|
Moto wateketeza bweni, wanafunzi watano walazwa
2006-07-23 11:01:08
Na Thobias Mwanakatwe, PST, Korogwe
Moto mkubwa umeteketeza bweni moja la Shule ya Sekondari ya wasichana ya Mkalamo wilayani Korogwe na kuunguza mali za wanafunzi.
Kufuatia moto huo, wanafunzi watano wamelazwa katika zahanati ya kijiji cha Kwalukonge baada ya kupata mshituko.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Bw. Issaya Mngulu, alisema moto huo ulitokea Julai 20, asubuhi. Hata hivyo, chanzo chake hakijafamika. Pia alisema thamani ya vifaa vilivyoteketezwa haijafahamika.
Chumba hicho wanacholala wanafunzi sita kiliungua moto kilikuwa kimefungwa wakati wanafunzi hao wakiwa madarasani.
Kamanda Mgulu alisema wanafunzi hao walipojulishwa kuhusu moto huo, watano walianguka ghafla kwa mshitukio na kukimbizwa katika zahanati hiyo.
Wanafunzi hao ni Saumu Rashid (19), Hadija Kijavala (17), Asha Ramadhani (19) Zainab Muhidin (18) na Neema Eliasi (16).
Baadhi ya vitu vilivyoteketea ni vitanda na kwamba uchunguzi wa awali uliofanywa na polisi unaonyesha kuwa huenda chanzo cha moto huo kimetokana na wanafunzi kuacha mshumaa au ubani ukiendelea kuwaka walipokwenda madarasani.
Tunahisi kwamba huenda chanzo cha moto huo kinatokana na mshumaa uliachwa ukiwaka au ubani kwani hosteli hiyo haina umeme bali wanafunzi wanatumia kandiri ambayo tumeikuta pembeni haina hata mafutaalisema Bw. Mngulu.
Kamanda huyo wa polisi alisema polisi bado wanaendelea na uchunguzi zaidi kubani chanzo cha kuzuka kwa moto huo na alishauri wanafunzi ambao shule zao hazina umeme kuhakikisha wanazima mishumaa, kandiri na udi wanapokwenda madarasani.
|