|
Ili iweze kwenda na wakati TPRI inahitaji msukumo zaidi
2007-05-01 10:28:21
Na Mwandishi Wetu
Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu (pesticides) katika nchi za Kitropki ijulikanayo kama ``Tropical Pesticides Research Institute (TPRI)``ya jijini Arusha ni chombo muhimu cha utafiti kwa sekta nyingi hasa ya kilimo.
Licha ya taasisi hiyo Kuwepo kwa miaka mingi, bado inakabiliwa na changamoto nyingi na matatizo mengi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa fedha na vifaa vya kufanyia utafiti kama anavyoelezea Mwandishi wetu wa PST.
KITUO cha TPRI katika miaka ya 1950 hadi mwaka 1962 kilikuwa kinajulikana kama ``Colonial Insecticides Research Unit``, na makao yake yalikuwa Entebe nchini Uganda.
`Kwenye miaka 1962-1977 kilikuwa Taasisi chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla ya kuvunjika mwaka 1977 na baadaye TPRI kiliwekwa chini ya Wizara ya Mipango na baadaye Wizara ya Kilimo.
Jukumu kubwa la taasisi hii ni kufanya utafiti wa ubunifu kwa ajili ya kutoa huduma zinazohusu udhibiti wa visumbufu, viuatilifu na bionuwai kwa kushirikiana na wadau ambao ni pamoja na sekta za serikali, sekta binafsi, serikali za mitaa, Mashirika ya umma na yasiyo ya kiserikali, Jumuia ya Afrika Mashariki na Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
TPRI pia inashughulikia masuala ya hifadhi na utunzaji wa mazingira na ekolojia na biolojia ya viumbe.
Azma kubwa ya TPRI ni kuwa endelevu katika utafiti wa sayansi na teknolojia na kuwa na ubora wa ubunifu katika utafiti husishi kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya visumbufu na magonjwa ya mimea, mifugo na binadamu, ufuatiliaji wa matumizi ya viuatilifu, na utunzaji wa bionuwai ili kuboresha maisha ya watu na viumbe.
Taasisi hii kwa kiasi kikubwa inatoa mafunzo kuhusu udhibiti wa visumbufu, matumizi sahihi ya viuatilifu, utunzaji wa bustani ya kuhifadhi mimea na uoto wa asili, kilimo endelevu na kutafiti mbinu za kitaalam na kanuni bora za kilimo.
TPRI inajihusisha pia na Usajili na udhibiti wa viuatilifu vya mazao, mifugo na binadamu.
Vile vile inafanya usajili wa viuatilifu vya kudhibiti visumbufu na magonjwa ya mimea kwa niaba ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, chini ya sheria ya Kudhibiti Visumbufu vya Mimea ya Mwaka 1997.
Aidha inadhibiti wadudu waenezao magonjwa ya mifugo na binadamu kama vile mbung`o kwa kutumia vitambaa vyenye viuatilifu au vivutia harufu (odour attractants), ukaguzi wa viuatilifu kwenye maduka, ghala na mipakani, sambamba na udhibiti wa mbu kwa kutoa utaalamu wa kuweka viuatilifu kwenye vyandarua, mapazia na mablanketi.
Uchunguzi wa ubora na usafi wa mimea na mazao kabla ya kuingizwa ndani ya nchi au kusafirishwa nje ya nchi hufanywa na taasisi hii. Pia, husimamia matumizi endelevu ya hazina ya nasaba za mimea na kuhifadhi kumbukumbu zake.
TPRI inalinda soko la ndani na nje kwa kudhibiti masalia ya viuatilifu kwenye mazao, mbegu, kwenye bidhaa zitokanazo na mimea na wanyama, na kwenye mazingira kwa ujumla.
Masuala haya ni muhimu sana kwenye ulimwengu wa leo kwa sababu wateja hawapendelei mazao au bidhaa za kilimo zenye masalia ya viuatilifu na madawa mengine ya kilimo yanayozidi viwango vya kimataifa vilivyokubalika.
Walaji wana wasiwasi wa kupata magonjwa kama mzio (allergy) au saratani, yatokanayo na kemikali zilizozidi viwango.
Kutokana na kuwekwa chini ya Wizara ya Mipango na baadaye Kilimo baada ya Jumuiya kuvunjika, TPRI ilikosa nguzo na muhimili imara wa kujisimamia kama taasisi yenye umuhimu wa kipekee.
Kutokana na umuhimu wake kwa Taifa, taasisi kama TPRI haipaswi kuwa moja ya Taasisi chini ya idara ya Wizara moja tu ya Kilimo wakati inawajibika kuhudumia karibu kila wizara na sekta mbalimbali.
TPRI inapashwa kuwa na uwanja mpana wa kuhudumia kila nyanja hapa nchini na hivyo kutengewa fedha za kutosha za kuiwezesha kutoa huduma za utafiti wenye tija kwa taifa.
Kwa sasa TPRI inaendeshwa kwa kiwango kikubwa kwa fedha kidogo kutoka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ambazo haziwezi kutosheleza matakwa ya utafiti.
Michango ya fedha za utafiti inayotoka Wizara nyingine kama Wizara ya Mifugo na Afya kwenda TPRI ni kidogo sana ikilinganishwa na mahitaji.
Kwa mfano asilimia 63 ya fungu la fedha linalopelekwa na Wizara ya Kilimo pale TPRI linatumika kulipa mishahara ya wafanyakazi, utawala hutumia asilimia 32 na shughuli za utafiti zinatengewa asilimia 3 hadi 5 tu jambo ambalo linachangia kurudisha nyuma shughuli na maendeleo ya utafiti ambao ni muhimu sana kwa taifa.
Kwenye taasisi za nchi zinazoendelea haraka, bajeti ya utafiti ndio huwa kubwa na kupewa kipaumbele kuliko masuala mengine. Hapa kwetu bajeti ya mishahara ndio inayopewa umuhimu mkubwa na kipaumbele.
Lakini ni jambo la kusikitisha ni kwamba Tanzania inatenga asilimia 0.02% tu ya bajeti nzima kwa ajili ya utafiti badala ya asilimia 1 iliyojiwekea zaidi ya miaka kumi iliyopita.
Bila kuwekeza kikamilifu kwenye utafiti wa sayansi na teknolojia na nyanja nyingine muhimu za uchumi (strategic areas) itakuwa vigumu sana kwa nchi yetu kupata maendeleo ya haraka.
Kwa ujumla Taasisi hii ni nguzo muhimu hasa tunapoelekea katika muungano wa Jumuia ya Afrika Mashariki ambapo kwa wenzetu wa Kenya na Uganda taasisi kama TPRI, mfano ``Kenya Plant Health Inspectorate Services (KEPHIS)``, ``Kenya Agricultural Research Institute (KARI)``, ``Uganda National Agricultural Research Organization (NARO), ziko mbali kiutafiti, tofauti na Tanzania ambapo bado tuko nyuma hata katika mfumo wa utendaji wa taasisi yenyewe.
Kwa mfano hivi sasa nchi jirani ya Kenya iko mbali katika utafiti juu ya uwezekano wa kuwa na mfumo wa kilimo cha tija kinachotumia teknolojia na mbinu za kisasa zinazofuata taratibu za kilimo chenye ubora wa kimataifa na teknolojia za kisasa.
Pia Kenya na Uganda zimeanza utafiti wa teknolojia za jenetiki za kukuza mimea ya mazao haraka na kuzalisha kwa wingi; teknolojia zinazowezesha mimea kujikinga na wadudu na magonjwa hivyo kupunguza matumizi ya dawa za kuua wadudu waharibifu (viuatilifu); na teknolojia za uzalishaji wa mazao na bidhaa za kilimo zinazozingatia hifadhi ya mazingira na uzalishaji kwa viwango na ubora unaohitajika kwenye soko la kimataifa.
Lakini Tanzania ndiyo kwanza ipo katika hatua ya kuandaa sera ya matumizi ya teknolojia ya jenetiki (Genetic Enhancement).
Aidha kitengo cha ukusanyaji na uhifadhi wa nasaba za mimea (Genebank) kilichopo TPRI hadi sasa kimekusanya jumla ya mimea 4,600 tu wakati Kenya imekusanya jumla ya mimea 40,000.
Tatizo la kusuasua kwa TPRI kunachangiwa na ukosefu wa raslimali muhimu za utafiti, hasa watafiti wanaojituma na wenye elimu, maarifa na uzoefu wa kisasa; maabara na vifaa vya utafiti vya kisasa; na fedha za kununulia nyenzo na vitendea vya kufanyia utafiti.
Bajeti ya nchi yetu bado inategemea wafadhili na wahisani. Kwa hiyo ni vyema watafiti wetu wakajituma ipasavyo kwa njia mbalimbali hata kwa kuandika tungo (proposals) ili kupata fedha za kufanyia kazi ya utafiti.
Taasisi za nchi nyingine za utafiti kwenye maeneo muhimu ya nchi zinafadhiliwa na serikali.
Kwenye maeneo mengine watafiti wanaandika tungo za miradi na kuzituma kwa serikali, na washiriki wa utafiti ndani na nje, na wanapata fedha za kufanyia kazi.
Tafiti utakaofanywa utaleta matokeo muhimu yenye manufaa kwa jamii na uchumi wa nchi au maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kwa kuzingatia utandawazi na ushindani mkali uliopo sasa duniani, taasisi kama TPRI inahitaji kufanya kazi kwa niaba ya wadau wa utafiti wa nchini na duniani.
Kila mtafiti lazima awajibike katika eneo lake analofanyia kazi. Wataalamu wake wanapaswa kutoa ushauri na utaalamu kwa nchi nyingine, kama TPRI ilivyokuwa huko nyuma, mfano kwenye karantini ya mimea, uchunguzi na ufuatiliaji wa maeneo wadudu waharibifu wanapozaliana na kusambaa, na ushauri wa njia za kuwadhibiti.
Wataalamu lazima waanze kufanya kazi, kupata matokeo yanayohitajika na taifa, na wawasilishe ripoti ya kazi wanazozifanya kwa wadau na washiriki wa utafiti, na kuyachapisha kwenye majarida ya sayansi yanayojulikana.
Taasisi nzima ina wafanyakazi 288. ambapo wenye kiwango cha stashahada (diploma) ni asilimia 10, Shahada asilimia 8, Shahada ya uzamili (Masters) asilimia 9, na wenye taaluma ya falsafa (PhD) ni asilimia 3.
Desemba mwaka jana, Dk. Deodorus Bubelwa Kamala, Naibu Waziri Wizara ya Afrika Mashariki alifanya ziara TPRI kujionea hali ilivyo na kutathimini mahitaji ya miundombinu na vitendea kazi utafiti na aliahidi kuwa serikali itaisadia TPRI ili ijiandae kikamilifu kabla ya kuingia kwenye Shirikisho la Muungano wa Afrika ya Mashariki.
Ni mategemeo kuwa ahadi hizi zitatiliwa maanani na kutekelezwa ipasavyo ili kuinusuru TPRI na kuiendeleza ili itekeleze majukumu na malengo yake iliyojiwekea kwenye Mpango Mkakati kwa Miaka 2005-2015.
|