03 May 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kutoa habari kwa ajili ya umma ni haki, si utashi
 
2007-05-03 09:37:20
Na Mhariri

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali hapa nchini leo wanaungana na waandishi wengine duniani katika kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ambayo inawapa fursa ya kutafakari jinsi uhuru huo muhimu unavyoruhusiwa kufanya kazi nchini.

Hii ni siku ambayo huwakutanisha waandishi na wadau mbalimbali wa habari nchini katika kutafakari jinsi ambavyo wananchi wanapata habari sahihi kwa wakati na waandishi nao wanapata mazingira bora ya ukusanyaji wa habari hizo.

Kimsingi dhana ya uhuru wa vyombo vya habari ni miongoni mwa haki muhimu za binadamu ambazo zimeainishwa kwenye Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU) ambapo Tanzania pia imeridhia.

Hata hivyo, katika tahariri fupi kama hii siyo rahisi kuweza kufafanua kwa kina maana halisi ya uhuru huu wa habari na athari zake iwapo haupatikani.

Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAJA) leo kimeandaa hafla maalum katika Ukumbi wa Karimjee uliopo Dar es Salaam kwa ajili ya kuwakutanisha wadau mbalimbali wa habari nchini ili kuweza kukaa pamoja na kutafakari mambo ya msingi kuhusiana na uhuru wa habari Tanzania.

Rais wa TAJA, Bw. Hamza Kondo aliliambia gazeti hili jana kwamba hafla hiyo imelenga hasa kuwapa fursa waandishi wa habari na wadau wote wa habari kwa ujumla nchini kuweza kuangalia jinsi ambavyo uhuru huu unaweza kuboreshwa zaidi.

Ni lazima ikaeleweka kwamba kila mtu anayo haki kamili ya kikatiba ya kukusanya, kupokea, kusambaza, kuzungumza, kusikiliza, kutazama na kujadili habari mbalimbali ilimradi havunji sheria.

Lakini tatizo ambalo limekuwa likijitokeza ni hii hali ya baadhi ya watoaji habari, tena ambao wapo kwenye utumishi wa umma kuamua kukwepa au kugoma kutoa habari hizo kwa vyombo vya habari kwa ajili ya umma wanaodai kuutumikia.

Baadhi ya watendaji hawa hudai kuwa eti habari kama hizo ni nyeti au siri kubwa ambapo haziruhusiwi kuchapishwa au kutangazwa kwenye vyombo vya habari kwa sababu za kiusalama wa taifa!

Hali kama hiyo ndiyo ambayo imekuwa ikisababisha baadhi ya habari kuandikwa na kutangazwa zikiwa hazijakamilika au kutolewa zikiwa na makosa kwa vile watoa habari hao hushindwa kutoa ushirikiano unaostahili.

Halikadhalika kuna watoa habari ambao hujenga dhana potofu kwamba vyombo vya habari vipo kwa ajili ya kuandika habari mbaya tu na hivyo waandishi wa habari ni watu wa kuogopwa na kukimbiwa.

Dahana kama hizi ndizo ambazo zimekuwa zikileta migongano baina ya waandishi wa habari na watoa habari.

Bila kujadili kilichomo katika ule muswada tata wa habari, sisi tunatoa wito kwamba katika siku kama ya leo ambapo wadau wa habari wanaadhimisha Siku ya Uhuru wa Habari Duniani ni vyema viongozi katika ngazi mbalimbali wakabadilika na kuona kwamba utoaji wa habari ni jambo la haki na siyo ridhaa ya mtoa habari.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.