08 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

TFF itafute ufumbuzi wa Stars kukosa mechi
 
2008-02-08 09:12:43
Na Mhariri

Kwa mara ya pili, timu ya taifa, Taifa Stars tumeshuhudia ikikosa michezo ya kimataifa ya kirafiki, hali ambayo inatoa wakati mgumu kwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbrazili Marcio Maximo.

Stars ilitakiwa Jumatano iliyopita kucheza na Malawi, mchezo wa kirafiki lakini ikajitoa katika dakika za mwisho.
Bado ni kitendawili kwa nini Stars inaendelea kukosa michezo ya kirafiki, ingawa viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) wakitoa sababu mbalimbali.

Kama ni kujifunza, TFF ilipaswa kujifunza pale ilipoialika timu ya taifa ya Nigeria halafu ikashindwa kuja ingawa baadae TFF ilidai kuwa Wanigeria ndio walikiuka makubaliano.

TFF ilidai Nigeria ilikuwa tayari kuja lakini tayari katika vyombo vya habari kulikuwa na taarifa kwamba timu hiyo ilikuwa imejipanga kucheza mechi yake nchini Kenya.

Shirikisho hilo baadae lililazimika kutoa mwaliko wa haraka kwa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes.

Michezo ya kirafiki ya kimataifa ni suala ambalo linatambulika kimataifa, ambapo pia husaidia katika kupandisha kiwango cha nchi kwenye orodha ya viwango vya FIFA.

Kweli, inawezekana ni ngumu kwa kuweza kukusanya kikosi chake kwa wakati muafaka, lakini pia ni rahisi kwa nchi yeyote kufanya hivyo endapo TFF itawasiliana mapema na nchi ambayo wanaziona zinafaa kucheza na timu yetu.

Hali hii ya kukosa timu za kukifanyia kikosi cha Stars majaribio itaendelea mpaka lini tarehe zilizopangwa na FIFA kwa ajili ya michezo ya kirafiki ya kimataifa zinajulikana.

Mialiko ya kushtukiza imepitwa na wakati, hivyo kuna haja kwa TFF kujipanga mapema pale inapoona kunahitajika mchezo wa kirafiki kama ilivyotokea hivi karibuni na kuangalia upya mikakati yao ya kutoa mialiko.

TFF, inaijua vizuri kalenda ya FIFA ambayo hiyo ndio inatumiwa na mataifa yote Duniani, hivyo ni lazima ijifunze kufanya taratibu za kuialika nchi mapema.

Kutokana na ukweli kuwa moja ya sababu za Stars kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ilikuwa ni ukosefu wa mechi za kimataifa.

Watanzania walio wengi wameshuhudia fainali za Kombe la Mataifa zinazoendelea nchini Ghana na kuona kiwango cha juu cha soka kilichoonyeshwa na nchi mbalimbali.

Kutokana na hali hiyo ni wazi, bila kujipima nguvu kwa mechi kali itakuwa ndoto kwa Stars kufuzu kwa fainali zozote za mashindano hayo.0

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.