|
Sheria hizi kandamizi kwa wanawake sasa basi
2006-07-17 10:17:30
Na JACKSON KALINDIMYA
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Rais Jakaya Kikwete, ametoa matumaini mapya kwa wanawake nchini pale alipotamka wazi kwamba sheria zinazowakandamiza wanawake zimeanza kushughulikiwa kwa kasi, nguvu na ari mpya.
Alitoa matumaini hayo Jijini Dar es Salaam juzi, wakati alipokuwa akijibu risala ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya CCM ya Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT), Anna Abdallah, aliyoitoa katika sherehe ya kumpongeza kuchaguliwa Mwenyekiti mpya wa CCM na kumuaga aliyekuwa na wadhifa huo, Rais Mstaafu Awamu ya Tatu, Bw.Benjamin Mkapa.
Rais Kikwete katika kuonyesha dhamira yake ya dhati kuhusu kilio cha wanawake, akasema katika sherehe hiyo kwamba amempa rungu Waziri wa Sheria na Katiba, Dk.Mary Nagu kusimamia urekebishaji au ufutaji wa sheria ambazo zimekuwa zikimkandamiza mwanamke.
Mmelalamika kuhusu baadhi ya sheria ambazo zinamkandamiza mwanamke...kama tatizo ni sheria, Waziri wa Sheria ni mwanamke, kilio kina wenyewe, wanaume tutawasaidia kuwafuta machozi, alisisitiza.
Kilio cha wanawake kuhusu sheria kandamizi hakikuanza leo.
Itakumbukwa hata serikali (siyo awamu ya sasa), iliwahi kuunda Tume kuhusu marekebisho ya sheria ambapo ilipendekeza sheria zipatazo 40 ambazo ni kandamizi zifutwe, miongoni zikiwemo ile ya uchawi, ukeketaj, watoto wa kike kuolewa na umri wa miaka 15 na kadhalika.
Tangu wakati huo, hakuna hatua za dhati ambazo zilichukuliwa, jambo ambalo lilipelekea wanawake kuendelea kuteseka.
Wapo wanawake vikongwe ambao wamekuwa wakiuawa kila kukicha kutokana na imani za uchawi, ukeketaji wa mabinti wadogo na hata kuwaozesha kwa nguvu wakiwa na umri mdogo.
Haya ni matumaini mapya kwa wanawake kwamba serikali imeingia ulingoni kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo hilo. Uchungu wa mwana, hakika aujua mzazi.
Kwa mantiki hiyo, tunaamini kwamba Waziri wa Sheria ambaye ni mwanamke, atafanya kila linalowezekana ama kurekebisha vipengele vyote kandamizi ndani ya sheria zetu na zile zilizopitwa na wakati kuzifutilia mbali.
Hakuna asiyetambua kwamba hiki ni kizazi cha mabadiliko. Dunia sasa imeingia katika sura ya kisayansi na kiteknolojia. Mambo ambayo yanarudisha nyuma maendeleo kama sheria hizo kandamizi hayana tena nafasi kwa sasa.
Watu wanataka amani na utulivu, maisha bora yenye matumaini. Athari zinazotokana na sheria zinazopigiwa kelele ni dhahiri ndani ya jamii yetu.
Wazee vikongwe wanafupishiwa maisha kutokana na kudhaniwa ni wachawi. Haki ya binadamu kuishi hapa iko wapi.
Watoto wetu wa kike ambao ndio wazazi wa baadaye wanatumbukizwa mapema katika matatizo ya kiafya na kifamilia. Wapo wengi wanaokatishwa masomo na kuozeshwa japokuwa umri hauruhusu.
Wapo wanaopoteza maisha kutokana na uzazi katika umri mdogo. Hupoteza damu nyingi, athari za kiakili na kwa wale wanaoketetwa hali kadhalika.
Serikali imekuwa ikihimiza ongezeko la watoto wa kike kuandikishwa shule hata ngazi za vyuo vikuu. Sasa kama sheria kandamizi zitaendelea kufumbiwa macho na athari ndio hizo tumeshaziona, matarajio hayo yatafikiwa vipi?
Lazima turudi nyuma tuangalie mizizi ya tatizo. Sheria zetu ambazo tulizianzisha wenyewe ndizo zinazotunyonga. Maadamu tumeshazigundua, basi tuzifanyie kazi kwa bidii zote.
Ni matarajio yetu kwamba Waziri wa Sheria baada ya kupewa rungu na Rais atazifanyia kazi sheria zote kandamizi ama kwa kuzirekebisha ili zikidhi mahitaji ya kizazi cha sasa au azifutilie mbali kutokana na madhara yake kwa jamii yetu.
|