|
TFF msibabaishe kutafuta vipaji vya vijana
2006-07-21 09:35:33
Na Mhariri
Timu ya Vijana ya Tanzania imepata nafasi ya kwenda Uingereza kufanya mazoezi kwa siku kadhaa na ikiwa huko itacheza mechi za kirafiki ili kuipima timu hiyo inayoundwa na vijana wenye umri chini ya miaka 20.
Ofa hiyo imetolewa na Kampuni ya Global Scouting Bureau, GSB, inayojishughulisha na uwakala wa soka chini ya rais wake Jack Pemba.
Kimsingi ziara hiyo ya Uingereza itawasaidia wachezaji wa timu hiyo kuitangaza Tanzania na kutangaza vipaji vyao, ambavyo huenda vikasaidia kuanzisha soko la wachezaji wa kulipwa kutoka Tanzania.
Ziara hiyo inaweza kuwafumbua macho mawakala wa Uingereza na barani Ulaya kujua kumbe Tanzania nayo imo katika soka, kitu ambacho kitasaidia kuintangaza vizuri nchi yetu.
Timu hiyo ya taifa inatarajia kuondoka nchini Agosti 12 kwenda Uingereza, huku Kampuni ya Global Scouting Bureau ikiwa tayari imeingia mkataba kwa ajili ya kuisafirisha timu hiyo na kuipatia mechi kadhaa za majaribio.
Ikiwa nchini Uingereza timu hiyo ya taifa ya vijana itaweza kucheza na timu mbili za huko, Chelsea na Watford.
Kwa kweli ziara hiyo sio ya kuifanyia mzaha kwani itawawezesha wachezaji wetu kuingia katika soka la kulipwa la kimataifa.
Pia ziara hiyo itamwezesha mchezaji kujua misingi sahihi ya soka la kimataifa, ili baada ya miaka mitatu ijayo Tanzania iweze kuwa na wachezaji kadhaa wanaocheza soka Ulaya au kwingineko.
fursa ya kucheza na timu hizo kutawapatia wachezaji wa timu ya vijana kupata somo kutoka kwa wataalam wa timu ya Chelsea na Watford mbali na mafunzo watakayoyapata kutoka kwa kocha Stuart John Hoe, mtaalam wa soka la vijana aliyeiibua nchi ya Trinidad & Tobago hadi kufika chati za juu za soka la kimataifa.
Pamoja na ofa hiyo hatuna uhakika kama kweli Shirikisho la Soka la Tanzania, TFF, limechukulia kwa umakini ofa hiyo, hasa suala la maandalizi ili kuweza kupata wachezaji wazuri watakaoweza kuuzika Ulaya.
Hatuna uhakika kama TFF inafuatilia kwa karibu mashindano yanayoendelea huko Arusha au yale ya vijana yaliyomalizika hivi karibuni mjini Moshi, ambayo yaliandaliwa na Taasisi ya EMIMA.
TFF inatakiwa kufanya ziara nchi nzima na hasa katika mashule ya soka na yale ya kawaida ili kupata wachezaji wenye vipaji vitakavyoiwezesha nchi yetu kujitangaza vizuri ili wachezaji waweze kupata soko nje ya nchi.
Tusitumie nafasi hii kwa kupeleka ndugu na jamaa bali itumike kikamilifu kuhakikisha kwamba wachezaji na shirikisho la soka nchini linanufaika katika kila hali kisoka.
Tunaamini kwamba Tanzania ina vijana wenye vipaji vya uhakika vitakavyowashawishi mawakala nje ya nchi kununua wachezaji.
|