|
Semina elekezi: JK anajichanganya, au ni dira halisi?
2008-02-25 08:39:00
Na Ani Jozeni
Mara baada ya kuapisha Baraza jipya la mawaziri katika Ikulu ndogo mjini Dodoma, Rais Jakaya Kikwete alitangaza kile kilichoitwa ``kupiga marufuku`` semina elekezi, jambo ambalo lilistua kidogo baadhi ya watu.
Kwa maana yake `sanifu,` kupiga marufuku kunafanyika kuhusu jambo ambalo linatokea kawaida, yaani lina mkondo wa shughuli za kila siku, na kwa jumla linakubalika kisheria.
Huwa linaweza kuwa na utata kimaadili, likavumiliwa, au ``kupigwa marufuku.``
Sasa kwa maana hiyo ni vigumu kuona jinsi \'semina elekezi\' zilivyo jambo la kawaida, zimekuwa na utata kimaadili, zimevumiliwa; sasa zinapigwa marufuku na Mkuu wa Nchi, kwa tamko lililoashiria aina fulani ya hali ya hatari.
Wale waliopokea tangazo hilo kwa mikono miwili walisema semina hizo zilikuwa ni chanzo cha kufuja ``mamilioni ya fedha`` na hazikuwezesha utendaji wowote bora.
Ni kama vile JK ameshtuka kuwa hiyo ni mbinu tu ya ubadhirifu, nukta.
Kuwa hayo ndiyo mawazo ya JK sasa hivi haina ubishi, kwani ameelekea kukiri hivyo, kwani ``kupiga marufuku`` ni hatua ambayo inachukuliwa kwa mikutano haramu ya kuashiria kuvuruga amani, au kupika pombe kama gongo.
Si kwa suala `nyeti` kama wakuu wa idara na wizara za serikali, na wale wa mikoa na wilaya, kuketi kujadili mambo kwa kina, ili kufanya kazi kwa mtazamo wa pamoja, na si kila mmmoja akicheza ngoma anayoijua mwenyewe.
Hayo ndiyo madhumuni ya `semina elekezi;` iweje JK aongee kama kwamba hafahamu hilo?
Kwa vile JK anafahamu hilo, na katu hawezi kuwa miongoni mwa wale wanaoona `semina elekezi` ni mahali tu pa kufuja fedha, yaani kukaa kwenye hoteli safi za kitalii, kula na kunywa, kupewa `masurufu ya ziada, na kukuta mshahara unangoja ofisini baada ya wiki mbili, tuseme sababu zake ni zipi?
Labda kwa haraka tuseme kuwa wale waliopo serikalini kimsingi ni wale wale, kwa vile `semina elekezi` za wakati ule zilijumuisha manaibu waziri, na hasa ndiyo walipata nafasi kubwa zaidi.
Wengine ni wabunge wanaoingia `barazani,` na wao pia walikuwa wamejumuishwa, hivyo wanafahamu majukumu waliyoelekezwa.
Kwa maana hiyo JK anataka kusema hakuna maelekezo mapya yanayohitajiwa, na kwamba anatazamia kuwa walioteuliwa walikowapo kwenye semina hizo, wanatakiwa wazingatie waliyoelezwa, siyo kuona kana kwamba kuna serikali mpya, ianze kuangalia masuala kwa upya.
Ina maana kuwa kiwango kikubwa cha utendaji serikali kitabaki pale pale, kwa maana ya maelekezo yaliyopo, na ni katika msisitizo tu ambako JK alitaja kuwa atafanya mabadiliko pindi ikibidi.
Hivyo tatizo linakuwa ni sababu gani iliyomfanya JK akachagua usemi wa ``kupiga marufuku`` kufanyika semina kama hizo, wakati ambapo zilifanyika kwa vile yeye alitaka zifanyike, au kwa kukubaliana na Waziri Mkuu wake.
Ila tu itakuwa si rahisi kusema kuwa ni Waziri Mkuu aliyeongoza semina hizo au kuwa na wazo la aina hiyo, kwani ushiriki wa rais ulikuwa wa dhati na wa kina, ikiwa ni ufuatiliaji ziara zake za awali katika idara na wizara, alipoingia madarakani.
Kupiga marufuku semina hizo kuna maana ya ziada, ambayo labda ni halisi, kuwa zisiandaliwe warsha au semina katika ngazi yoyote ya utawala, iwe ni kwa wizara au idara.
Moja ya warsha au semina kama hiyo ni kuweka wazi nini nia za serikali mpya, mwelekeo wake kiutendaji, ikilinganishwa na ile iliyotangulia.
Jawabu analotaka kutoa JK ni kuwa kusiwe na mjadala kama huo, kuwa yeye binafsi hauhitaji, na angependelea kusiwe na wizara inayoanza warsha hizo.
Kimsingi tatizo ni kwanini suala hilo likawa la haraka kiwango hicho, tena kwa kupiga marufuku aina zote za `semina elekezi,` kana kwamba hakuna masuala ya kuongea baada ya serikali mpya kutangazwa.
Na isitoshe, waziri mkuu mpya Mizengo Kayanza Peter Pinda ametoa maelezo ya mrengo wa sera na kazi yake, mwelekeo wa ufuatiliaji, ambao ni tofauti na ule wa Edward Lowassa.
Hivi mabadiliko kama hayo yasingehitaji kujadiliwa kwa kina kiasi?
Hapa labda ndipo `siri` ya huko `kupiga marufuku` inajitokeza, kuwa mfuatano wa utendaji kazi kimsingi ni ule ule; hapatakuwa na vikao vya kula na kunywa huku wajumbe wa `semina elekezi` wakifurahia kuondolewa madarakani kwa Edward Lowassa.
Hiyo hasa ndiyo maana ya ``kupiga marufuku,`` kwa maana kuwa wahusika wasianze kabisa kutafakari yale ``mema`` ya semina elekezi, au umuhimu wake kuelewa tofauti ya ufuatiliaji wa ``shughuli za maendeleo`` au kwa lugha fasaha zaidi matatizo ya kiutawala, kati ya Mh. Lowassa na Mh. Pinda,, n.k.
Yako masuala ya ``kutenganisha uongozi na biashara`` ambayo bila shaka yanahitaji semina elekezi, na hata mkutano mkuu maalum wa CCM, na mengine.
Mpangilio kama huo wa ufafanuzi unaashiria vile vile kuwa pamoja na kuwa JK ametulia au kuridhika kuwa dhoruba iliyoukumba utawala wake imepita, bado kuna mapengo ya kihisia.
Inabidi akubali serikali mpya yenye ladha ya watu wanachotaka, lakini hawezi kushiriki dhifa, semina na hafla za kujipongeza, kama alivyowaasa mawaziri wapya kutoonyesha furaha kupita kiasi, kuitisha sherehe na mambo kama hayo.
Ni wazi kuwa mpangilio huo wa hisia unaonyesha kuwa kuna urafiki wa dhati na maelewano kati ya wakuu hao wawili, na kuwa JK hayuko katika mandhari ya kufurahia kuondoka kwa waziri mkuu na msaidizi wake mkuu kabla ya hapo.
Ni katika utendaji wa Mh. Lowassa ambako ``kasi mpya`` ilionekana; hotuba zake pia zilisheheni takwimu za kile ambacho kimefanyika, na inawezekana sehemu nyingine za utendaji zikawa zimekosa msukumo.
Ndizo anazotaka kuziangalia Mh. Pinda, hasa kuhusu utawala katika ngazi ya wilaya, na matumizi ya fedha.
Ndiyo maana wanaounga mkono mkondo huu wa mageuzi kwa kuwaponda wale waliokuwa mawaziri waandamizi kama ni ``mafisadi`` na wanatazamia kuwa sasa ni wakati wa ``mapinduzi`` ya kina, kutenganisha (kabisa) biashara na uongozi, wasitarajie kuwa wanaye swahiba wa dhati Ikulu kwa mpangilio huo wa fikra.
Ingefaa zaidi wazingatie matamshi ya Waziri Mkuu Pinda kuwa ``yaliyopita si ndwele tugange yajayo,`` na iwe ni pamoja na kuachia vyombo husika kumaliza kisheria suala la akaunti za Richmond, malipo yaliyobaki, n.k. Siyo kamata hii…
|