25 Oct 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Waziri afia katika ajali
 
2007-10-25 10:07:04
Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Salome Mbatia (55), amefariki dunia jana jioni baada ya gari lake kugongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Ilembula wilaya ya Njombe, mkoani Iringa.
Kwa mujibu wa Spika wa Bunge, Bw. Samwel Sitta, Waziri Mbatia alifariki pamoja na dereva wake na mtu mwingine ambaye hajafahamika.

Akiongea na Nipashe kwa njia ya simu jana, Bw. Sitta alisema lori hilo inasemekana lilikuwa limejaza shehena ya mbao na lilikuwa likitokea Makambako kwenda Njombe, mkoani Iringa.

Bi. Mbatia alikuwa njiani akitoa Songea kuelekea Iringa, katika ziara ya kikazi ya kuhamasisha ukemeaji wa mila potofu zinazowakandamiza wanawake.

Bw. Sitta, alisema ajali hiyo ilikuwa mbaya sana baada ya lori hilo kulilalia gari la waziri na kusababisa miili ya marehemu hao kutolewa kwa shida baada ya kubanwa na lori hilo.

Hata hivyo, alisema haikufahamika mara moja iwapo abiria mwingine aliyekuwa kwenye gari hilo alikuwa ni msaidizi wake ama ofisa aliyeambatana naye kutoka mkoani Iringa.

Alisema ofisi yake pamoja na ya Waziri Mkuu (Bunge) inatarajia kutoa taarifa zaidi leo.

Wakati huo huo Thobias Mwanakatwe wa PST Mbeya, anaripoti kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Dk. David Mathayo, aliyekuwepo eneo la tukio ambapo alisema ajali hiyo ilitokea saa 11.15 jioni ikilihusisha gari la Waziri na lori namba T299 AFJ.

Dk. Mathayo alisema lori hilo liligongana uso kwa uso na gari la Naibu Waziri eneo la Sankoti.

Naibu Waziri Mathayo, alikuwa safarini kwenda Tunduru kwa ziara ya kikazi mkoani Ruvuma.

Habari kutoka eneo hilo ambazo hazikuthibitishwa zilisema Waziri Mkuu Mstaafu Bw. Frederick Sumaye ni miongoni mwa watu waliokuwepo kwenye ziara pamoja na marehemu Mbatia.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Bw. Advocate Nyombi, alisema atatoa maelezo zaidi kuhusu ajali hiyo kwa vile hadi tunakwenda mitamboni alikuwa anakwenda eneo la tukio.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Wilaya ya Njombe ya Kibena.

Kabla ya kuwa Naibu katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto, aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango, Uchumi na Uwezeshaji.
Kwa mujibu wa wasifu wake, Marehemu Mbatia alizaliwa Juni 17, 1952 na kupata elimu katika Sekondari za Wasichana Korogwe pamoja na St. Joseph.

Alipata shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1973 na 1976. Mwaka 1982 hadi 1983 alipata shahada ya pili katika kozi ya Menejimenti ya Taasisi ya nchini Marekani.

Kiu yake ya kusoma ilimpeleka nchini Uholanzi mwaka 1987 alipojiunga na Taasisi ya RVB ya Delft-Holland, ambapo alitunukiwa diploma ya uzamili katika Utawala na Menejimenti.

Katika maisha yake alishika nyadhifa mbalimbali katika sekta ya umma na binafsi.

Hii ni ajali ya tatu inayohusisha magari kuwapata wabunge na mawaziri katika kipindi kisichozidi miezi miwili. Wa kwanza alikuwa Mbunge wa Mchinga (CCM) Bw. Mudhihir Mudhihir na kisha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Prof. Juma Kapuya.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.