23 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kubadili majengo ya sekondari kuwa vyuo tunarejea wapi?
 
2006-07-23 10:46:11
Na Mhariri

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Bw.Omar Kwaangw’ ameishauri serikali isikubali kubadili shule za sekondari kuwa vyuo kwa sababu hatua hiyo itasababisha kupunguza nafasi kwa elimu ya sekondari nchini.

Bw. Kwaangw’ alitoa ushauri huo bungeni juzi kwenye taarifa ya maoni katika kuchangia hotuba ya bajeti ya makadirio na matumizi ya Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2006/2007.

Katika taarifa hiyo, Bw. Kwaangw’alisema kumekuwepo na mtindo wa kuanzisha vyuo vya elimu ya juu kwa kutumia majengo ambayo yametumika kwa muda mrefu kutoa elimu ya sekondari. Mfano majengo ya sekondari Magamba iliyoko Tanga na Mazengo ya Dodoma.

Mwenyekiti huyu, hakika amefumbua kitendawili ambacho wamekuwa wakijiuliza katika miaka ya hivi karibuni ambapo majengo yaliyokuwa yakitumika kama sekondari sasa yamebadilishwa na kuwa vyuo.

Tunaungana kwa asilimia mia na Bw. Kwaangw’ kwamba hatua hiyo siyo sahihi hasa katika wakati huu ambapo mahitaji ya elimu ni makubwa ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kuongeza idadi ya wasomi wetu, msingi ukianzia shule za msingi.

Hatua hiyo pamoja na kuonekana ni ya manufaa kwa upande mmoja, lakini kwa upande mwingine inapunguza idadi ya shule za sekondari ambazo tayari hazitoshi kuwabeba wanafunzi wanaomaliza shule za msingi.

Hali halisi serikali imeona hasa katika kipindi cha miaka miwili ya karibuni ambapo idadi kubwa ya wanafunzi japokuwa walifaulu kuingia kidato cha kwanza, lakini hawakupatiwa nafasi.

Matokeo yake Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa akaingilia kati na kuagiza shule mpya zijengwe haraka kuwapokea wanafunzi hao.

Tunafurahi bw. Kwaangw’ ameliona hilo na kuliweka hadharani kwani tunaamini pia kama ushauri huo utazingatiwa, basi hata shule nyingi za msingi ambazo nazo zimeanza kugeuzwa kuwa sekondari, mfano baadhi katika Jiji la Dar es Salaam hazitaguswa.

Kilichopo, ni kwa serikali kuendelea kuhimiza taasisi zisizo za kiserikali, mashirika ya dini na hata watu binafsi kuchangia katika kujenga vyuo badala ya kuruhusu majengo yaliyokuwa kwa matumizi mengine hasa ya shule kugeuzwa vyuo. Hakika vyuo tunavitaka. Lakini uandaliwe utaratibu ambao kiutekelezaji hautaathiri upande mwingine.

Kama alivyosema Bw. Kwaangw’ hatua ya kubadili majengo yaliyojengwa zamani kwa madhumini tofauti, kunahitaji gharama kubwa, hivyo ni vema kwa watu na taasisi zenye nia ya kuwekeza katika elimu ya juu, wajenge vyuo vikuu vipya na serikali iwawezeshe kupata maeneo ya kutosha.

Bila shaka wahusika wamesikia na wataufanyia kazi ushauri huo ili tusonge mbele na siyo turudi tulikotoka.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.