|
Mazingira magumu yachangia watoto kuambukizwa Ukimwi
2006-07-21 09:37:51
Na Sifa Sebastian
Watoto wanaoishi katika mazingira magumu wana uwezekanoi kubwa ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kutokana na hali ya maisha wanayoishi.Hii inatokana na uwezekano wao wa kujiingiza kwenye ngono na madawa ya kulevya. Mwandishi Sifa Sebastian inaelezea.
Takwimu zaoyesha kuwa Tanzania ina watoto yatima wapatao milioni 2.5. Ukimwi umekuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la watoto yatima.
Kuna aina mbili za watoto yatima. Wale ambao wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili kutokana na ugonjwa wa Ukimwi na kuna ambao wamezaliwa wakiwa na virusi vya Ukimwi.
Mtoto anayelelewa na mzazi mmoja mara nyingi hujikuta katika wakati mgumu, hasa pale mzazi wake anaposhindwa kumpatia mahitaji muhimu ya kila siku kama vile chakula.
Hali hiyo, humsababishia mtoto kujikuta akiishi katika mazingira magumu huku baadhi yao wakijikuta wanaingia mtaani kujitafutia chochote.
Mwangaza (si jina halisi), ni binti mwenye umri wa miaka 14. Alijikuta akianza kufanya biashara ya ukahaba kutokana na hali halisi ya nyumbani kwao baada ya mamaye kuugua Ukimwi.
Tumeuza vitu karibu vyote humu ndani lakini ndiyo hivyo tena mama siku zote ni mtu wa kuumwa tu, unapomuona pale alipolala ni wa kumlisha na kumbadilisha nguoanasema Mwangaza.
Baba yao aliondoka nyumbani na hajarudi tangu mama yake aannze kuugua.
Nasikia siku hizi kuna mwanamke mwingine anaishi naye, kuna watu walimuona ndiyo wakaja kutuambia, sina hata muda wa kumfuatilia.
Mwanaume huyo anajua kuwa mkewe huyo wa kwanza anaumwa Ukimwi.
Sina kazi yoyote ya kuniingizia kipato, na siku hizi hata shuleni siendi kwa ajili ya kumuuguza mama.Kuna kilabu cha pombe hapo nyuma ya nyumba yetu, jioni huenda kumsaidia mama mwenye kilabu kuuza pombe.
Hunipa chochote wakati mwingine ukipata mwanaume anaweza kukupa Sh. 2,000 au Sh. 3,000, tunatumia. anasema Mwangaza.
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Bi. Louise Setshwaelo anasema kuwa kuna watoto milioni 15 duniani kote wanaoishi katika mazingira magumu yanayotokana na ukosefu wa huduma mbalimbali ikiwemo chakula.
Anasema kuwa, asilimia tisa ya watoto wenye umri chini ya miaka 15 wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.
Kila mwaka Tanzania inawapoteza maelfu ya watanzania kutokana na kufa kwa ugonjwa wa Ukimwi.
Wazazi wengi ambao ndiyo walezi wa familia wamekuwa wakifa kutokana na Ukimwi na wakati mwingine hulazimika kuuza mali zao ili kujipatia fedha za matibabu hali inayofanya kuwaacha watoto bila urithi wowote.
Kutokana na vifo hivyo watoto wengi wamekuwa wakiachwa bila ya kuwa na msaada wowote na hapo hujikuta wakijiingiza kwenye vitendo hatari.
Matatizo yanayowakabili watoto yatima waliokuwa katika mazingira magumu ni pamoja na
Kukosa chakula.
Pale mzazi mmoja akiwa anaumwa na kukosa uwezo wa kufanya kazi yoyote kwa muda mrefu hata ile familia inayotegemea kilimo inaathirika na hasa watoto.
Watoto wengi waliofiwa na wazazi wao wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa waangalizi.
Wengi wa watoto wamekuwa wakiacha shule na kubaki nyumbani kuwauguza ndugu wanaougua magonjwa yanayotokana na Ukimwi.
Watoto wa kike ndiyo wanaonekana kuathirika zaidi kutokana na kujikuta katika majukumu makubwa ya kuuguza ndugu wagonjwa na kuwalea wale walioachwa.
Watoto wengi walio katika mazingira magumu wamejikuta wakilazimika kujiingiza kwenye ngono wakiwa na umri mdogo kwa kusukumwa na matatizo waliyonayo.
Wengine wamekuwa wakifanya hivyo kutokana na kukosa elimu ya afya na jinsi na wengine hufanya hivyo ili kujitafutia fedha za kujikimu na familia.
Kwenye miji mikubwa watoto wamekuwa wakitumiwa kwenye biashara ya ngono bila watoto hao kuelewa madhara yake na kujikuta wakipata Ukimwi wakiwa na umri mdogo.
Watoto wanaoishi katika mazingira magumu ni rahisi sana kwao pia kujiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya ambapo hupelekea kujiingiza katika ngono zisizo salama na kujikuta wakipata ugonjwa wa Ukimwi.
Mwanafunzi mmoja Elizabeth Mussa anasema ,Unapotumia bangi au madawa ya kulevya akili yako inakuwa si nzuri kwa hiyo unawaza kufanya mambo maovu tu.
Mbaya zaidi yatima wengi wamejikuta wakiishi katika mazingira magumu kutokana na kunyimwa urithi wa mali za wazazi wao baada ya kufariki.
Kutokana na watoto kuwa katika hali ngumu, wanakuwa katika hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na kukosa chakula na matibabu pale wanapokuwa wagonjwa na kuhitaji msaada wa haraka.
Kuna umuhimu kwa serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, Taasisi za dini, watu binafsi na vikundi mbalimbali vya kijamii kuhakikisha kuwa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya inawafikia walengwa ili kuchukua tahadhari ya kupambana na Ukimwi.
Elimu itawasaidia watu wengi kuweza kuepukana na janga hilo la Ukimwi.
Wananchi waelimishwe juu ya faida za kuandika mirathi mapema ili pindi watakapokufa watoto wao wawe na uhakika kupata mali hizo.
Pia kuna umuhimu kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na serikali kwa ujumla kuwa na utaratibu wa kutembelea vituo vinavyolea watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kuzungumza nao ili kuwasaidia jinsi ya kutatua matatizo yao ya kweli na kutatua.
Kuendelea kutoa misaada tu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu bila kujua sababu zilizofanya wawe pale haitasaidia kwani watoto wengine wametoka katika familia zenye wazazi wote wawili au mmoja.
Tukiweza kujua sababu ya kweli kwa watoto wanaokimbia kwao ambao wana familia pengine itasaidia kupata ufumbuzi wa kudumu wa kuwarudisha hao na wengine wasifanye tena hivyo.
|