|
Mwakilishi asifu viongozi wakuu Muungano
2006-07-23 11:04:56
Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar
Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar amesifu hatua ya viongozi wakuu wa Serikali ya Muungano na Zanzibar kukutana na kuanza kutatua kero za Muungano kuwa ni hatua kubwa ambayo haijawahi kufanyika siku za nyuma.
Mwakilishi wa kuteuliwa, Bw. Ali Mzee Ali, alisema hayo wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Kiongozi katika mwaka wa fedha 2006/07, katika kikao cha baraza kinachoendelea mjini hapa.
Aidha, aliwaomba wajumbe wa Baraza hilo kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika kutatua kero za Muungano.
Alisema kwamba hatua ya watendaji wakuu wa Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar kukutana kuanza kutatua kero za Muungano ni hatua kubwa na haijawahi kufanyika na viongozi wa Bara na Zanzibar katika siku za nyuma.
Alisema kwamba kitendo cha Waziri Kiongozi, Bw. Shamsi Vuai Nahodha, kukutana na Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa na watendaji wao kujadili kero hizo kitasaidia kuondoa malalamiko yanayojitokeza baina ya pande mbili hizo.
Hatua ya mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa kasoro za Muungano iliyofikiwa inastahili kupongezwa na kuungwa mkono na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, alisema Mwakilishi huyo.
Alisema kwamba ni vyema wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM na CUF wakatumia mjadala wa bajeti unaoendelea kuchangia utatuzi wa kero hizo ili michango yao iweze kuleta faida katika mazungumzo hayo.
Hata hivyo, alisema kwamba ni vyema Mamlaka ya uvuvi wa bahari kuu itakayoanzishwa makao makuu yake yakawa Zanzibar na iwe na sura ya Muungano kwa watendaji wake.
Alisema kwamba iwapo Zanzibar itapata asilimia 40 ya mapato ya uvuvi wa Bahari Kuu kama ilivyokubaliwa katika kikao cha pamoja itaweza kuinua mapato yake na kuimarisha sekta ya uvuvi.
Waziri Kiongozi nakupa hongera sana wewe na wenzako katika hatua mnazochukua kutafuta ufumbuzi wa kero za muungano na sisi tupo nyuma yako, alisema Mzee.
Alisema kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta faida kubwa za kisiasa na kiuchumi na Wazanzibari walio wengi hawako tayari kuona muungano huo ukivunjika.
Muungano huu tunauchangia na tunaukubali, lakini hatuko tayari kuuona unabomoka, hilo haliwezekani, alionya Mwakilishi Ali Mzee.
Alisema hali ya kisiasa Zanzibar ni shwari ikilinganishwa na miaka ya nyuma tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Wakichangia bajeti hiyo wajumbe wa kambi ya Upinzani CUF waliema kwamba haikuwa muafaka kwa Waziri Kiongozi Bw, Shamsi Vuai Nahodha kuwawakilisha Wazanzibar katika utatuzi wa kero za Muungano bila ya kupata baraka ya wananchi wenyewe.
Walieleza hatua hiyo kuwa ni sawa na suala la kifamilia kuzungumzia na kutolewa ufumbuzi na mtu mmoja na kushauri serikali ichukue maoni ya wananchi katika ufumbuzi wa kero za muungano.
|