|
Umuhimu wa Lishe Bora kwa Jamii
2008-02-03 11:30:52
Na Badru Kimwaga
Ijumaa ya Februari Mosi, 2008 kituo cha Televisheni cha ITV kiliendesha kipindi cha Kipima Joto, kilichozungumzia masuala ya Lishe na Umuhimu wake kwa Jamii, ambapo Mwandishi wetu Badru Kimwaga alifuatilia kipindi hicho tangu mwanzo hadi mwisho.
Wageni waalikwa katika kipindi hicho walikuwa ni Dk Tumaini Martin Lema, Mkurugenzi wa zamani na wa kwanza wa Shirika la Chakula na Lishe Tanzania, aliyekuwa mzungumzaji mkuu, Bw. Nassor Mohammed na Bi Safina Maeda.
Mtangazaji Reinfred Masako alisema kuwa mada hiyo ya Lishe iliwekwa ili kuokoa kipindi baada ya mada iliyokuwa izungumzwe siku hiyo ya masuala ya Afya kushindikana kutokana na waalikwa toka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wote kushindwa kuitikia mualiko.
Kwa kuanza alimuuliza Dk. Lema, mtu anaposema lishe humaanisha ni chakula cha aina gani, ambapo msemaji huyo alisema kuwa lishe huwa ni matokeo ya kile kinacholiwa na mtu kama chakula.
Dk. Lema alifafanua kuwa ipo lishe nzuri ambayo humjenga mtu kiafya na kunawiri na lishe mbaya inayomsababishia mtu madhara kama kuugua, kuwa na upungufu wa damu na kukonda.
Alipoulizwa juu ya upungufu wa damu, alisema mara nyingi husababishwa na mtu kukosa kula vyakula vyenye wingi wa madini ya chuma, akidai madini hayo ndio huzalisha damu inayohitajika mno mwilini mwa mtu.
Alisema kuwa damu ni muhimu katika mwili wa binadamu kutokana na kazi yake kuwa ya kusaidia kusafirisha hewa ya Oxygen katika mapafu na kusambazwa mwilini mwa mtu katika kumpa uhai.
``Pia upungufu wa damu mara nyingi huwapata watu wanaugua malaria mara kwa mara na hasa watoto na mama wajawazito ambao uathirika sana,`` alisema.
Mtangazaji aliuliza juu ya kiriba tumbo na kutaka kujua husababishwa na nini na Dk. Lema, alisema kuwa hali hiyo hutokana na mtu kunenepa kupita kiasi kutokana mtu kuzidisha lishe, akidai ipo kiwango cha lishe cha chini, kati na juu na walao kwa kiwango cha juu hupata kiriba tumbo.
``Kwa kawaida mtu akinenepa kiasi huwa anatokwa na kitambi , lakini akizidisha lishe yaani kiwango cha juu hupata kiriba tumbo na hii huwapata hasa watu wasiofanya kazi ngumu au watu wa maofisini na wanaokula sukari na vinywaji ambavyo hubadilika na kuwa mafuta,`` Dk. Lema alisema.
Akasema pia suala la uchumi nalo huwaletea watu kiriba tumbo na hata mabadiliko ya makazi akitolea mfano wakazi wa vijijini kama wafanyakazi wa ndani wanapokuja mijini na kukutana na vyakula ambavyo walikuwa hawavipati watokapo hubadilika na kunenepa ovyo.
Hata hivyo alisema kwa kawaida watu wanaopatwa na matatizo hayo ni watu wa kipato cha kati na wathirika wakubwa watu wenye uwezo ambao hupata vyakula na vinywaji mara kwa mara ukilinganisha watu wa kipato cha chini.
Akatoa njia ya kukabiliana na hali hiyo ya kuwa na kiriba tumbo ni watu kupenda kufanya mazoezi angalau mara moja kila siku ilimradi watoke jasho na hasa wale wasiofanya kazi ngumu .
``Mwenye kijishamba basi alime ama kukimbia ili atoke jasho na kupunguza mafuta, pia wazidishe kula mboga za majani na matunda na kupunguza kula sukari nyingi ama bia,`` Dk. Lema alisema.
Alipogeukiwa Bw. Nassor, yeye alisema anahisi mazingira na kipato kidogo kinachangia mtu kula ilimradi bila kuzingatia mlo bora japo hutamani kula na kueleza ndio maana wapo wafanyao kazi ngumu, lakini wakala lishe duni na kupelekea kutokuwa na afya njema.
``Lishe bora kwa watu wengi ni tatizo kutokana na ukweli nchi yetu uchumi wake ni mdogo na raia wake kuwa na kipato duni cha kumuwezesha kula mlo kamili unaohitajika na hivyo kula chochote ili mradi bora liende,`` Bw Nassor alisema.
Hata hivyo msemaji huyo alimgeukia Dk. Lema na kumuuliza ni vyakula vya aina gani vinavyofaa kuliwa kwa kulingana na kazi ya mtu na katika mazingira ya joto ama baridi, ambapo alijibiwa kuwa mtu wa kazi ngumu ale vyakula vya kuongeza nguvu kama ugali na vinginevyo vyenye wanga.
``Kwa mazingira ya nchi yetu, suala la chakula gani kiliwe kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa si sana, ila kwa wenzetu wa nje kama Ulaya kwenye baridi kali kwa kawaida hula vyakula vyenye joto kwani mwili uhitaji mno joto, `` Dk. Lema.
Hata alisema upo umuhimu wa jamii kuelimishwa juu ya mpangilio wa vyakula kutokana na kazi zao ama majira jukumu alilodai lipo mikononi mwa Shirika la Chakula na Lishe, akidai vitabu vya namna hiyo vipo ila havijawafikia wananchi.
Alisema lau kama vitabu hivyo vya kuelimisha juu ya lishe bora ni wazi ingesaidia kuondoa matatizo ya kiafya yanayowakuta watu, ambapo watu hujikuta wanafanya kazi ngumu kama akina mama wa majumbani, lakini wakala mlo duni.
``Hata wajawazito wamekuwa wakipata matatizo na kuzaa watoto wadogo kwa vile hawapati mlo kamili kutokana na ukweli wao wamekuwa hawajui chochote kuhusu elimu ya lishe, kitu kinachopasa shirika la lishe kuelimisha umma,`` alisema.
Naye Bi. Maeda alipoulizwa kwa ufahamu wake juu ya Lishe kwa mtoto aliyezaliwa, alisema ni muhimu kupata maziwa ya mama ama maziwa ya kopo kwa wale ambao hawana maziwa mengi ama wanaotingwa na majukumu ya kikazi.
Pia alifafanua juu ya lishe nyingine zaidi ya maziwa ya mama ama ya kopo kama mchanganyiko wa nafaka kama mahindi, mtama, ulezi, karanga na vinginevyo, ambapo hata hivyo alisema tatizo la kiuchumi ni kikwazo cha kupatikana kwa lishe.
Dk. Lema aliweza kutoa ufafanuzi mzuri juu ya umuhimu wa mama wajawazito kulishwa vema wakati wakilea mimba na hata wanapojifungua na kusisitiza ubora na umuhimu wa maziwa ya mama kwa mtoto kabla ya lishe nyingine.
Alitaka watoto wanyonyeshwe maziwa ya mama na hasa yale ya awali ambayo wengi hudhani ni machafu, bila kujua kuwa ni kinga umuhimu kwa mtoto dhidi ya maradhi mbalimbali ikiwemo magonjwa ya tumbo na mengineyo.
``Wazazi wasidhubutu kuwalisha watoto wao kitu kingine hata kama ni maji katika muda wa chini ya miezi sita na badala yake wamnyonyeshe mtoto maziwa ya mama kumlisha vyakula vingine ni kuruhusu mtoto kupata maradhi mbalimbali,`` alisema.
Dk. Lema alisema hakuna kitu kibaya kama mtoto akalishwa maziwa ya kopo kwa kutumia chupa, akidai inachangia watoto wengi kupata bakteria na vijidudu vya maradhi mengine na kuwafanya waugue na kuwa dhaifu.
``Kuhusu suala la mtoto kuhara akiota meno ama kupityia mabadiliko mbalimbali ya ukuaji havina ukweli, bali ni vile mtoto analishwa vijidudu kutokana na kuwepo kwa mazingira machafu katika vyombo vya mtoto,`` Dk. Lema alifafanua.
Wachangiaji wengine wa mada hiyo kwa kupitia simu kama Oven wa Msasani, Happiness wa Mbezi, David Mabibo, Mama Hamida wa Morogoro na Ngaille wa Chuo Kikuu waliuliza maswali mengi juu ya lishe na kupewa majibu ya jumla na Dk. Lema na wengine wakisisitiza kipato duni ni tatizo la Watanzania wengi kupata lishe bora inayotakiwa kwa afya zao.
Dk. Lema alihitimisha kwa kufafanua tatizo la watu kupata Tezi la Shingo, akidai inatokana na ukosefu wa madini ya joto na kuwataka watu kula chumvi yenye madini hayo ili kujiepusha na ugonjwa huo.
Alisema ndio maana hata serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha ulaji wa chumvi yenye madini hayo na kusaidia kupunguza ugonjwa huo ambao kipindi cha nyuma uliwapata watu wengi kutokana na ardhi kukosa madini hayo na kupelekea mimea ya vyakula kutokuwa na madini ya Joto.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuwekwa kwa mtaala maalum mashuleni kwa ajili ya kufundisha masuala ya lishe ili jamii ianze kujua umuhimu wa lishe bora tangu sheni na hata wanapokuwa wakubwa isiwe ni tatizo kwao kutambua.
Aliwataka pia wanaume kubadilika na kudhani jukumu la masuala ya lishe ni la wanawake tu na kazi yao ni kutafuta fedha za vyakula na kukaa mezani kula tu.
Dk. Lema alilitaka shirika la Chakula na Lishe pamoja na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuhamasisha jamii katika umuhimu wa kuzingatia na kuipa kipaumbele masuala ya lishe bora ili kuwanusuru na kuugua mara kwa mara maradhi tofauti.
|