|
Kweli Spika, maisha bora bila maji ni bure
2006-07-24 09:47:49
Na Mhariri
Mwishoni mwa wiki, Spika wa Bunge Bw. Samwel Sitta alifungua semina ya wabunge kuhusu Programu ya Kitaifa Kuhusu Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini.
Katika semina hiyo iliyofanyika Dodoma, Spika alisema utekelezaji wa ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania inapaswa kuzingatia upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Alisema upatikanaji wa maji safi na salama unapaswa kukidhi matumizi ya maji majumbani na katika shughuli mbalimbali za kiuchumi hapa nchini.
Sisi tunapenda kumuunga mkono Spika kwa kauli hii ambayo ameitoa wakati muafaka kabisa ambapo Serikali ya Awamu ya Nne ipo katika mikakati ya kutekeleza ahadi yake kuu, ambayo ni kumwezesha kila Mtanzania kuishi katika maisha bora.
Umuhimu wa maji kwa maisha ya binadamu hauna haja ya kuelezewa. Maji yana umuhimu mkubwa kwa uhai na maisha ya binadamu.
Lakini inasikitisha sana kuona kwamba maji bado ni tatizo kubwa kwa asilimia kubwa ya Watanzania, wote vijijini na mijini. Bado kuna Watanzania wengi sana hawapati maji, achilia mbali maji salama.
Tunakabiliwa na tatizo hili la maji huku tukiwa na hazina kubwa ya maji kila kona ya nchi. Tanzania inaweza si tu kutosheleza wananchi wake mahitaji ya maji, bali inaweza pia kuuza bidhaa hiyo nje!
Mungu ameibariki nchi hii kwa kuipatia mito mingi, maziwa mengi na bahari. Mito ni kama Rufiji, Kagera, Ruvuma, Pangani, Wami, Malagarasi, Mara, Kilombero, Ruaha kwa kuitaja michache tu. Tena hii ni ile midogo, kwani midogo ya misimu haina idadi.
Maziwa ni kama Victoria, Rukwa, Manyara, Tanganyika na mengineyo huku pia nchi yetu ikiwa imepakana na Bahari ya Hindi, moja ya bahari kubwa kabisa duniani.
Lakini pamoja na hazina zote hizi, kwa nini Mtanzania apoteze muda mwingi kuhangaikia maji?
Ndiyo maana tunaungana na kauli ya Spika, kwamba sasa ni wakati wa kuondokana na tatizo hili bandia la maji ambalo hatustahili kuwa nalo.
Huu ni wakati wa kuanza kwa dhati kutumia vyanzo vyetu vya maji ili kusambaza maji kila kijiji, kila mji, kila nyumba na kila kiwanda.
Ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania ianze kutekelezwa katika suala la maji, kwani tunaamini kwa kuanzia kwenye maji, huduma nyingine itakuwa rahisi kuzipata.
|