|
Wamarekani Wenye asili ya Afrika msiwe na wasiwasi na bara la Afrika
2006-07-23 11:03:10
Na Maura Mwingira, Abuja
Rais Jakaya Kikwete amewataka Wamarekani wenye asili ya Afrika, kutokuwa na mashaka na wasiwasi kuhusu Bara la Afrika, kwa kuwa lipo katika mwelekeo mzuri kisiasa na kiuchumi.
Aliyasema hayo jana wakati wa kikao cha viongozi wakuu wa nchi na serikali, waliokuwa wakihudhuria mkutano wa saba wa Leon Sullivan, uliomalizika jana hapa Abuja Nigeria.
Alisema kuwa ingawa ni kweli kuwa Afrika inakabiliwa na matatizo ya hapa na pale, lakini ni bara lililo katika mwelekeo sahihi wa kimaendeleo.
Msiwe na wasiwasi juu yetu, Afrika iko katika mwelekeo mzuri, mkutano huu wa saba na mingine iliyopita Afrika imeonyesha utayari na imani kwa dada na kaka zao walio nje ya bara hili, alisema Rais katika mkutano ambao pia ulihudhuriwa na wajumbe wa mkutano wa saba wa Sullivan.
Katika kusisitiza kuwa Afrika iko katika mwelekeo sahihi, Rais alisema kuwa, Afrika sasa kupitia Umoja wa Afrika (AU)haivumilii wala kuzipokea serikali ambazo kuwapo kwake madarakani kunatokana na mapinduzi ya kijeshi.
Tunapambana na rushwa kwa nguvu kubwa, wala hatujitetei katika hilo, tunaimarisha taasisi za Kikanda. Na Umoja wa Afrika una nguvu kubwa. NEPAD inaendelea kustawi na tunao mchakato wa kujitathmini wenyewe, alisema Rais.
Katika hotuba yake iliyoelekea kuwagusa wajumbe waliokuwa wakimsikiliza na ikionyesha utofauti mkubwa na viongozi wengine waliomtangulia kuzungumza, Rais alisema kuwa viongozi wa Afrika wamejiwekea utaratibu wa kutatua migogoro inayojitokeza katika nchi zao.
Alibainisha kuwa mitaji na uwekezaji unaongezeka, kasi ya wafanyabiashara wa kati inaongezeka, uchumi unakua na mwelekeo wa Afrika katika siku zijazo ni mzuri.
Kuna habari nyingi na nzuri zinazolihusu Bara la Afrika na ambazo zinatakiwa kutangazwa na kusikika, tunawajibika kuzisambaza habari hizo kama vile tunavyowajibika wakati picha mbaya zinazohusu vita na machafuko kama vile Somalia, ukame au zinazohusu ugumu wa maisha katika makambi ya wakimbizi, zinavyotoa picha mbaya kwa Mama yetu Afrika,alisisitiza.
Rais Kikwete ambaye alikuwa miongoni mwa marais waliohudhuria mkutano huo uliowashirikisha wajumbe kutoka nchi 44, alisema kuwa mkutano huo umetoa fursa nzuri kwani viongozi hao na washiriki wa mkutano huo wameweza kujadiliana na kubadilishana mawazo katika mambo yanayohusu afya, elimu, miundombinu na uwekezaji.
Alibainisha kuwa kwa Mama Afrika, changamoto kubwa wakati wote imekuwa ni raslimali, teknolojia, na fedha kwa ajili ya maendeleo ya kijamii, uchumi, kushawishi na kukuza ujasiliamali na kujenga taasisi za utawala zinazolenga katika kuwatumikia wananchi vizuri.
Naye Rais Paul Kagame wa Rwanda, alisema mchakato unaofanywa na Taasisi ya Leon Sullivan ya kujenga daraja linalowaunganisha Waafrika na wenzao Wamarekani wenye asili ya Afrika, ni kielelezo cha uletaji wa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kwa Afrika.
Alisema sekta za umma na binafsi lazima zijenge ushirikiano utaoweka misingi ya majadiliano kati ya Waafrika na wawekezaji wa kimataifa.
Alisisitiza kuwa kinachotakiwa si kujadiliana matatizo ya Afrika, kwani kila mmoja wao anayafahamu.
Kinachotakiwa ni kutafuta njia za utekelezaji wa malengo yao.
Lazima tuwe Waafrika wenye fikra na mitazamo mipya ili kwayo tuweze kunufaika na ushirikiano, alisema.
|