19 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Simulizi za Mradi wa Mchuchuma zinachosha
 
2006-07-19 10:31:28
Na Mhariri

Mradi wa makaa ya mawe ya Mchuchuma sasa umekuwa kama hadithi isiyokuwa na mwisho. Kuna Watanzania wengi tu ambao walianza kuusikia mradi huu wakiwa wanafunzi wa shule ya msingi na sasa wamezeeka au kuwa na umri mkubwa, huku mradi huo ukiendelea kusimuliwa kama vile ni hadithi za mapokeo.

Miaka nenda rudi mradi umekuwa ukizungumziwa na kuundiwa mikakati karibu kila kikao cha bunge, lakini hakuna kinachofanyika.

Kelele nyingi kuliko vitendo zinazopigwa kuhusu mradi huu zinaweza kufanana na zile zilizokuwa zilizohusu ujenzi wa barabara ya Kiboto- Lindi iendayo mikoa ya Kusini toka Dar es Salaam.

Tunakumbuka wakati fulani kuna wabunge walidiriki kuangusha machozi kulilia ujenzi wa barabara hiyo ambayo sasa, baada ya vilio vya miaka mingi, imeanza ’’kujengwa kwa vitendo’’.

Mradi huu wa makaa ya mawe Mchuchuma ulipaswa kupewa kipaumbele cha juu kabisa ili nchi yetu iweze kukabiliana na tatizo la umeme linaloendelea kuwa sugu kadri miaka inavyosonga mbele.

Mpaka lini wabunge wataendelea kulia bungeni kuhusu mradi huu? Au ni mpaka pale nchi yetu itakapoingia gizani moja kwa moja kwa kukosa hata ule umeme wa mgawo? Au ni mpaka wabunge na wananchi watoe machozi ya damu?

Sasa tunapaswa kuacha masihara. Wahenga walisema maneno matupu hayavunji mfupa, na ndiyo maana leo nchi inaadhirika kwa kukosa umeme kutokana na uzembe wetu na hulka yetu ya kupanga mambo bila kuyatekeleza kwa vitendo.

Tunadiriki kusema kwamba hili tatizo kubwa la umeme tunalokumbana nalo hivi sasa ni adhabu tuliyopewa na Mungu kwa kushindwa au kuzembea kutekeleza mradi huu nyeti na muhimu ambao ungeweza kuwa mbadala mkubwa wa umeme wa maji.

Tunapenda kuungana na wabunge wa upinzani walioitaka uchunguzi wa kina ufanywe na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB) ili kubaini ni nani hasa waliokwamisha utekelezaji wa mradi huu.

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), wakati akitoa maoni ya upinzani kuhusu bajeti ya wizara hiyo, alieleza waziwazi kwamba mradi huu wa Mchuchuma umezingirwa na wingu la rushwa.

Alisema upande wa upinzani unashangaa kuona kwamba wizara husika inaamua kukaa kimya wakati ’wajanja’ walipoamua kuachana na mradi huu wakati utekelezaji wake ulishaamuliwa na Baraza la Mawaziri.

Sisi hatusemi kwamba kuna rushwa, bali pia tunashangaa ni kwa vipi kama kweli mawaziri walipitisha uamuzi huo, likatokea kundi la watu wakatupilia mbali maamuzi hayo na kufanya kile walilotaka wao na mawaziri nao wakaamua kukaa kimya?

Simulizi za mradi huu sasa zimetosha na hatuamini kama watu wanapenda kuendelea kuzisikiliza tena. Ni hadithi ya kuchosha sasa kinachotakiwa ni utekelezaji kwa vitendo. Na hii ndiyo imani kubwa ya wananchi.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.