|
Mke na mume wote wana nyumba ndogo nje!
2006-07-23 10:44:15
Na Flora Wingia
Famili ni baba, mama na watoto. Kwanza inaanza ikiwa na baba na mama, kisha anazaliwa mtoto au watoto.
Vipo vitu kadhaa vinavyosababisha familia kutengana, kumeguka na hata kusambaratika kabisa. Kwa mfano kifo, uhamisho, fumanizi na hata mahangaiko ya kimaisha kutafuta riziki.
Topiki ya leo itajikita katika hilo la mwisho la mtu kuiacha familia yake na kwenda eneo lingine iwe ndani au nje ya nchi kuhangaikia pato la familia.
Yapo mambo mengi yanayojitokeza ila nitajaribu kudokeza machache.
Kipo kituko kimoja cha jamaa yangu ambacho nimeona nikiweke hadharani kuonyesha Maisha Yalivyo katika baadhi ya familia zetu. Ni kichekesho kwa jinsi mazingira yake yalivyo.
Naam. Yupo jamaa yangu ambaye hivi karibuni ametuacha midomo wazi kwa mshangao baada ya kuja na mke mwingine huko alikoenda kuhangaika kikazi na kumtambulisha bi-mkubwa.
Jamaa huyu ni Mkristo. Bi-mkubwa naye kuona mambo ndio hivyo, naye akampasulia kwamba anaye njemba wake hivyo ngoma ni droo.
Kwa kifupi ni kwamba jamaa yetu huyu alikwenda mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuhangaikia maisha. Huku nyuma, Jijini Dar es Salaam aliacha mke na mtoto(hawana ndoa) lakini ndiye mkewe.
Alimpangishia chumba mke huyu na amekuwa akituma fedha za matumizi pamoja na pango kwa muda wote takribani miaka miwli. Naye alikuwa akija kuona familia yake mara mbili kwa mwaka.
Kumbe jamaa huyu huko Kusini alimpata mwanamama mmoja waliyeshibana hata kujitambulisha kwa wazazi wake.
Na hii ni baada ya kupata ujauzito hatimaye kujifungua mtoto wa kiume. Wazazi wa bibie wakachachamaa lakini baadaye wakatulia, wakawapa chumba cha kuishi katika nyumba yao.
Jamaa yangu huyu kabla alishamjulisha bibie kuwa ana mke na mtoto, jambo ambalo hakuonyesha kujali kwa kuwa anampenda.
Kivumbi ni hivi karibuni jamaa alitaka kuja nyumbani lakini bibie akangangania sharti waende wote akamuone na mke mwenzake.
Jamaa akaweka utaratibu wakaja wote hadi kwa bi-mkubwa. Katika utambulisho, jamaa akababaika na kuongopa eti ni mfanyakazi mwenzake.
Bi-mdogo kusikia vile akachachamaa, mwambie ukweli mimi ni mke kama yeye...unamficha nini...tutabanana humu humu ndani.
Bi-mkubwa naye hakukaa kimya, hata kama ni mke mwenzangu, humu ndani kwangu hakai, ondoka naye. Baada ya malumbano ya muda jamaa aliondoka na bi-mdogo wake.
Lakini aliporejea usiku ikabidi ambane bi-mkubwa kuhusu habari alizopewa na wadaku kwamba ana jibaba, mume wa mtu anayetesa naye tena anamjengea nyumba.
Bila ajizi na jinsi alivyojisikia vibaya kutambulishwa mke mwenza, ghafla naye akakubali. Ndiyo ninaye wangu wa kuniliwaza...unapotelea huko muda mrefu unafikiri nitafanya nini...yawe na yatakayokuwa. Mzozo karibu usiku mzima.
Jamaa alipobaini ukweli kwamba mkewe naye ana mchuchu wake, akafunga safari kurejea kazini kwake.
Kufika huko akanitumia(mimi) ujumbe wa simu uliosomeka hivi, mama...kanitumia ujumbe akiniambia nimsahau kwa yote...hata mtoto ni zawadi yangu.
Sawa kabisa, nikirudi huko nitamshughulikia... atatimka tu simhitaji, unamalizia ujumbe wa jamaa yangu huyo.
Mpenzi msomaji, hayo ndiyo mambo yanayotokana na familia iliyogawanyika kutokana na kuhangaikia maisha. Kwa ujumla nimejaribu kutafakari familia hii ya jamaa yangu nikagundua yafuatayo.
Bi-mkubwa ambaye mumewe alimwacha ndani akiwa hana kazi, baada ya mume kukaa muda mrefu bila kuja nyumbani, aliamua kutafuta kazi ambayo alipata.
Hata fedha za matumizi zikichelewa, angalao pato la kazi ile lilimsaidia.
Na inawezekana katika mizunguko yake ndipo akakutana na mshikaji wa kujiliwaza ambaye ni mume wa mtu.
Kwa ujumla alishindwa kujizuia hasa baada ya mume kujichimbia huko Kusini. Kumbe mume naye huko nako akaona kukaa mpweke hawezi na pia kulambalamba vidosho wa mitaani hakuna maana.
Akaamua kumnasa wake ambaye ndiye huyo aliyemleta kumtambulisha.
Sababu za maamuzi ya bi-mkubwa na mumewe, hakika zinafanana.
Kila mmoja alipata wa kumfariji. Lakini ugumu unakuja wakati kila mmoja akimtambulisha mwenzake.
Nilipomhoji jamaa yangu kwanini aliamua kumleta bi-mdogo kumtambulisha bila woga, alijibu, mbona najua muda mrefu ana bwana? Hata nilipombana hivi majuzi alikubali. Kwa hiyo ngoma hii ni droo (nguvu sawa).
Familia hii ambayo iko ukingoni kumeguka, inaonekana kila mmoja ameridhika na kule alikoegemea.
Swali hapo ni je, awali walipendana kwa dhati au ilikuwa ni fix tu? Kama jibu ni ndiyo mbona kila mmoja anafurahia egemeo jipya?
Wasalaam
E-mail:fwingia@guardian.co.tz
|