|
Polisi walimuua OCD kwa bahati mbaya
2006-07-23 11:07:10
Na Jackson Kimambo, PST, Arusha
Wakili Bw. Midium Mwale, anayewatetea washtakiwa wawili wanaokabiliwa na shtaka la mauaji ya Kamanda wa Polisi wa wilaya ya Ngorororo mkoani Arusha, SSP, I.A Kongoa, amedai kuwa polisi ndio waliomuua mkuu wao kwa bahati mbaya.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Ropene Oletira (35), mkazi wa Loliondo na Adan Nuru (44), Mkazi wa Namanga, wanaodaiwa kufanya mauaji hayo Julai 29, 1998 wakati wa msako wa majambazi.
Wakili huyo litoa madai hayo juzi mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha, Bi. Razia Sheikh, anayesikiliza kesi hiyo na kuongeza kuwa askari waliokwenda kusaka majambazi katika misitu ya kijiji cha Soi Tsambu, wilayani humo ndio waliomuua mkubwa wao.
Bw. Mwale alisema hayo wakati akimhoji shahidi wa Jamhuri PC E.5800 Mtajuka ambapo pamoja na mambo mengine alidai mbele ya mahakama hiyo kuwa askari walimuua mkubwa wao wakati wakirushiana risasi lakini sasa wanawasingizia kesi hiyo wateja wake waliokaa rumande kwa zaidi ya miaka tisa sasa.
Hata hivyo, shahidi huyo huku akiongozwa na wakili wa serikali Bw. Hashim Ngole, alikana madai hayo.
Akielezea tukio hilo, shahidi huyo alidai kuwa Julai 29, 1998 alikuja Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho na kutoa taarifa za kuwapo kwa majambazi wa Kisomali katika maeneo ya mlimani hivyo anaomba yakakamatwe.
Alidai kuwa taarifa hizo zilisambaa hadi kwa wakubwa zake na siku ya Julai 30, mwaka huo akiwa katika kituo kidogo cha polisi cha Soi Sambu, alikuja OCD na kuwataka kufanya msako mkali wa majambazi hayo ya kisomali.
Alidai baada ya taarifa hizo walianza safari ya kuelekea sehemu ambayo waliambiwa walipo majambazi na kuwa wakati huo mshitakiwa wa kwanza alishakamatwa baada ya msako katika kijiji cha Soi Sambu.
Alidai kuwa walipofika kwenye eneo waliloambiwa na mshitakiwa huyo kwenye msitu mkubwa na kuingia ndani, baada ya muda walianza kusikia sauti za watu wakinongona.
Tulijipanga katika eneo la tukio na muda mfupi tulisikia mlio wa risasi iliyotoka kwa OCD, kuashiria kuanza kushambulia na baada ya muda zilipigwa risasi za mfululizo sehemu walipokuwa majambazi.
Alidai kuwa baada ya muda walisikia OCD akiita, njooni mimi nimeshapigwa risasi ya kiuno na baada ya muda kidogo kupita hakusikika tena.
Alidai kuwa baadaye walianza kuishiwa nguvu kutokana na kupungua kwa risasi na kuamua kukimbia kila mtu na njia yake na kukutana chini ya milima ambapo kuna shule.
Alidai kuwa wakati huo hawakuwa na OCD kwa kuwa katika eneo la mapambano alikaa kimya kwa muda mrefu wakatambua alishakufa na siku ya pili yake walienda kuchukua mwili wa marehemu akiwa hana silaha yake aina ya SMG aliyokuwa nayo.
Hata hivyo, alidai kuwa hawakukuta mtu mwingine akiyekufa katika eneo la mapambano.
Yafuatayo ni mahojiano kati ya Bw. Mwale na shahidi huyo PC Mtajuka ambaye ni askari polisi.
Mwale: Waliomuuwa OCD walikuwa ni askari wenzake kwa bahati mbaya.
PC: Hapana si askari.
Mwale: Mshitakiwa wa kwanza alikuwa na silaha gani
PC: Hakuwa na silaha na kuwa siku ya tukio hilo Julai 30,1998 alikuwa chini ya ulinzi akienda kuwaonyesha mahali majamazi wa kisomali walipo katika msitu huo.
Mwale: Kuna wakati wowote mshitakiwa huyo ulimwona akimfyatulia risasi OCD.
PC: Hapana sikumwona.
Mwale: zile risasi zilizokuwa zikirushwa ukikuwa ukiziona kwa macho yako.
PC: Hapana huwezi ukiona.
Mwale: Baada ya kuishiwa nguvu katika eneo la mapamabo ilikuwaje.
PC: Mtajuka Kila mmoja aliondoka kivyake.
Mwale: Je wakati mnaondoka mliweza kutambuana yule ni fulani na yule ni fulani.
PC: Kwa kuwa ilikuwa ni mapambano hatari niliondoka kivyangu.
Mwale:Katika jeshi la polisi askari akizidiwa nguvu akakimbia kusalimisha maisha yake ni kosa la kinidhamu.
PC: Hapana
Mwale:Kwa mshitakiwa wa kwanza kukimbia kusalimisha maisha yake kuna ubaya wowote.
PC: Hakuna ubaya.
Mwale:Kuna kosa lolote la kijinai kwa mshitakiwa huyo kukimbia kama nyie mliweza kukimbia kusalimisha maisha yenu.
PC: Hapana
Mwale:Wewe umekuja kufanya nini mahakamani
PC: Kutoa ushahidi
Mwale:Ushahidi gani?
PC: Kuhusu mauaji ya marehemu.
Mwale:Unamfahamu aliyemuuwa marehemu
PC: Majambazi
Mwale:Majambazi uliyaona.
PC:Mtajuka Hapana niliwasikia.
Mwale:Mlimwuliza mshitakiwa wa kwanza uhusiano wake na majambazi hayo .
PC: Alidai kuwa yeye walimteka.
Mwale:Je mlimuuliza kutekwa kwake.
PC: Ndio kwa maana pale alidai ametumwa kutafuta taarifa information awapelekee.
Mwale:Wewe ndio uliompora shitakiwa wa kwanza shilingi 10,000 na kununua bia mbili na kuzinywa na kisha kwenda kwenye eneo la tukio.
PC: Hapana
Mwale:Unakumbuka mtuhumiwa wa kwanza alikamatwa lini.
PC: 31Julai asubuhi kabla ya kwenda kwenye eneo la tukio kwenye mashambulizi.
Mwale: Katika kumhoji aliwaeleza nini.
PC: Alidai alikuwa na majambazi wenye silaha na alikuwa amewaacha hapo juu ya mlima.
Mwale:Mlichukua hatua gani.
PC: Tulimchukua na kumfunga kamba hadi kituo cha ororosokwani na kumhoji.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kesho.
|