06 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Watoto wanaopata mimba nini kifanyike?
 
2008-02-06 08:49:54
Na Mwandishi Wetu

Suala la watoto kupata mimba linaendelea kujitokeza siku hadi siku, katika maeneo mbalimbali nchini.

Takwimu mbalimbali mashuleni, mikoani na zile za taifa zinaonyesha kuwa wasichana wanaopata mimba na kulazimika kukatiza masomo ni ushahidi tosha kuwa, tatizo hili lipo na linaendelea kuwatokea wasichana.

Sheria ya Elimu ipo wazi kuwa, msichana anayepata mimba ni lazima afukuzwe shuleni. Matokeo yake ni kwamba wasichana wanaopata mimba wamejikuta wakiathiriwa kwa kuondolewa shuleni bila ya kuzingatia uwezo wao darasani ulikuwa upi na malengo yao ya kimaisha yaliku nini.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta akifungua mkutano wa Kitaifa wa Vijana wa FeminaHIP kuhusu Uongozi wa Vijana kwenye Elimu ya VVU/Ukimwi na Ujinsia katika mazingira ya shule za sekondari nchini, alitoa changamoto ya kuchukuliwa kwa uzito unaostahili mjadala wa wizara hiyo kuhusu jinsi ya kuzuia mimba shuleni, jinsi ya kuwashughulikia wanaowapa mimba wanafunzi na kuangalia uwezekano wa kuwarudisha shuleni wanafunzi waliopata mimba baada ya kujifungua.

Waziri Sitta alisema kuwa watoto na vijana ni muhimu sana kwa taifa kwa sababu wamebeba matumaini.

Hata hivyo, makosa yamekuwa yakifanyika kwa kukosa mbinu na stadi za kuwasiliana nao kuhusu elimu ya ujinsia.

``Zamani jamii iliwasaidia sana vijana kukabiliana na changamoto za utu uzima kwa kutumia mfumo wa jando na unyago. Mila hii ilisaidia kuwaelimisha wasichana na wavulana juu ya ujinsia na kutambua wajibu wao.``

Anasema leo hii ni wachache tu wanaoendelea nayo na ukimya umetawala. Vijana wenyewe wanasema kuwa wanautamani sana uwazi na uwezo wa kuzungumza na wakubwa wao.

Hivyo anasisitiza haja ya kudumisha mila nzuri. ingawa anakiri kuwa kuna baadhi ya mila zimepitwa na wakati.

`` Tuchambue mila zetu kwa lengo la kuziendeleza zilizo nzuri na hasa zile zinazohusu umuhimu wa kujitunza. Tuzungumze na watoto wetu na kuwapa taarifa sahihi.``

Kwani anasema vijana hao wakiwezeshwa kwa kuwapa taarifa sahihi watatoa mchango mzuri zaidi. Hivyo anasema wasikilizwe na kuheshimu mawazo yao mazuri.

Waziri alisema kuwa ni muhimu wazazi kuwa na msimamo lakini pia watoto na vijana wasilikizwe wanasema nini.

Waonekana kama ni wadau wetu kwani wanajua wanachokihitaji. Wapewe taarifa za ukweli juu ya haki, ujinsia, kukua na kujikinga na VVU.

Kwavile wakipatiwa uwezo wa kujiamini watakuwa wamepatiwa zawadi kubwa.Katika mazingira hayo ni muhimu apewe stadi za maisha.

Na kuwataka wazazi na walimu kushirikiana katika kuwasaidia vijana na watoto kuhusu masuala hayo.

Waziri Sitta alisema kuwa mfumo wa elimu lazima utumike kutoa elimu ya ujinsia na stadi za maisha kwa sababu kuna sera na miongozo inayohusu masuala hayo.Ukimwi,Ujinsia na stadi za maisha zimeingizwa katika mitaala ya elimu kwa kuzingatia viwango vya wanafunzi.

``Tunahitajika kuwa wazi kuhusu ujinsia na mahusiano binafsi na ujinsia.Tusiwanyime vijana haki yao ya kupata taarifa hizo. Vijana wanahitajika pia kupewa haki yao ya huduma. Wanahitajika kujua juu ya mahusiano na ujinsia, elimu ya afya na uzazi ili kulinda maisha yao.

Alisema wanafunzi wanashauriwa kuwa mstari wa mbele kwa kujihusisha kwenye shughuli tofauti kama vile klabu, elimu rika, michezo ya kuigiza wakisaidiwa na walimu wao.

Kuhusu FeminaHIP, alisema kuwa anafahamu kuwa ni programu zilizopo katika shule za sekondari, ikisambaza jarida la Fema na kuhimiza uanzishawaji wa klabu hizo katika shule za sekondari. Pia taasisi hiyo inaamini kwamba uwazi ni muhimu katika masuala ya ujinsia na Ukimwi.

Jarida la Fema limekuwa rafiki, mshauri wa vijana na chombo chao muhimu cha mawasiliano ambapo baadhi hushiriki kwa kutoa habari na utatuzi wa matatizo yao.

Aliwapongeza FeminaHIP kwa kutoa nakala 92,000 za jarida la Fema ambalo hutolewa bure katika shule za sekondari nchini.

``Hapa nchini tuna shule za sekondari zaidi ya 3,000 na tunaomba ikiwezekana shule zote zipate jarida hili ili wanafunzi wote wanufaike na elimu hii, kwani wanafunzi wa shule zote nchini za serikali na zisizo za serikali zinakabiliwa na changamoto zinazofanana.

Waziri Sitta alikiri kuwa Fema ni chombo ambacho hata watu wazima huelimishwa, kuburudishwa na kuwezeshwa kuzisikia sauti za vijana na kwamba walimu wote nchini Tanzania wanapaswa kulijua jarida hili, ambalo hubeba makala zinazowalenga wao na jinsi ya kuibua mawasiliano baina ya wazazi na watoto.

Mkurugenzi Mtendaji wa FeminaHIP, Dk. Minou Fuglesang akizungumzia kuhusu mada za mkutano huo, alisema kuwa zilichaguliwa kwa sababu kila kijana ana haki ya kupata elimu ya VVU, Ukimwi na Ujinsia.

Pamoja na ukweli kwamba Tanzania kuna sera na miongozo mbalimbali kuhusiana na suala hilo, hakuna vyanzo mbalimbali na vya kutosha kuwezesha utoaji wa elimu hii, ikiwa ni pamoja na machapisho na kutokuwepo kwa mafunzo ya kutosha ya elimu hii kwa walimu.

``Wakiwezeshwa, vijana wanaweza kutoa mchango wao katika eneo hilo katika mikono yao,`` alisema.

Dk. Fuglesang alisema, kwa sasa kuna klabu za Fema zaidi ya 450 nchini ambapo wanachama wa klabu hizo wamekuwa wakielimishana kuhusiana na masuala mbalimbali kama vile ujinsia na VVU/Ukimwi, lakini pamoja na mafanikio hayo klabu nyingi zaidi zinatakiwa kuanzishwa ziwe za Fema na zinazofanana na hizo zikilenga utoaji wa Elimu ya Ujinsia na VVU/Ukimwi hivyo kuhakikisha kuwa vijana wanashiriki kwenye uongozi katika eneo hilo.

Mkuu wa SIDA-Sweden nchini , Bw Torbjorn Pettersson, alisema kuwa mada muhimu sana kuhusu vijana wadogo wanaoingia utu uzima na kukabiliana na suala la kujamiiana ni uwazi na uwajibikaji.

``Ni mada ambayo ni nyeti katika tamaduni zote. Imekuwa ikichukuliwa kuwa ni suala binafsi ambalo linawahusu watu wazima tu. Ni nyeti kwa sababu ndio njia ya kuzaliana kwa mwanamume na mwanamke kukutana na kwamba suala hilo linahitaji kuelimishana hata kwa watu wakubwa``.

Akiwa baba wa watoto watatu, alisema kuwa anawajibika kuwa mfano kwa watoto wake akijadiliana nao kuhusu suala hilo la wao kuingia katika daraja la ujana na utu uzima.

``Maarifa makubwa kwa baba ni vitendo vyako na sio maneno tu. Sweden katika nusu ya karne iliyopita ilikuwa ni nchi ambayo haijaendelea, watu wengi hawana ajira, familia kubwa, utapiamlo na vifo vingi vya watoto.Wanawake waliishi katika hofu ya kupata mimba, kutoa mimba kwa njia haramu na mengine. Lakini kwa njia ya elimu imeleta msukumo wa mabadiliko makubwa,`` alisema.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.