07 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Ripoti ya Richmond, Wabunge kazi kwenu
 
2008-02-07 09:37:11
Na Mhariri

Ripoti ya Kamati ya Teule ya Bunge ya kuchunguza mkataba wa uzalishaji umeme wa dharura kati ya Serikali na Richmond Development Company LLC ya Houston, Texas, nchini Marekani uliotiwa saini mwaka 2006 imetolewa bungeni mjini Dodoma jana.

Ripoti hiyo, imetoa matokeo ya uchunguzi uliofanyika kwa kuwahoji watu mbalimbali, wenye nyadhifa na fursa tofauti ndani na nje ya nchi.

Mambo mengi yamejitokeza katika ripoti hiyo, lakini mawili makubwa ni kwamba Richmond haikushinda kihalali zabuni hiyo, na hivyo ilipendelewa.

La pili ni kwamba mkataba huo ulikuwa bomu kwani Richmond haikuwa na ujuzi wa kutosha na hivyo taifa likaingia hasara.

Watu wanaodaiwa kuhusika katika kufanikisha kampuni ya Richomond kupata zabuni ya kuzalisha umeme, wakiwamo viongozi waandamizi serikalini wametajwa pia katika ripoti hiyo.

Leo, wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, wanaanza kuijadili ripoti hiyo, ambayo ndani yake kuna mapendekezo kadha wa kadha yaliyotolewa.

Tunaipongeza kamati hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Dk. Harrison Mwakyembe, kwa kutumia vizuri muda iliyokabidhiwa, kushughulikia suala hilo lenye umuhimu kwa maisha ya kawaida ya wananchi na Taifa kwa ujumla wake.
Kamati hiyo, imeonyesha kuzitambua dondoo zilizowasilishwa na Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta.

Pia, tunawapongeza watu na taasisi zilizojitokeza na kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo, hali iliyowezesha kufanikisha azma ya kupatikana ripoti iliyowasilishwa bungeni jana.

Tunaamini, kama watu na taasisi hizo wasingejitokeza kutoa ushahidi na maelezo yao, wakiwa katika kiapo ama nje ya kiapo, ufanisi wa ripoti hiyo usingekuwa kwa kiwango kilichopatikana.

Kamati ya Dk. Mwakyembe, imetoa mapendekezo na ushauri kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa, huku Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta, akiahirisha kikao cha Bunge jana, ili kutoa nafasi kwa wabunge kuisoma, kabla ya kuijadili leo.

Wakati tunapongeza mambo yaliyotokea katika mchakato wa utekelezaji majukumu yaliyokabidhiwa kwa kamati hiyo, tunawaasa wananchi wa kada tofauti, kuwa wavumilivu na kuepuka kauli, vitendo ama hisia zinazoweza kuibua uhasama na chuki miongoni mwa jamii.

Tunasema hivyo kwa sababu, suala la Richmond na matokeo yaliyoainishwa kwenye ripoti ya Dk. Mwakyembe, yana uzito ambao kama tahadhari haitachukuliwa, Taifa linaweza kujikuta katika mgawanyiko mkubwa.

Kwa kuwa dalili zimeonyesha kiwango kikubwa cha ukweli, uhuru na uwazi ulivyotumika, kwa kufuata misingi ya Katiba ya nchi na taratibu na kanuni za Bunge, hakuna sababu ya kushindwa kutoa nafasi, ili mlolongo huo uendelee kwa amani na salama.

Ni ukweli kwamba kasoro zilizojitokeza katika mkataba wa Richmond na serikali (kupitia TANESCO), zina athari kwa maisha ya kawaida ya wananchi, lakini tukio hilo linaweza kuchukuliwa pia kwa misingi ya kisiasa.

Tanzania ni nchi yenye mfumo wa vyama vingi, hivyo si jambo la kushangaza kuona, kwa mfano, kwa vile wahusika wengi waliotajwa wanatoka kwenye chama kimoja cha siasa, wanasiasa wa upande mwingine, wakaweza kuigeuza hoja hiyo kuwa ya kisiasa.

Hali hiyo ambayo ni vigumu kuiepuka, inaweza pia kutokea ndani ya chama wanachotoka wahusika, yaani waliotajwa kuhusika katika kadhia hiyo.

Kama tulivyoeleza awali, suala hili ni la kitaifa, linahitaji subira ya kitaifa na kutoa nafasi ili mkondo sahihi wa kisheri, kanuni na taratibu ufuatwe kwa maslahi kwa umma.

Kamati imeshakamilisha kazi yake. Wanachi wanangojea kwa hamu mjadala wa Wabunge na maazimio watakayofikia kuhusu yaliyobainishwa katika ripoti ya kamati ambayo waliiunda wao wenyewe.
Haya wabunge. Kazi kwenu.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.