|
JK atafanikiwa kiasi gani?
2008-02-08 09:17:02
Na HAMIS MZEE
Kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kutaka viongozi waache kujishughulisha moja kwa moja na biashara ni changamoto ambayo bila shaka inawaweka njia panda viongozi na kuwafurahisha wananchi.
Wakati Rais Jakaya Kikwete alipotangaza kwa mara ya kwanza dhamira ya kutaka kuweka utaratibu wa kuzuia viongozi kuchanganya shughuli zao za kazi na biashara, bila shaka alisababisha mshtuko mkubwa hasa kwa viongozi ambao wamejikita katika biashara.
Mara ya kwanza Rais alizungumzia suala hilo katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi aliyoitoa mwishoni mwa mwezi uliopita.
Bila shaka hata yeye mwenyewe alibaini baadaye kuwa kwa kauli yake hiyo alikuwa amegusa wenzake wengi na kumfanya kutoa ufafanuzi.
Akizungumza katika mkutano wa kuadhimisha miaka 31 ya CCM huko Pemba majuzi,Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho tawala, aliweka bayana dhamira yake ya kutaka kuchukua hatua ya kuwa na utaratibu wa vingozi kutenganisha shughuli zao za biashara na kazi zao za uongozi.
Inakera na inaudhi wananchi wanapoona viongozi wao wanajichimbia zaidi katika shughuli zao za biashara jambo ambalo linapunguza kama si kuondoa imani yao kwa viongozi hao.
Inaonekana sasa viongozi hawazingatii maadili yao lakini Rais Kikwete amefafanua kuwa si kwamba anawataka waache biashara zao la hasha.
Anachotaka ni kwamba wakati wakiwa katika nyadhifa hizi za uongozi wakae kando na wawape wengine kuwaendeshea biashara zao.
Kauli ya kwanza ya Rais ilieleweka kuwa ni kutaka viongozi waache biashara ilikubaliwa na wananchi wengi waliunga mkono lakini kwa ufafanuzi huu, bila shaka utawachanganya.
Itaonekana kuwa ``vigogo`` wataendelea na mambo yao kama kawaida, kwani itakuwa vigumu kwao kukaa kando ya biashara zao.
Dhana hii inajengeka kutokana na kauli aliyoitoa mmoja wa viongozi wa CCM ambaye kwa muda mrefu na hasa katika awamu ya nne ya uongozi huu wa Rais Kikwete amekuwa mtu wa karibu sana.
Mbunge mmoja wa muda mrefu na mjumbe wa kamati kuu ya CCM amekaririwa na gazeti moja mara baada ya kauli hiyo ya rais kwamba inamweka njia panda.
Mbunge huyo alisema katika hali ya uchanga wa biashara hapa nchini, kuwaachia wengine waendeshe biashara yako ni kutaka kufilisika!
Mkanganyiko unaojitokeza sasa na unaoonyesha sura ya viongozi wengi kuchangamkia biashara bila shaka unatokana na uamuzi wa 1991 wa Chama Cha Mapinduzi wa kulegeza masharti yaliyowabana viongozi.
Maadili ya uongozi ya wakati huo yaliwabana kiasi cha kuwafanya wasiwe na kipato zaidi ya mishahara yao.
Maadili yaliyopitishwa baada ya azimio la Arusha
yalimtambua mtu yeyote anayepata mshahara wa sh. 1,066 kwa wakati huo kuwa ni kiongozi na yalimbana.
Maadili hayo yalikwenda mbali zaidi kuwa kiongozi ni mtu pamoja na mkewe na hivyo wakati huo hata ukifuga kuku kwa mgongo wa mkeo, ulionekana kuwa ni ukiukaji wa maadili!
Wakati Rais mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Mwinyi akitoa ufafanuzi wa Azmio la Zanzibar ambalo lililegeza masharti ya Azimio la Arusha alikariri Msahafu - kitabu kitakatifu cha Waislamu - kwa kusema kuwa ``Likuli ajalin kitabu`` aya ambayo Mwingireza mmoja alitafsiri kuwa To every age its book ikimaanisha ``kila zama ina kitabu``.
Alisema kuwa`` na sisi CCM tunakubali kuwa kila zama zinahitaji kuwa na mwongozo wake``.
Licha ya kukiri kuwa Azimio la Arusha ni dira na mwongozo wao unaoonyesha mwelekeo wa jamii, lakini tafsiri zake zinabidi kurekebishwa kila inapohitajika ilizisipitwe na wakati.
Kwa mfano wakati mtu aliyepata sh. 1,066 alionekana kiongozi wakati wa azimio hilo katika miaka ya katikati ya 1980 kima cha chini cha mshahara kilifikia sh. 2,500 na kwa maana hiyo kila mtu anaonekana ni kiongozi!
Azimio la kutaka CCM isipitwe na wakati la Zanzibar lilifungua milango na kutoa ruhusa kwa viongozi kuweza kupangisha nyumba, na watu kuwa na vipato halali zaidi ya kimoja.
Katika ufafanuzi wake katika hotuba kwa wazee wa Dar es Salaam Mzee Mwinyti ambaye amepata umaarufu wa kuitwa Mzee Ruksa, alisema kuwa iwapo mtu ana nyumba aliyoijenga kwa mkopo kwanini asipangishe ili imsaidie kulipia deni.
Vile vile iwapo kiongozi amehamishiwa sehemu nyingine na ilipo nyumba yake, basi kwanini asiipangishe badala ya kuiacha nyumba ile ikae tupu.
Alisisitiza kuwa kinachokatazwa kwa wakati ule ni kiongozi kujenga majumba ya kupangisha. ``Anakopa anajenga na kupangisha na kuendelea kujenga tena na kupangisha``
Kwa upande wa mishahara ama mapato mawili ni kwamba mtu anaweza kuwa mtaalamu wa jambo fulani na ameajiriwa.
Anafanyakazi yake kama kawaida na baada ya kazi anaweza kutumia utaalamu wake kwa kutoa ushauri na kuweza kujiongezea kipato… hiyo haina shida.
Kuzingatia kauli ya Mzee Ruksa kuwa kila zama ina kitabu chake, katika zama za ukweli na uwazi za Rais Benjamin Mkapa ambaye alishika uongozi wa nchi baada ya Mwinyi mambo yakabadilika zaidi.
Viongozi kuanzia mwenyewe Rais wakawa wanafanya biashara kujiongezea vipato kwa kasi iliyotisha na kutafsiriwa kuwa wanajilimbikizia mali.
Inawezekana kabisa kuwa hiyo isingekuwa mbaya kama wangefanya hivyo bila kutumia nyadhifa zao na raslimali za umma.
Katika kipindi kile cha miaka 10 ya Mkapa ambaye Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alimpigia debe aingie Ikulu kwa kuwa alikuwa mtu safi kimaadili, viongozi waliingia katika mashindano ya kujitajirisha.
Nafasi ilijitokeza kwa kuwa ni wakati wa kuuza mashirika ya umma na kukaribisha vitega uchumi.
Viongozi wakajichukulia maeneo makubwa ya ardhi bila hata kujali madai na mahitaji ya wananchi wa maeneo husika.
Kushoto, kulia na katikati viongozi walipigana vikumbo kujiongeza mali - au utajiri.
Sasa kaingia Kikwete, watu walimpigia kura nyingi kutokana na kuwa na matumaini makubwa naye.
Kwa miaka miwili amejaribu kuwajengea wananchi mazingira ya kuwa na maisha bora.
Ametoa mikopo ya kusaidia wale ambao hawawezi kukopeshwa na mabenki.
Kwa bahati mbaya kwa kiasi kikubwa mikopo hiyo haikuwafikia walengwa.
Kikwete sasa yuko katika mwaka wa tatu, pamoja na kuongeza nafasi za elimu kuwezesha watoto wengi zaidi kupata elimu ya sekondari, bado wananchi walalamika.
Maisha yanazidi kuwa magumu, mfumuko wa bei umepeleka hali kuwa ngumu zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya kuingia yeye madarakani.
Kulikoni? Bila shaka katika kutafuta jawabu Kikwete ameng\'amua kuwa ``kikulacho ki nguoni mwake``...Ni viongozi wenzake.
Viongozi badala ya kutimiza majukumu yao na kuwatumikia wananchi wamejitoma zaidi katika shughuli zao za kibiashara--- wengine wana migodi, viwanda, maduka makubwa , majumba mengi ya kupangisha, wengine ni mawakili wenye mtandao wa kimataifa.
Hizi kashfa za ufisadi zinazoibuka zinaonyesha vidole kwa baadhi ya viongozi.
Sasa nini cha kufanya?
Yeye mwenyewe Rais ametamka kuwa wananchi wanakosa imani na viongozi wao.
Kwa upande mwingine kwa kuwa tatizo hili la viongozi au watu waliozoea uongozi kujihusisha na biashara ni la muda mrefu, itabidi itazamwe njia mbadala.
Badala ya kuzuia viongozi kujihusisha na biashara moja kwa moja pengine serikali iweke mikakati na kubuni mbinu za kuhakikisha kuwa ingawa kiongozi ana miradi basi asiwe kuthubutu kutumia raslimali na muda wa kazi katika shughuli zake.
Hili bila shaka likifanywa kwa uangalifu na bila kuoneana haya linawezekana.
Rais Kikwete bila shaka kwa kuzingatia usemi wa afadhali ya lawama kuliko fedheha ameona alishughulikie suala la viongozi na biashara.
Atafanikiwa kiasi gani? Itabidi awabwage wakaidi au awabebe hivyo hivyo?...Ni suala la muda.
|