|
Mwanamke auawa kwa kubakwa na makuli
2006-07-23 11:02:04
Na Frank Mbunda
Mwanamke mmoja mfanyabiashara wa nyanya na vitunguu, mkazi wa wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, ameuawa baada ya kubakwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni makuli wanaobeba mizigo katika mji mdogo wa Ilula, wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi Advocate Nyombi, alisema hayo alipozungumza na Nipashe kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio.
Kamanda Nyombi alimtaja mtu aliyeuawa kuwa ni Joyce Msamila (35), aliyekuwa akifanya biashara kati ya Ilula na Dar es Salaam.
Watu watano tayari wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo.
Kamanda Nyombi alisema marehemu alikumbwa na maafa hayo baada ya kukaa kwa muda mrefu akitafuta usafiri wa kumrejesha Dar es Salaam akiwa na matenga 15 ya nyanya.
Aliongeza kwamba akiwa katika eneo hilo, mama huyo alikuwa na vijana watano ambao ni wabeba mizigo wanaosadikiwa kuhusika na mauaji hayo.
Alisema baada ya kuichunguza maiti ya marehemu, polisi ilibaini kwamba mama huyo alikuwa amebakwa na watu alikuwa nao katika kituo hicho cha usafiri.
Aidha, alisema wanaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini kama kuna watu wengine waliohusika na kifo cha mama huyo.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja majina ya watu waliokamatwa wakituhumiwa mauaji hayo, kwa vile upelelezi ulikuwa unaendela.
Kamanda Nyombi alisema jeshi la polisi lilipokea taarifa hiyo kwa uzito unaostahili na kuamua kulifanyia kazi haraka, ikizingatiwa kwamba tayari kuna mtu aliyetendewa unyama na kupoteza maisha, hali iliyosababisha hofu katika jamii ya watu.
Wakati huo huo, kuna taarifa kwamba mwanafunzi mmoja katika mji wa Ilula, ameuawa na watu wasiojulikana na kunyofolewa viungo vyake vya mwili sehemu za siri, maini na figo.
Habari kutoka kwa watu walioshuhudia mwili huo, zilidai kuwa watu wasiojulikana wameanzisha vitendo hivyo vya kuvizia na kuua watu na baadaye kukata viungo.
Baadhi ya watu waliozungumza na Nipashe kutoka Ilula, walisema wananchi wameingiwa na hofu kufuatia matukio hayo mawili yaliyotokea wiki hii.
Mwenyekiti wa umoja wa wakulima wa nyanya na vitunguu katika jiji huo, Bw. Yohanes Muhanga, aliiambia Nipashe kwamba matukio hayo yameutia doa mji huo wa kibiashara.
Kwa kweli watu hapa wameingiwa na mashaka makubwa, kufuatia mauaji haya ya watu, kwanza kimetokea kifo cha mwanafunzi wa shule, na sasa jana (juzi) ameuawa mfanyabiashara, alisema Bw. Muhanga.
Hata hivyo, kamanda Nyombi hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo na kuomba apewe muda ili aweze kutafuta taarifa kamili.
Ni kweli kuna mtoto aliuawa mwanzoni mwa wiki hii, lakini kwa hapa nilipo sina jina lake, ila nimeagiza kufanyika kwa msako mkali kwa ajili ya matukio hayo mawili ya mauaji, alisema Kamanda Nyombi.
|