|
Uboreshaji kilimo usiathiri mazingira endelevu
2006-07-19 10:30:35
Na Jackson Kalindimya
Watanzania wengi wanaishi vijijini wakijishughulisha na kilimo. Pamoja na juhudi kubwa zinazoendelea kufanyika ikiwa pamoja na kupanua mashamba, kufyeka misitu na shughuli nyinginezo za binadamu umasikini umekuwa kama sehemu ya maisha ya wakulima.
Makala hii ya Mwandishi Wetu, Jackson Kalindimya yazungumzia umuhimu wa kilimo kisichoathiri mazingira endelevu.
Tanzania tangu ipate uhuru, imekuwa ikisemwa kuwa ni taifa la wakulima na wafanyakazi. Umuhimu wa kilimo katika uchumi wa taifa ni mkubwa mno hasa ikizingatiwa kuwa nchi haina viwanda vikubwa ambavyo vinaweza kutegemewa sana kiuchumi kama ilivyo katika nchi zilizoendelea Pamoja na umuhimu huo kwa uchumi katika miaka zaidi ya 45 tangu uhuru upatikane, kumekuwa na mabadiliko si makubwa sana miongoni mwa wakulima kuhusu maendeleo ya kiuchumi, kijamii na teknolojia ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha umasikini wao. Jembe la mkono, shoka na mvua za msimu zisizotabirika zimeendelea kuwa zana muhimu kwa kilimo.
Umasikini wa watu wengi wa vijijini ambao ni wakulima ni dhahiri na maendeleo endelevu bado ni kama ndoto ya mbali licha ya juhudi za serikali zinazoendelea kufanywa.
Sensa ya mwaka 2002 zaidi ya asilimia 72 ya watanzania wanajishughulisha na shughuli za kilimo.Suala sio idadi kubwa ya watu wanaofanya shughuli hizo, ni aina gani ya kilimo na teknolojia inayotumika.
Wakulima wengi ni masikini wanaoendesha kilimo kwa kutumia teknolojia duni isiyozingatia uharibifu wa mazingira ili kujikimu kimaisha.Mashamba yale yale yamekuwa yakilimwa kwa muda mrefu bila ya kufanyika juhudi za makusudi katika kuirutubisha ardhi hata kukosa rutuba kwa kiwango ambacho familia sasa zinashindwa kupata hata chakula na fedha za kutosheleza mahitaji.
Ardhi ya aina hiyo inahitaji uwekezaji mkubwa ili kuifanya izalishe kwa tija. Kwao jitihada za kupiga vita umasikini maana yake ni kufyeka misitu zaidi, kuharibu mazingira na uoto wa asili wakati wakipanua mashamba na kutumia nishati ya kuni na mkaa katika maisha yao yote.
Bei ya pembejeo imekuwa ikipanda mara kwa mara hata kuwalazimisha baadhi ya wakulima kuacha kuzitumia ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa kutumia eneo dogo kwani vingenvyo ni kujibebesha mzigo.
Wakati hayo yakitokea ni kwamba, bei ya mazao ya kilimo imekuwa ikishuka au hailingani na gharama za uzalishaji, hata kusababisha wakulima au watu wengine kushindwa kuwekeza kikamilifu katika uzalishaji.
Kuporomoka kwa vyama vingi vya ushirika kumechangia kushuka kwa tija katika kilimo, kwa sababu ni kama hakuna taasisi yenye nia ya dhati hasa kuwasaidia wakulima kupata pembejeo hata kwa mkopo.
Mtaalamu mshauri wa taasisi ya utafiti ( ESRF),Prof Ndalahwa Madulu anasema mazingira duni ya kilimo yanawalazimisha wakulima kupanua amshamba kwa kufyeka misitu kama njia ya kujiongezea mazao yao ili kupunguza kiwango cha umasikini wao.
Hali hiyo inasababisha ardhi kuwa nusu jangwa na kuvuruga mfumo wa asili wa ardhi ikiwemo katika miteremko ya milima na kwenye mito.
Uchunguzi uliofanyika katika milima ya Usambara, Pare na Uluguru na katika baadhi ya mito kunathibitisha madai hayo kuhusu hali mbaya ya uharibifu wa mazingira.Mkakati wa makusudi unatakiwa kuchukuliwa ili kuyanusuru mazingira.
Uharibifu wa mazingira licha ya kuwepo katika maeneo mengi pia umekitihiri katika mabonde huko Iringa na ulimaji katika kingo za mito mkoani Dodoma na Shinyanga.
Kilimo katika maeneo hayo kimelenga kupiga vita umasikini lakini athari zake si rafiki wa mazingira endelevu.
Wakati uharibifu wa mazingira unazidi kuongezeka katika maeneo mbalimbali nchini, ni kwamba kiwango cha umaskini wa watu pia kinazidi kuongezeka.Upanuaji wa kilimo kwa wakulima bado haujawasaidia sana kupunguza kiwango cha umasikini.
Akichambua uhusiano kati ya umasikini na mazingira,Cooksey na Likwelile(2002) ameainisha umuhimu wa mazingira kwa watu masikini. Watu maskini wanategemea mno raslimali zilizomo katika mazingira kwa ajili ya maisha yao ambapo wanateseka sana wakati mazingira yanapoathiriwa au wanapowekewa vikwazo vya kuzifikia raslimali zilizomo.
Mazingira endelevu yana umuhimu wa kipekee kwa maisha ya watu katika kuamua hali ya umasikini kwa sababu watu masikini hasa wa vijijini wanategemea sana kuhusu bionuwai kwa ajili ya kupata mahitaji ya lazima kama vile uzalishaji wa chakula na shughuli nyingine zikiwemo upatikanaji wa nishati za kupikia, dawa, chakula, maji na fedha.
Pamoja na kwamba kumekuwa kukifanyika shughuli mbalimbali kwa kile kinachosemwa kuwa kuchangia kupiga vita umasikini na kuchangia kukua kwa uchumi wa taifa,baadhi ya shughuli hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira kama vile ufyekaji wa misitu, mmomonyoko wa ardhi na uharibifu wa maji, hewa na raslimali za habarini na majini.
Serikali katika tangazo lake la hivi karibuni kuhusu hatua za haraka za kuhifadhi mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji, lililotolewa na Makamu wa Rais, Dk Ali Mohammed Shein alisema shughuli za kilimo zisizo endelevu, zinazofanwa katika maeneo ya vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kwenye vilele vya milima, miteremko ya milima na sehemu nyingi kama vile makundi makubwa ya mifugo kuhamahama na kuathiri uoto wa asili imechangia sana uharibifu mkubwa wa ardhi, vyanzo vya maji, miti na uchomaji wa misitu.
Nchi imefikishwa mahali ambapo sasa uharibifu wa mazingira ni kiini kinachosababisha hali ya jangwa, ukame na kukauka kwa vyanzo vya maji nchini.Kwa wastani hekta za misitu zipatazo 91,300 hupotea kila mwaka.
Dk Shein aliwataka wakulima na wafugaji waliovamia mabonde ya Usangu na Kilombero waondoke mara moja. Hatua hiyo pia inawahusu wafugaji na wakulima walio ndani ya hifadhi za mbuga za wanyama na maeneo ya ardhi-owevu ya Ihefu na eneo owevu la Kilombero lililotengwa kimataifa chini ya mkataba wa Ramsar na maeneo mengine kama hayo.
Aliwataka wakulima wa tumbaku, chai na watumiaji wengine wakubwa wa miti, kuni na makaa waanzishe mashamba yao ya miti. Agizo hilo pia linazihusu taasisi za elimu, majeshi na viwanda waandae vitalu vya miche ya miti ifaayo, wapande miti na kuitunza kwa ajili ya nishati, ifikapo Januari 2007.
Kwa namna yoyote ile hatua hii ya kuyalinda mazingira na kuyafanya kuwa endelevu ni ya kuungwa mkono na watu wote ambao wanaitakia mema nchi na kuirithisha kwa vizazi vijavyo ikiwa na mazingira endelevu.
Labda suala la kuangaliwa kwa makini ni kuhusu elimu ya hifadhi ambayo imekuwa ikitolewa kwa miaka mingi je njia zinazotumika ni sahihi na zimeleta mabadiliko yoyote katika maisha ya watu na mazingira yao?
Waziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula, Bw Joseph Mungai akiwasilisha makadirio ya fedha katika kipindi cha mwaka 2006/07 alisema mavuno ya chakula mwaka huu yanatarajiwa kufikia tani milioni 10.73.
Inakadiriwa kutakuwa na ziada ya tani milioni moja za chakula toka katika makisio ya mahitaji ya sasa ya tani milioni 9.73.
Katika makadirio hayo, imebainisha kuwa mkazo mkubwa utakuwa katika mbinu za kuboresha sekta ya kilimo hasa kuanzisha miradi ya umwagiliaji katika ngazi ya taifa na wilaya. Serikali imetenga sh tirioni 1.9.
Yatarajia kutumia sh bilioni 1,493 kwa ajili ya umwagiliaji katika ngazi ya wilaya na sh bilioni 474 kwa ngazi ya taifa na mikakati mingine.
Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza ruzuku kwenye mbolea na utekelezaji wa Sekta ya Programu ya Maendeleo ya Kilimo(ASDP)
Mhe Rais Kikwete hivi karibuni aliweka jiwe la msingi la Mradi wa Upanuzi wa Kiwanda cha Uzalishaji Mbolea cha Minjingu,mkoani Manyara.
Alisema serikali imekusudia kufanya mageuzi makubwa ya kilimo nchini kwa kusisitiza matumizi ya mbolea kwa kiwango cha juu ili kupata mavuno yenye kukidhi ubora wa mahitaji ya ndani na soko la nje.
Katika bajeti ya mwaka huu, kumekuwa na ongezeko kubwa kwa ruzuku ya mbolea toka sh bilioni saba hadi sh bilioni 21. Hatua hii ni nzuri na motisha kwa kilimo ambayo imelenga kuongeza faida kwa kupunguza gharama za uzalishaji.
Dk Damian Gabagambi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) akichambua bajeti ya mwaka huu, alisema kuwa utoaji wa ruzuku ya mbolea ambao umekuwa ukisifiwa sana na jamii, yawezekana usitoe matokeo yanayotarajiwa hata baada ya matumizi ya sh bilioni 21, kutokana na hali halisi ya huko nyuma.serikali ilitoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ili nchi ijitosheleze kwa chakula.
Utoaji huo wa ruzuku ulioanzia kwa zao la mahindi haujaleta mabadiliko huku wakulima wakilalamika kuwa mbolea iliyowekewa ruzuku haiwafikii.
Uchunguzi umebainisha kuwa mbolea hiyo nyingi imekuwa ikiishia kwenye maduka yanayozingata biashara na faida au kuvushwa kwenda kuuzwa katika nchi jirani.
Halidhalika hata kama mbolea hiyo iliwafikia wakulima, haifahamiki sawasawa kama itatumiwa kwa uzalishaji wa mahindi tu na sio mazao mengine yanatoa faida haraka kama vile nyanya, kabeji na vitunguu.
Matokeo yake wakulima hawapigi hatua za uhakika wa maendeleo na kubakia wakiendelea na kilimo kisicho endelevu kwa mazingira.
Hatua zinazochukuliwa zinazodhaniwa kuwa zitaboresha kilimo, kuokoa uharibifu wa mazingira na kuinua hali za maisha ya wakulima walio wengi hautafikiwa kama umakini hautakuwepo.
Wakulima wataendelea kuwa masikini,hawatabadili aina ya kilimo chao,matumizi ya nishati ya kuni na mkaa na uharibifu wa mazingira.
Kwa hiyo jitihada zozote za kuboresha hali ya kilimo kwa wakulima sio tu zizingatie upatikanaji wa mbolea ni pamoja na kutilia mkazo hifadhi ya mazingira, teknolojia rahisi, pembejeo na hifadhi ya uoto wa asili katika misitu na majini ambavyo ni vyanzo vya maisha ya viumbe na malihai vinginevyo ni kujidanganya na kushindwa kufikia Malengo ya Milenia(MDG).
Mkurugenzi Mkuu wa The World Conservation Union,Achim Steiner alisema kuwa hifadhi ya mazingira kwa ajili ya kupiga vita umasikini ni juhudi zinazoelekea kupunguza umasikini na usalama wa maisha ya watu ambayo ni muhimu.
Mkakati wa Kupiga Vita Umasikini na Kuinua Uchumi(MKUKUTA) uhakikishwe kuwa unatoa kipaumbele kwa uwezezaji wa dhati katika elimu, teknolojia na fedha katika maendeleo ya kilimo, hifadhi ya mazingira na uboreshaji miundo mbinu ikiwemo barabara ili wakulima baada ya kuongeza uzalishaji waweze kuyafikia masoko na mfumo wa bei ya mazao uzingatie gharama za uzalishaji kama kweli tunataka kuona wakulima wanajinasua katika tope la umasikini na mazingira kuwa endelevu.
|