|
Mazingira yaboreshwe kuvutia wataalam vijijini
2007-05-02 10:22:22
Na Mhariri
Pamoja na Tanzania hivi sasa kuonekana inajitahidi katika kuongeza idadi ya vyuo vinavyotoa elimu ya juu katika taaluma mbalimbali, bado kuna upungufu mkubwa wa wataalam hasa katika maeneo ya vijijini kutokana na mazingira mabovu.
Baadhi ya wataalam ambao upungufu wao umekuwa na athari kubwa kwa wananchi waishio vijijini ni madaktari, wauguzi, walimu, mabwanashamba, waganga wa mifugo na kadhalika.
Hali hii imekuwa ikiwasababishia wananchi hao kulazimika kutembea kwa miguu umbali mrefu kwa ajili ya kupata huduma. Kuna taarifa za vijiji kuwa na zahanati lakini zikiwa hazina watendaji ama shule zikiwa na walimu pungufu.
Serikali mara kadhaa imekuwa ikiwahimiza wahitimu wa taaluma mbalimbali wanaobahatika kupata ajira kwenda katika vituo walivyopangiwa ili kuwapunguzia kero wananchi wanaoishi vijijini.
Hata hivyo, waajiriwa wengi wanaopangiwa vituo vilivyopo katika mazingira mabaya huishia kuripoti au kutokwenda kabisa katika vituo hivyo.
Ijumaa iliyopita, mathalani, serikali ilitangaza kusudio lake la kuajiri mabwanashamba 2,500 katika mwaka huu wa fedha ili waweze kuwa karibu zaidi na wakulima.
Kauli hiyo ilitamkwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Stephen Wassira wakati alipokuwa akizindua Bodi ya Wakala wa Mbegu za Mazao jijini Dar es Salaam.
Waziri huyo alisema kwamba serikali itahakikisha kwamba mabwanashamba hao watakaoajiriwa watakwenda kufanya kazi zao na kuishi vijijini na siyo mijini kama ilivyozoeleka katika siku za nyuma.
Halikadhalika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nayo hivi karibuni ilitangaza kuwa na mikakati ya kuwajengea nyumba bora walimu katika maeneo mbalimbali nchini, hususan vijijini.
Hakika hata sisi tunaona kwamba kuna haja kubwa sasa kuhakikisha kwamba kunajengwa mikakati ambayo walau inawezesha kuwepo na mahitaji ya msingi vijijini ili kuwavutia wataalam mbalimbali.
Tuna hakika kwamba yapo mambo ambayo kama wananchi wa maeneo hayo wanawezeshwa na kushirikishwa yanaweza kuwa vivutio kikubwa kwa wataalam hawa kama walimu, madaktari, wauguzi, mabwanashamba na kadhalika.
Ujenzi wa nyumba za watumishi unaweza kushirikisha nguvu za wananchi kwa kutumia fedha zinazotolewa na mifuko kama vile Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na mingineyo nchini.
Serikali nayo katika mipango yake ya muda mrefu inatakiwa kuangalia maeneo kama hayo na kuboresha miundombinu na hasa barabara.
Kivutio kingine ni kutoa mishahara na vivutio vingine vya marupurupu ambavyo vitakuwa ni vya upendeleo maalum kwa wanaofanya kazi katika maeneo yenye mazingira magumu.
Mpaka sasa hatujui ni kwa nini baadhi ya marupurupu ama mishahara minono wanapewa wafanyakazi, tuseme, wa cheo kilekile walioko mijini badala ya vijijini eti kwa maelezo kuwa hali ya maisha vijijini ni ya chini.
Tunadhani kwamba dhana hii tunapaswa kuanza kuibadili na kuwa kinyume chake ili kuwavutia watendaji kwenda kufanya kazi vijijini.
Utaratibu wa ulipaji wa mishahara nao unatakiwa kuboreshwa badala ya kuwafanya watumishi kusafiri umbali mrefu na wakati mwingine kulazimika kulala kwenye nyumba za kulala wageni, wakati mwingine hadi wiki nzima kusubiri malipo yao!
Watumishi wa maeneo haya vilevile waangaliwe kwa karibu jinsi ambavyo wanaweza wakaendelezwa kitaaluma hasa ikizingatiwa kwamba wengine huogopa kuripoti maeneo hayo kwa hofu kwamba husahauliwa kwa masomo ya kujiendeleza kwa vile wapo `shamba`.
Siyo sahihi kabisa kudhani kwamba wasomi au wataalam wote hugoma kuripoti katika sehemu wanazopangiwa kufanya kazi eti tu kwa sababu hazina umeme au maji ya bomba bali ni mambo kama hayo tuliyoyabainisha hapo juu!
|