|
Hosea anafahamu maana ya uwajibikaji wa kisiasa?
2008-02-23 09:10:14
Na Haji Mbaruku
Kamati teule ya Bunge iliyopewa jukumu la kuchunguza mkataba wa uzalishaji umeme wa dharura wa Richmond ulitoa mapendekezo hivi karibuni kuwa, baadhi ya wahusika wawajibishwe kwa manufaa ya umma kutokana na sababu mbalimbali.
Kwanza, kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo ukiisoma wala haichoshi, kampuni ya Richmond haipo nchini Marekani, ni sawa na Masumin hapa nchini.
Halafu, Richmond yenyewe ambaye ilikuwa inapigiwa debe sana na baadhi ya watendaji serikalini haikuwa na hata uwezo wa kuchomeka balbu kwenye kishikizo chake.
Kwa hiyo, watanzania tunailipa Richmond kila siku shilingi milioni 152.
Hata hivyo, baada ya kubainika yote hayo, kamati teule ikapendekeza kuwa, kwa vile masuala yote hayo yalikuwa chini ya mamlaka ya Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa ambaye ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za serikali, kamati ikaona ni vyema abebe msalaba huo.
Kamati pia inaona viongozi wa Taasiri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU wawajibishwe kwa kuisafisha Richmond wakati ilipopewa kazi ya kuchunguza.
Hata hivyo, Hosea mwenyewe ambaye hivi karibuni alitunukiwa shahada ya udaktari pale Chuo Kikuu cha Dar es salaam, amevunja ukimya akisema hawezi kujiuzulu kamwe.
``Kama nilitaka kujiuzulu, nisingekuwa kwenye mkutano huu leo,`` alisema Hosea kwenye mkutano wa masuala ya rushwa pale Zanzibar alipozungumza na waandishi wachache.
``Wako huru kunihukumu. Rais wangu ananijua mimi. Anajua kazi yangu na uwezo wangu. Ananiamini.Yeye ndiye anayeweza kuamua kuhusu suala hili.``
Hosea aliendelea tena kusema kuwa TAKUKURU ilifanya uchunguzi wake kuhusu mkataba wa Richmond kulingana na sheria zinazotawala taasisi yake na kugundua kuwa hakukuwa na rushwa.
``Nataka umma uelewe kuwa kazi yangu kwa mujibu wa sheria ni kuchunguza kama kulikuwa na rushwa kwenye mkataba. Wasiwasi wangu haukuwa kama mkataba ulikuwa mzuri ama mbaya.``
Kusema kweli Hossea ametoa madai ya kushangaza sana.
Ametoa madai huku akiwa hajui ni nini maana ya uwajibikaji wa kisiasa.
Na ndio maana katika masuala ya utawala, tunasisitiza kuwa ni vyema watawala wetu wakajifunza siasa ili wajue dhana nzima ya utawala na siasa.
Kuwajibika kisiasa kumeelezwa vizuri sana na kamati ya Dk.Mwakyembe na wala hakuhitaji kutumia muda mwingi kumuelewesha Hossea na wengine wanaokataa kuwajibika.
Tatizo kubwa tulilokuwa nalo watanzania wa kizazi cha sasa ni kuwa, ni wavivu sana wa kusoma.
Ni watanzania wachache tu ambao wana utamaduni wa kusoma vitabu ama ripoti.
Hossea hakutumia muda wake ipasavyo wa kuisoma ripoti hiyo kwa sababu tu anadhani ameonewa.
Hata baadhi ya wabunge hadi leo wanaona uvivu kuisoma ripoti hiyo na ndio maana baadhi yao wanaonekana kung`ang`aa macho bungeni wakati mjadala ulipokuwa ukiendelea.
Ripoti iko wazi. Hata mimi baada ya kuiona kuwa haichoshi kuisoma, nikaisoma na kila wakati nairudia kuisoma. Ni tamu kweli kweli.
Hossea anapaswa kujua kuwa Waziri Lowassa hakujiuzulu kwa sababu alipewa rushwa, la hasha, Lowassa alijiuzulu kama mzee Mwinyi alipofanya hivyo wakati alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Hata mimi katika kuisoma kwangu ripoti ile iliyochapishwa kwenye magazeti, sikuona sehemu yoyote ile ambayo inamtaja Waziri Lowassa kuwa alipewa mshiko.
Isipokuwa Waziri Lowassa aliwajibishwa kwa sababu uozo huu umetokea kwa watendaji walio chini yake.
Kwa hiyo, kisiasa, hata John Locke, mtaalamu wa masuala ya siasa wa Marekani wa enzi za kale, anasema kuwa Waziri Lowassa anawajibika kisiasa.
Uwajibikaji wa kisiasa maana yake ni kiongozi wa juu anawajibika kwa kujiuzulu kutokana na utendaji mbovu uliofanywa na watendaji wake wa chini ambao umeisababishia nchi aibu, hasara ama hata kashfa.
Ndio maana Dk.Mwakyembe alisema, ``Kamati imegundua kuwa matatizo yote ya Richmond, chanzo chake ni Waziri Mkuu kwa sababu yeye ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali.``
Kwa hiyo, Dk. Mwakyembe akahitimisha kuwa, ``Ni jukumu lake mheshimiwa Lowassa kupima matokeo ya uchunguzi wa ripoti ya kamati hii.``
Kwa hiyo, Waziri Lowassa hakuwa na jinsi, kwa vile watendaji walio chini yake walimuangusha, naye akajikuta akibeba msalaba huo.
Ndivyo alivyofanya Waziri Mwinyi alipokuwa Mambo ya Ndani kwa sababu ya uwajibikaji, Mwinyi akaona anawajibika kwa kosa hilo.
Ndio uwajibikaji wa kisiasa unavyokuwa, unawajibika kutokana na utendaji mbovu wa watu walio chini yako ambao walikuwa wanakupeleka peleka bila wewe mwenyewe kufanya uchunguzi.
Sasa Bw.Hossea anadai Rais anajua kazi yake ndio maana hawezi kujiuzulu, kwani ni mtanzania gani asiyejua kuwa Hossea ni mkurugenzi wa Takukuru au kwanini Rais asijue kazi ya Hossea wakati ndiye aliyemteua kuchukua nafasi ya Bw.Anatory Kamazima aliyestaafu?
Hossea hana utetezi katika hili. Ni bora angeendelea kukaa kimya tu kuliko anavyoendelea hivi sasa.
Mwenzake Mwanasheria mkuu wa Serikali ameona bora aendelee kukaa kimya kuliko kuzidi kuwatia hasira watanzania kutokana na kushindwa kuishauri serikali vizuri katika masuala ya kisheria.
Watanzania wanadhani sasa Hossea amefikia kikomo na hawezi kusaidia katika uchunguzi wa ufisadi BOT.
|