07 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Manispaa Kinondoni kukabili tatizo la miundo mbinu mibovu
 
2008-02-07 09:36:09
Na Abdul Mitumba

Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam inakabiriwa na uchafuzi wa mazingira unaotokana a utiririshaji wa maji machafu yakiwemo ya vyooni barabara na katika makazi ya watu. Hali hiyo ni kikwazo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Kwa kutambua hilo, Manispaa hiyo imelazimika kutumia zaidi ya sh.milioni 356 kuimarisha miundombinu ya barabara na mifereji kama Mwandishi Abdul Mitumba anavyoeleza katika maka hii.

Ukipita maeneo mengi ya manispaa hiyo, utasikia harufu mbaya au maji machafu yakiwemo ya vyooni yakitiririka. Hali hiyo inasikika katika maeneo kadhaa, ikiwemo katika vituo vya basi ambapo mifereji ya maji inatoa harufu mbaya kutokana na maji yaliyochanganyika na uchafu kutuama kwa muda mrefu.

Maeneo mengine pia mifereji inatoa harufu mbaya kutokana na takataka kurundikana na kuzalisha uchafu, hatua ambayo wakati mwingine inasababisha kuzuka kwa milipuko ya magonjwa ya kuambukiza, kikiwemo kipundupindu.

Kutokana na hali hiyo, Manispaa hiyo imelazimika kutenga zaidi ya sh.milioni 356 ili kujenga miundombinu upya, ikiwemo kukarabati barabara, mifereji, madaraja pamoja na ujenzi wa kituo cha mabasi cha Makumbusho Sokoni ambacho peke yake kimegharimu sh.milioni 136.

Kiasi hicho cha fedha kimetumika katika nusu ya mwisho wa mwaka jana na fedha hizo zimetengwa na kupitishwa na Baraza la Manispaa ya Kinondoni.

Mhandisi wa ujenzi wa barabara wa Manispaa hiyo, Bw.Mapinduzi Magesa alisema kiasi hicho cha fedha pamoja na mambo mengine kimetumika kufanikisha ujenzi wa kituo kwa kiwango cha changarawe na kukamilisha ujenzi wa barabara zinazozunguka kituo na zile zinazoingia na kutoka kutuoni hapo.

``Katika ujenzi huo uliofanywa na kampuni ya Delmonte Tanzania Limited ya jijini, pia ulihusisha ujenzi wa mifereji na uwekaji wa kifusi na changarawe katika barabara zaidi ya tatu zinazoanzia barabara kuu ya Bagamoyo,`` alisema.

Alisema ujenzi wa kituo hicho kwa sasa umekamilika na hatua inayofuata imetafutiwa mwekezaji mpya ili kuendeleza hadi kufikia kiwango cha lami na ujenzi wa majengo ya maduka kuzunguka kituo hatimaye kuwa cha kudumu.

Alisema maduka hayo yatatumika na wafanyabishara wadogo maarufu kama wamachinga ambao kwa sasa wanaendesha biashara zao kuzunguka kituo hicho.

Mbali na mradi huo, Bw.Magesa alisema Manispaa pia imeanza ujenzi wa barabara ya Idrisa yenye urefu wa kilomita 2.7 inayopitia mitaa ya Idrisa na Chemchem katika kata ya Magomeni, ambapo mitaa kadhaa imebainika kuwa na mifereji michafu inayotiririsha maji ya kinyesi katika makaro.

Katika mtaa mmoja pekee, makaro manne yenye vina virefu yamegundulika yakiwa wazi huku yakipokea maji machafu kutoka vyooni, hivyo kutoa harufu mbaya.

Baadhi ya wakazi wa mtaa huo na mitaa ya jirani wamesema hali huwa ni mbaya zaidi kila mvua zinavyonyesha, ambapo makaro hayo hufurika maji machafu yalioambatana na kinyesi kusambaa hadi ndani ya nyumba na kuhatarisha afya zao.

Hali hiyo imemlazimisha mbunge wa jimbo la Kinondoni aliyekuwa katika ziara ya siku moja kukagua miradi ya ujenzi wa miundombinu, Bw. Idd Azzan kuomba Ofisa Mtendaji wa kata ya Magomeni pamoja na Ofisa Afya wake na Mtendaji wa mtaa kuwashirikisha wananchi kuhakikisha hali hiyo inatoweka haraka iwezekanavyo.


``Hali hii haivumiliki hata kidogo na pia hatuwezi kuzungumzia maisha bora kwa kila mtanzania wakati wenzetu kama hawa wanaishi katika mazingira hatarishi kiafya kama haya,`` alisema.

Akaongeza kuwa kama mnapenda kuendelea kujenga imani kwa wananchi, fanyeni kila mnaloweza kurekebisha hali hii mbaya.

Akawaagiza wananchi wa kata hiyo, hususan wa mitaa ya Chem Chem na Idrisa kujali na kuheshimu kanuni za usafi ili kujihakikia mazingira bora ya kuishi.

Amewataka watu wote waliounganisha mabomba machafu kutoka vyooni na kuelekeza katika mifereji hiyo kuondoa mara moja ili kuacha maji ya mvua pekee yatumie mifereji hiyo hatua ambayo itapunguza uchafu wa sasa.

Akizungumzia hali hiyo, Ofisa Mtendaji wa kata hiyo Bi.Latifa Ramadhani alisema, jambo hilo lipo chini ya uwezo wake na kwamba ofisi yake italishughulikia haraka kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu ya kipekee.

Kwa upande wake, Mhandisi Magesa alisema kiasi cha fedha kilichotengwa pia kitatumika kujenga barabara nyingine tano zenye urefu wa kilomita 8.9 kwa hatua ya changarawe pamoja na ujenzi wa daraja la Madaba lililopo katika mto Msimbazi.

Alizitaja barabara hizo ambazo ujenzi wake unakaribia kukamilika kuwa ni Kagera First Inn, Kondoa, Kagera Popobawa na ile ya ITV ambazo zitagharimu sh.milioni 97 zitakapokamilika ingawa hazitakuwa na mifereji ya maji ya mvua.

Akasema hatua hiyo inaondoa madimbwi katika maeneo mengi, hivyo kuharibu miundombinu ya mbu kuzaliana hatimaye kuzalisha vijidudu vya malaria.

Kadhalika, Mhandisi Magesa alisema Manispaa imefanikisha ujenzi wa daraja la watembea kwa miguu la Madaba liliojengwa ili kuunganisha kata ya Kigogo kwa na Mzimuni kwa upande wa Kinondoni na kugharimu sh.milioni 23.

Hata hivyo, akikagua ujenzi wa daraja hilo, Mbunge Azzan alisema hajaridhishwa na kiwango cha ujenzi wake, hasa baada ya nguzo moja kati ya nne zinazoshikilia daraja hilo kuanza kukatika.

Hali hiyo ilimlazimu Bw.Azzan kumfokea mhandishi aliyekuwa akisimamia ujenzi huo pamoja na timu yake kutoka idara ya ujenzi na uchumi ya Manispaa hiyo.

``Wakandarasi kama hawa hawapaswi kupewa tena tenda ya miradi yoyote ya ujenzi katika Manispaa hii na endapo ningekagua kabla hajamaliza ningeamuru anyang\'anywe kazi,``alisema.

Akihitimisha mazungumzo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira, Bw.Hassan Rajab alisema ofisi yake inahakikisha kuanzia sasa kila mradi unafanikishwa kuwa ufanisi ya hali ya juu ili kujenga imani kwa wananchi.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.