06 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wenye uhaba wa chakula wasaidiwe
 
2008-02-06 08:47:33
Na Mhariri

Hali ya uhaba wa chakula, imeripotiwa kutokea katika sehemu tofauti za nchi, hivyo kusababisha hatari ya kuwapo baa la njaa.

Juzi, gazeti hili liliripoti taarifa za uhaba wa chakula katika halmashauri ya manispaa ya Singida, inayohitaji msaada wa tani 3,119 ili kunusuru maisha ya wananchi wake.

Licha ya uhaba kuwapo wilayani Singida, taarifa zilizokaririwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, zilibaini kuwapo uhaba wa chakula katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Kama ilivyotokea wilayani Sindiga, ambapo wananchi wake wanadaiwa kula matunda aina ya zambarau, wakazi wa baadhi ya maeneo ya Lindi na Mtwara, wanadaiwa kula matunda pori na mizizi.

Taarifa hizo zinadhihirisha wazi kuwa, hali ya upatikanaji wa chakula cha kutosha hivi sasa si nzuri katika maeneo mengi nchini, hivyo hatua za haraka zinapaswa kutekelezwa, ili kuzuia hatari zinazoweza kutokea.

Alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) hivi karibuni, pamoja na mambo mengine, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Steven Wasira, alizungumzia upungufu wa chakula uliopo katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Hata hivyo, akasema taarifa zilizopatikana kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, zilieleza kutokuwapo kiwango kikubwa cha uhaba wa chakula, na kwamba wizara yake, ilimuagiza (Mkuu wa Mkoa), kuwasilisha takwimu za kiasi halisi cha chakula kinachohitajika.

Kwetu sisi, suala la kiwango cha chakula kinachohitajika kwa wananchi wanaokabiliwa na njaa, ni hoja ya msingi, lakini wizara na mamlaka husika, zinapaswa kwenda mbele na kusubiri kujua kiwango hicho.

Lakini uzoefu unaonyesha kuwa, viongozi wengi wa Serikali, hasa katika ngazi za mikoa na wilaya, wamekuwa na kasumba ya kuwatuma wasaidizi wao, kutembelea maeneo yenye matatizo, kama yale yanayokabiliwa na ukosefu wa chakula.

Miongoni mwa wasaidizi hao, wanashindwa kutambua umuhimu wa kuwa wazi katika kutoa taarifa sahihi, na hivyo kuwasilisha takwimu zisizolingana na uhalisia kwa Wakuu wao, ambao pia wanazitoa kwa Serikali Kuu.

Tunasema hivyo kwa sababu, tafsiri ya ukosefu wa chakula, ni jamii husika kukabiliwa na njaa, hivyo kuwa katika hatari ya kukabiliwa na vifo.

Tunatambua kuwa katika maeneo yaliyobainika kuwa na uhaba wa chakula, kuna watoto na wanawake, wakiwamo wajawazito, wanaohitaji lishe bora, ili waweze kukua ama kujifungua salama.

Hivyo, kwa kutambua umuhimu huo, uhaba wa chakula unapaswa kushughulikiwa kwa mkakati madhubuti, utakaowezesha wananchi, wakiwamo walio katika kada za wajawazito na watoto, kupata lishe na hivyo kuwa na afya bora.

Kwa vile matokeo ya mwisho yanayosababishwa na ukosefu wa chakula ni vifo, hatua za makusudi, kama vile usambazaji wa chakula kutoka katika hifadhi ya Taifa, kwenda kwa walengwa, zinapaswa kutekelezwa.

Serikali inatakiwa kufuatilia kwa karibu sana, habari zinazohusiana na ukosefu wa chakula, na kuchukua hatua za haraka, badala ya kutegemea mifumo yenye ukiritimba wa kukusanya taarifa na kushughukilia kadhia hiyo.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.