01 May 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wafanyakazi imarisheni mshikamano
 
2007-05-01 10:29:59
Na Mhariri

Wafanyakazi wa Tanzania leo wanaungana na wafanyakazi wengine duniani katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi Ulimwenguni.

Hii ni siku ambayo wafanyakazi hutafakari mafanikio na matatizo ambayo wameyapata katika kipindi cha mwaka mzima.

Siku kama ya leo wafanyakazi, hasa waliopo katika utumishi wa umma au serikalini, hutega masikio yao kuwasikiliza viongozi wakuu serikali, na hasa rais kuona kama atapandisha viwango vya mishahara.

Kwa lugha nyingine wafanyakazi wengi hupima mafanikio yao katika sehemu zao za kazi kulingana na kiwango ambacho wanalipwa mishahara.

Lakini sisi tunadhani kwamba katika siku kama ya leo, wafanyakazi wa Tanzania, ikiwa ni pamoja na walio katika sekta binafsi, wanatakiwa pia kufikiria zaidi ya mishahara au marupurupu wanayopata katika sehemu zao mbalimbali za kazi.

Kuna haja kubwa ya kuangalia ni kwa jinsi gani wao wenyewe wanashirikiana katika sehemu zao za kazi katika kuongeza tija.

Vilevile ipo haja ya kuangalia ni kwa kiwango gani wao kama watumishi wa taasisi moja wanavyoshirikiana na watumishi wa taasisi nyingine.

Katika siku kama hii, pamoja na wafanyakazi bora mbalimbali kuzawadiwa kutokana na utumishi uliotukuka, ni lazima wafanyakazi wa Tanzania waitumie siku hii katika kutafakari namna ya kubuni ama kuwataka waajiri kuwasaidia njia mbalimbali ambazo zinaweza kuinua kipato chao nje ya ajira, alimradi shughuli hizo za binafsi zisiathiri utendaji wao wa kila siku.

Baadhi ya vitu ambavyo vinaweza kuinua mapato ya wafanyakazi ni kubuni miradi mbalimbali au vitegauchumi kama ilivyofanywa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambacho hivi karibuni kimezindua jengo lake la kitegauchumi jijini Dar es Salaam.

Tunaamini kwamba kama panakuwepo na uongozi na usimamizi sahihi wafanyakazi wa Tanzania wanaweza kuwezeshwa na wakaanzisha miradi inayoweza kuboresha hali zao za maisha.

Kuna haja pia kwa serikali kuvipa nguvu vyama mbalimbali vya wafanyakazi nchini katika kuhakikisha kwamba wanafikia malengo ya kutetea haki za wadau wao.

Wafanyakazi katika maeneo mbalimbali wanatakiwa kujenga hali ambayo itazidi kuwafanya wawe katika mazingira ya kuishi kama ndugu wa tumbo moja.

Kwa upande wa serikali, pamoja na kupandisha viwango vya mishahara, wimbo mtamu ambao wengi wangependa kuusikia leo, serikali ni vyema ikaangalia namna ambavyo inaweza kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali nchini.

Kunakuwa hakuna maana yoyote iwapo kiwango cha mshahara kinapandishwa na bei za bidhaa nazo zikapanda maradufu.

Kila la heri wafanyakazi wa Tanzania. Ongezeni mshikamano na kufanya kazi kwa bidii ili kuinua pato la taifa na vipato vyenu kwa ujumla.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.