|
WOWAP waja na mbinu ya kufunda bila kukeketa
2007-05-02 10:23:05
Na Mwandishi Wetu
Wanawake Amkeni, maarufu kama Women Wake Up (WOWAP) ni shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa mwaka 1996, mkoani Dodoma kwa lengo la kupambana na mila potovu ya ukeketaji mwanamke na kuelimisha njia mbadala zisizo athiri mila na desturi ya kabila husika.
Shirika hilo ambalo ofisi yake kuu ipo mkoani Dodoma na imefungua tawi katika mkoa wa Tanga na limedhamiria kuelimisha jamii kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kama ukeketaji na vingine kupitia mpango shirikishi wa jamii.
Wanawake wengi katika nchi zinazoendelea wanakumbana na matatizo mengi ya kijamii kama vile ubaguzi, umaskini na unyanyasaji wa kijinsia.
Kutokana na matatizo hayo hata nafasi ya ushiriki wa wanawake katika masuala ya kiuchumi ni ndogo ambapo baadhi ya tamaduni nyingi za Kiafrika humchukulia mwanamke kama mtu asiye na maamuzi yake kuhusu kila kitu chake.
WOWAP limekuwa likitumia njia mbadala kuwafunda watoto wa kike wanaoingia katika utu uzima, bila ya kuwakeketa, ili kuionyesha jamii kuwa sio mila zote ambazo hazifai, bali baadhi zinafaa kudumishwa na husaidia msichana akawa na tabia nzuri katika jamii.
Moja ya mila nzuri, ambayo shirika hilo limekuwa likiitumia kuwaelimisha wananchi na watoto wa kike, wanaovunja ungo, ni kuwaweka ndani wakati wa likizo ndefu na kuwafundisha usafi, jinsi ya kuwaheshimu watu wote, kujithamini na kuwa waaminifu pindi watakapoolewa.
Shirika hilo hukusanya wasichana wa kijiji kizima na kuwapeleka katika kambi iliyo mbali na wazazi wao ambapo huishi wakipewa mafundisho mbalimbali na bibi zao bila ya kuwakeketa.
Sababu moja inayowafanya baadhi ya wazazi kuwakeketa watoto wao wa kike ni ile ya kuwafanya wawe waaminifu katika ndoa zao wakiamini kuwa wakishakeketwa watapunguza hamu za kufanya mapenzi, na pia kuwa wajasiri pale wanapofikwa na machungu mbali mbali kimaisha.
Sababu nyingine wasichana na wazazi hutaka kupata zawadi siku ya sherehehe ya kuwatoa ndani ya mabinti zao, hivyo wanafikirikuwa wasipowfanyia vitendo hivyo hawatapata fursa ya kupata zawadi hizo.
Njia hiyo mbadala inayotumiwa na WOWAP imekuwa ikifanywa kwa kutumia njia zote ambazo kabila husika huzitumia katika kumfunda mtoto wa kike ikiwa ni pamoja na kufanya sherehe siku ya mwisho na kuwapa zawadi wazazi na mabinti hao.
Kitendo hicho kimewasaidia baadhi ya vijiji ambavyo tayari baadhi ya mabinti walifundwa kwa njia mbadala na kuona umuhimu wake, badala ya kuwakeketa na kuishi kupata maumivu.
Hata hivyo pamoja na njia hiyo, wapo baadhi ya wazazi na mangariba ambao wamebuni njia mpya ya kuwakeketa watoto, mara tu wazaliwapo, kwa lengo la kukwepa mkono wa sheria.
Njia hiyo wakati mwingine hufanywa na mangariba bila wazazi kujua, ambapo bibi huongea na mkunga wa j adi au ngariba wakati wanapomsaidia mwanamke kujifungua na kumkeketa mtoto.
Wakati huo mwanamke huwa amechoka au ana maumivu ya kujifungua, hutumia mwanya huo kumkeketa mtoto wake, na anapokuja kugundua baadaye anakuwa ameshatishwa na wazazi wake na hivyo hukosa la kufanya.
Kutokana na hali hiyo na kuhakikisha kuwa elimu hiyo inawafikia wananchi wengi ndani na nje ya mkoa wa Dodoma, hivi karibuni wanaharakati mkoani Dodoma waliadhimisha siku ya kuzuia ukeketaji duniani, ambapo ulimwenguni kote siku hiyo huadhimishwa kila tarehe 6 Februari.
Wanaharakati walioadhamisha siku hiyo ni kutoka katika mashirika ya (DIAC), (WOWAP) na shirika la (AFNET).
Mashirika hayo yaliungana kwa pamoja katika kuunganisha nguvu katika kutoa sauti ambayo itawafikia wengi kwa wakati muafaka ili waweze kutambua madhara mbali mbali yanayompata mwanamke aliye keketwa.
Katika maadhimisho hayo ilibainika kuwa ukeketaji nchini bado ni kikwazo kikubwa cha maendeleo hasa kwa wanawake, ambapo mkoa wa Arusha ndio unaongoza kwa vitendo hivyo kwa asilimia 81, ukifuatiwa na Mkoa wa Dodoma kwa asilimia 67, huku mikoa ya Mara, Tanga, Kiliamnjaro na Singida ikifuatia kwa asilimia kati ya 25 na 36.
Takwimu hizi ni uthibitisho tosha kuwa vitendo hivi bado vinaendelea kwa kiasi kikubwa hapa nchini na hasa katika maeneo ya vijijni ambako vitendo hivyo vinafanywa kwa kiasi cha kutisha licha ya mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa elimu juu ya madhara ya ukeketaji kwa wanawake na watoto wa kike.
Licha ya mashirika hayo kuwa mstari wa mbele katika kampeni za kupiga vita vitendo hivyo, yamekuwa yakipata vikwazo mbalimbali ambavyo vimekuwa vikikwamisha juhudi hizo ambazo zinaungwa mkono kwa kiasi kidogo na serikali.
Moja kati ya vikwazo hivyo ni pamoja na sheria ya makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998 kifungu cha 16A kifungu ambacho kimekuwa kina mapungufu na kufanya maamuzi kuwa magumu.
Katika kifungu cha 16A cha sheria ya adhabu, mtu anayebainika kumkeketa mtoto wa kike huhukumiwa kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya shilingi laki tatu au kulipa fidia mwanamke ambaye amefanyiwa kitendo cha ukeketaji, au vyote kwa pamoja.
Adhabu hii ni ndogo sana ikilinganishwa na kitendo chenyewe kilivyo cha ukatili na mara nyingine mwanamke anaweza kufa na kupata ulemavu wa maisha.
Ni vigumu sana kulimaliza tatizo hili kama serikali haitaungana na wadau mbalimbali wanaohusika katika kupiga vita ukeketaji yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali kupinga kwa nguvu zote ukeketaji kwa mama na mtoto wa kike.
Kadhalika kuzifanyia marekebisho sheria ambazo zinazotoa adhabu ndogo kwa wahusika wa vitendo hivyo, na kuwaelimisha viongozi wa vijiji na wananchi juu ya ukatili huo, ili kazi hiyo iweze kufanywa kwa nguvu ya pamoja kama ilivyo kwa majanga mengine kama ukimwi na malaria.
Iwapo serikali italikemea kwa nguvu zote suala la kupokea rushwa ndogondogo kwa baadhi ya watumishi kwa ngazi za vijiji, wilaya na katika vyombo vya dola, vitendo hivyo vinaweza kuisha miongoni mwa jamii.
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, itenge fedha kwa ajili ya kuanzisha kitengo maalum cha kuelimisha jamii madhara ya mila potofu kupitia televisheni, redio, mikutano ya hadhara ya vijiji na kwenye mihadhara ya dini.
Hakuna lisilo wezekana, kama tulivyoweza kutokomeza magonjwa sugu ambayo hapo awali yalikuwa yakisumbua jamii kama pepo punda na magonjwa mengine, tunaweza kutokomeza ukeketaji mwanamke, kama njia hizo zitatumika kikamilifu.
|