatizo makubwa matatu yanayolitanza taifa hili tangu uhuru.
Kutokana na haya yote ni wazi kuwa inabidi utoaji wa elimu nchini unjengewe mstakabali mpya kabisa utakaowezesha kila mtu kulingana na rika, jinsia na kigezo kingine aweze kupata elimu.
Hii inawezekana endapo tu kutakuwa na sera kabambe inayoanisha matakwa na wajibu wa taifa na nini ambavyo kila raia anavoweza kufaidika.
Kwa manzili hayo, mapendekezo yaliyotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu kuongeza ada za masomo yangesubirishwa kwanza-hususan ikitiliwa maanani matatizo yanayolikabili taifa hivi sasa.
Kwa vile sasa masuala yote yanayohusu elimu yanashughulikiwa na wizara moja, ingekuwa vama kama ingeundwa tume maalum ya Rais itazame namna ambavyo elimu ingetolewa kwa kila Mtanzania kwa gharama nafuu.
Ikiwa ni pamoja na kuoanisha viwango vinavyotozwa isiwe vile vya shule za msingi vinapita vya vile vinavyotozwa vyuo vikuu.
Haiingii akilini kuwa ada za elimu katika shule za awali, msingi na sekondari ni kubwa kuliko katika vyuo mbalimbali. Hii haiyumkiniki kwa nchi ambayo ni changa na inataka kuelimisha watu wake.
Inawezekana kabisa kwa shule zilizojengwa kwa Tanzania kwa sasa ikiwa ni karibu wastani wa shule zaidi ya moja ya msingi kwa kila kijiji kwenye nchi yenye vijiji zaidi ya 10,000 na shule za sekomdari karibu 4,000 (angalau moja kwa kila kata) kutoa elimu kwa kutumia shule za umma pekee.
Ni vema tujiulize kama kwa kiwango hicho cha shule za umma zilizopo, kuna haja ya kuwa na shule za waatu binafsi? Shule zinazoendeshwa na jumuiya za kidini pengine sawa, lakini sio shule zinazoendeshwa na watu ambao madhumuni yao ni kuchuma tu badala ya kusomesha taifa na walimwengu.
Tukilitazama suala la elimu na maadili yanayotakiwa katika kutoa elimu, kuna haja kweli ya kukabidhi amali hii ambayo ni muhimu sana katika maisha ya binadamu kukabishiwa kwa mtu binafsi ambaye matakwa yake ni wazi yanaonekena kupishana na matakwa ya jamii?
Ukitanzama utoaji wa elimu nchini utaona pia kuwa kuna mitaala mbalimbali inayotolewa na shule zilizopo huku kila shule ikijaribu kuonyesha namna ambavyo inavyoweza kushindana na nyingine bila pengine kuwa na vigezo maalumu wakati kila raia anayo haki ya kupata sawa na raia wengine kutokana na raslimali za nchi?
Yapo matatizo mengi katika medani ya elimu, lakini tatizo lililo kubwa kuliko yote ni kuwa ni kwa nini Watanzania wanakuwa kinara katika kubiasharisha elimu wakati ambapo bado inabaki kuwa ndiyo amali pekee ya maisha yao, taifa lao na dunia kwa ujumla.
Kuna haja ya kufanya mabadiliko na kuongoza mabadiliko haya kutoka katika vurugu hizi zilizosheheni katika utoaji wa elimu. Mabadiliko haya ni lazima yatazame sekta nzima ya elimu na kuanisha kuwa ni vipi raslimali za nchi hii zitatumika kuhakikisha kuwa tunajenga taifa lililoondokana na ujinga.
Hii ina maana kuwa serikali ni lazima pia itazame bejeti yake na kuona uwezekano wa kubadili mtazamo wa kuendesha shughuli zake na za wananchi kwa kutumia maguvu (majeshi) na badala yake ielekeze raslimali katika kuelimisha watu ili itumie maguvu kidogo kwa vile watu wengi watakuwa wamekwenda shule na wanatumia akili zaidi kuliko nguvu.
Hiki ndicho kinachotakiwa ili taifa liweze kuendelea. Vinginevyo tutakuwa tunaimba nyimbo kuhusu maendeleo ambazo hakuna muitikiaji.
Ni vema tusisahau, kama unadhani elimu ni aghali, basi jaribu ujinga.
|