|
Dawa ya deni kulipa
2008-02-25 08:35:39
Na Mhariri
Mwishoni mwa wiki hii, vyombo vya habari vilitawaliwa na sakata la mvutano baina ya Shirika la Majisafi na Majitaka (DAWASCO) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Sakata hilo lilianza pale DAWASCO ilipoamua kulikatia maji jeshi hilo jijini Dar es Salaam kutokana na kutolipa bili ya maji ambayo hadi Alhamisi wiki iliyopita, deni lilikuwa linasomeka kwamba ni shilingi milioni 276.
Katika operesheni hiyo maalum ya DAWASCO, vikosi, kambi, nyumba za maofisa na hospitali ya Lugalo vilikatiwa maji.
Baada ya maji kukatwa siku ya Alhamisi, ripoti zinaonyesha kwamba mafundi watano waliofanya \'kosa\' hilo walishikiliwa kwa muda na maofisa wa jeshi hilo kabla ya kuachiwa baadaye.
Hali hiyo ilisababisha zoezi la operesheni kata maji kusimama kwa muda hadi DAWASCO walipoleta mafundi wengine.
Kana kawamba hiyo haitoshi, siku iliyofuata, Jeshi hilo la Wananchi lilivamia ofisi ndogo za DAWASCO zilizopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwashambulia wafanyakazi watano wa shirika hilo mbele ya familia zao.
Mbali na kuwapiga wafanyakazi hao, waliwalazimisha kuwafungulia maji waliyokatiwa, kisha wakatumia nguvu kuwabeba hadi kambi ya jeshi la Lugalo.
Waandishi waliokuwepo katika matukio yote mawili walionja kidogo `joto ya jiwe` pia kwa kusukwa sukwa na wanajeshi ama watoto wao wakiwemo watumishi wa ndani na katika tukio moja mpiga picha alinyang`anywa kamera yake.
Ijumaa jioni, Jeshi hilo lilitoa taarifa likiishangaa DAWASCO kwa kukata maji huku ikijua kuwa ``jeshi ni taasisi ya serikali ambayo inategemea fedha kutoka serikalini na pia ni wadau wakubwa wa shirika hilo.``
Katika taarifa hiyo jeshi lilisema kwamba licha ya madhara yanayoweza kutokea katika maeneo nyeti, mfano hospitali kuu ya kijeshi, Lugalo, kulikatia maji kunaweza kuleta picha potofu kwa wananchi kwamba ``Jeshi haliwajibiki katika kulipia huduma wanazopewa wakati jeshi linalipia huduma zote hizo kulingana na bajeti. Jeshi (pia) limekuwa mstari wa mbele kuisaidia DAWASA na DAWASCO pale panapotokea madhara katika mfumo wa maji.``
Jeshi pia lilisema linapata bajeti ndogo ya maji kutoka serikalini na wakati mwingi bili za maji huwa zimekosewa na zinahitaji marekebisho kabla ya malipo kufanyika.
Inawezekana JWTZ wana hoja, kwamba DAWASCO walitakiwa kuvuta subira kwa vile jeshi lilikuwa halijapata pesa kutoka serikalini pamoja na suala zima la kuhakiki bili.
Lakini kilichofanya tuandike tahariri hii ni hatua za kibabe zilizochukuliwa na baadhi ya askari wa jeshi hilo za kuwakamata na wakati mwingine kuwapiga mafundi wa DAWASCO waliokuwa wakilinda kibarua chao kwa kutekeleza maagizo ya mabosi wao, kukata maji.
Taswira tuliyopata sisi kutokana na kitendo hiki ni kama vile wanajeshi wako juu ya sheria na pale raia unapofanya jambo la kuwaudhi, iwe amekosea ama ni halali, wanamuadhibu pale pale kadri wanavyopenda ama kuweza!
Tunafahamu kwamba viongozi wa DAWASCO walifungua mashitaka polisi dhidi ya askari wa jeshi hilo walioendesha operesheni ya kukamata na kuwapiga mafundi pamoja na waandishi wa habari, lakini tunachoshangaa ni kuona taarifa ya JWTZ ikiishia kuishangaa DAWASCO pekee bila kukemea KWA NGUVU ZOTE vitendo vya kihuni vilivyofanywa na maofisa wake wa chini.
Sisi tunadhani kwamba hii haijengi picha nzuri kwa wananchi na inaweza kumtisha kila raia, hususan anayefanya biashara na jeshi hilo.
Pili, kinachoonekana hapa ni kwamba Jeshi halikanushi kuwa linadaiwa na DAWASCO na hivyo kukatiwa ama kutokatiwa maji kunategemea hisani ya DAWASCO na mahusiano yaliyopo baina ya mteja na mtoa huduma.
Halikadhalika tunapenda kutumia nafasi hii kupingana na kauli ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya, ya kuwakingia kifua mawaziri wasiandikwe kwenye magazeti hata kama ni wadeni sugu.
Sisi tunawashauri DAWASCO kuendelea na kuwakatia maji na kuwaumbua wadeni wote sugu bila kuwaangalia usoni.
Waswahili wanasema; `Mwenye chake muungwana` na ``Dawa ya deni kulipa.``
|