|
Haruna Moshi atemwa Stars, aitwa Boniface
2008-02-02 08:44:04
By Onesmo Kapinga
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo amemtema mshambuliaji wa Simba Haruna Moshi kwenye kikosi chake na badala yake amemwita Geofrey Boniface wa Prisons kuziba nafasi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Shirikisho la Soka Tanzania, Florian Kaijage alisema kuwa wachezaji wa Stars kesho wanatarajia kuingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Kimataifa ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Malawi itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa wa zamani jijini.
Kaijage alisema kuwa Maximo amechukua uamuzi huo kufuatia mchezaji huyo kutokuwepo nchini.
Alisema kuwa mchezaji mwengine aliyeitwa ni mlinzi wa kushoto wa Ashanti United Juma Jabu ambaye ataziba nafasi ya Uhuru Seleman wa Coastal Union ambapo inasemekana anajiandaa kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Hispania.
Wakati huohuo, Kaiage alisema kuwa timu ya taifa ya Malawi inatarajia kutua nchini kesho kwa ajili ya mchezo huo.
Kaijage alisema kuwa timu hiyo itawasili majira ya saa 11.00 jioni kwa Ndege ya Shirika la Malawi ikiwa na msafara wa wachezaji 20 na viongozi watano.
Alisema kuwa TFF limeamua kutangaza viingilio vya aina nne tofauti, ambapo viti maalumu watazamaji watalazimika kulipa sh. 15,000, jukwaa kuu sh. 10,000, watakaokaa jukwaa la kijani sh. 5,000 na mzunguko sh. 2,000.
Mechi hiyo ni kwa ajili ya kujiandaa na kutafuta nafasi ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Afrika Kusini mwaka 2010, ambapo Tanzania katika kampeni hizo itaanza kucheza na Cameroon wakati timu zingine katika kundi lake ni Mauritius na Cap Verde.
|