17 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kiswahili kinavyokua lugha za asili zinakufa
 
2006-07-17 10:16:50
Na JACKSON KALINDIMYA

Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI),Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivi karibuni ilimuaga Mkurugenzi aliyemaliza muda wake,Profesa Mugyabuso Mulokozi.

Katika makala hii Mwandishi Wetu, JACKSON KALINDIMYA anahojiana naye juu ya mafanikio ,changamoto alizokumbana nazo katika uongozi wake , na nini kifanyike kuiboresha zaidi lugha hiyo.



SWALI:Umekuwa Mkurugenzi wa TUKI kwa kipindi cha miaka sita sasa.Je ni mafanikio gani ya kujivunia ambayo TUKI yaweza kujivunia katika uongozi wako?

JIBU:Hatua tulizopiga za wazi zaidi ni kukiingiza Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) ambalo ni tukio jipya.Tulifanikiwa kuandaa programu za Kilinux na microsoft husika kwa kiasi fulani ikiwa pamoja na kuandaa kisahihishi(spellcheck).

Tumetoa kamusi za elektroniki kwa lugha za Kiingereza kwa Kiswahili na kinyume chake.Mradi wa SALAMA ulihusika na kukusanya taarifa za Kiswahili na kuziweka katika hazina moja,sitilahi na nyinginezo.Hazina(kanzi) yote ya maneno na misemo ili isaidie kufanikisha lengo.

Katika kipindi hicho tumechapisha machapisho mbalimbali kutokana na utafiti na taaluma.Taaluma ya fasihi, tumeshughulikia maisha na kazi za Shaaban Robert.

Kwa upande wa utamaduni tumeshughulikia miviga(rituals) kama vile kuhusu Vita vya Majimaji ambapo wananchi walitumia imani za jadi wa watu wengi toka Ruvuma,Njombe,Pwani na kwingineko katika kutetea nchi yao.Imani zao za jadi zilifikisha ujumbe kwa watu wote.

Kuhusu Sarufi na Isimu(miundo ya matamshi) kwa sauti za Kiswahili.Tumejaribu kuchunguza huko shuleni wanafundifishwaje na tuwasaidiaje.

Tumetoa vitabu vinavyosomwa na walimu wa sekondari ikiwa pamoja na kanda ili kuangalia hali ya Kiswahili katika shule na mengineyo.

Huwezi kuendeleza Kiswahili katika ngazi ya Chuo Kikuu tu huku kwingineko hakuendelezwi.Tatizo kubwa la



Kiswahili kipo shuleni, baadhi ya walimu hawana upeo wa kutosha wa kufundisha.Mitaala nayo ina matatizo na hivyo tuliwasiliana na serikali ili iifanyie kazi.

Kwa upande wa ukuzaji wa Kiswahili nje ya mipaka ya Tanzania, mkakati wa makusudi umefanyika katika nchi mbalimbali zikiwemo Kenya na Uganda.

Tumeshiriki katika matamasha,makongamano na kutoa machapisho.Mkakati huo sasa nchi mbalimbali kama vile Zimbabwe wanajua wakiwa na shida kuhusu lugha ya Kiswahili waende wapi na hivyo tumekuwa na mawasilinao ya mara kwa mara kwa manufaa ya Kiswahili.

Tumeshiriki pia katika kuanzisha Chama cha Walimu wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki(CHAKAMA).

Tumesaidia sana uunganishaji na uratibu wa maendeleo ya lugha hiyo katika vyuo vikuu vya Makerere,Eldoret, Moi na Nairobi ambapo tunajua wanafanya nini kuendeleza lugha hiyo na tunakutana kila mwaka.Kikao kijacho kitakuwa Arusha.

TUKI imeshirikiana na serikali kuhamaisha Umoja wa Afrika (AU),Bunge la Afrika na kwingineko kuona umuhimu wa matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Iliundwa kamati ya kitaifa,iliyoongozwa wakati huo na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Mhe Jakaya Kikwete (sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania).Baadaye alimteua Waziri Mohamed Seif Khatib kuendelea na kazi yake.

Matokeo ya jumla ya mikakati hiyo ni kuongezeka kwa watumiaji wa Kiswahili katika eneo la ukanda huu wa Afrika na Maziwa Makuu ikilinganishwa na miaka 20 iliyopita.Kwa sasa Kiswahili kinazungumzwa sana Uganda.

(Kampala) na Kenya.Watu wanapenda sana kusikiliza na kuangalia matangazo ya vituo vya ITV-EATV kwenye mabaa na kwingineko Kiswahili kimeanza kuzoeleka.

Tulifanikiwa kuandaa mashindano ya wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vikuu.Wanafunzi wa nchi za Kenya na Uganda walishiriki na hii inadhihirisha namna gani Kiswahili kinaenea hadi vijijini.

Pia tulitoa Kamusi, toleo jipya la Kiswahili Sanifu ambalo ni bora zaidi.Toleo la kwanza mwaka 1981.Na tumetoa kitabu cha kufundisha taaluma ya Kompyuta kwa Kiswahili hata katika shule za msingi.

SWALI:Je changamoto gani zilizowakabilii katika kipindi hicho?

JIBU:Kimtazamo wa kisiasa nchini kuhusu lugha ya Kiswahili. Katika awamu iliyopita ni kama haikupenda sana kuyafanyia kazi mapendekezo mengi ambayo yalikataliwa.

Miongoni mwa hayo ni Kiswahili kitambuliwe katika katiba kuwa ni lugha ya taifa.Tatizo kubwa lipo kwa baadhi ya watu ambao wana mamlaka ya kuamua wana mitazamo hasi.

Bahati nzuri awamu hii ni welewa zaidi kwa suala hili na tunadhani baadhi ya mambo yatashughulikiwa kwa manufaa ya maendeleo ya Kiswahili.

Matatizo ya fedha na nyenzo za kufanyia kazi. Uwezo wa kufanya utafiti bado ni mdogo. Kama hakuna fedha ni vigumu kufika vijijini.

SWALI:Unazungumziaje hali ya Kiswahili huko nje? Kuna pilikapilika nyingi kuhusu lugha hii.Unadhani hayo yanafanyika ni kwa nia hasa ya kukipenda Kiswahili au kuna nini?

JIBU: Kuna makundi matatu ya watu. Kuna wale ambao wanakipenda Kiswahili na wako tayari kuona kinastawi. Wako wanaojishughulisha na Kiswahili kama sehemu ya taaluma.

Lugha ya Kiswahili ni changamoto kwao kwamba kama wanafanya kwa lugha nyingine na kufanikiwa kwa nini isiwe hii?

Kuna kundi jingine la wanaofanya hivyo kwa maslahi ya kitaifa. Ni muhimu kwao kwa sababu taifa lao linakihitaji kwa sababu mbalimbali kama vile kibiashara, kijeshi, kiusalama, kisiasa, mahusiano na mengineyo. Kila nchi inayoendesha pilikapilika za Kiswahili sio kwa sababu inapenda Kiswahili.

Marekeni inaleta wanafunzi kujifunza Kiswahili,inataka walimu toka huku.Yawezekana ni hali ya dunia ya sasa wamarekani wajue lugha hiyo.

Microsoft imeanzisha programu za Kiswahili kwa lengo la kibiashara kwa sababu lugha hii inatumiwa na watu zaidi ya milioni 100.

SWALI:Kadri Kiswahili inavyozidi kujiimarisha na kutumiwa na watu wengi zaidi nchini ni kama inachangia kuua lugha nyingine.Unasemaje kwa hilo?

JIBU: Umoja wa Afrika(AU) mwaka 1986, ilipitisha azimio lugha nyingine za kiafrika ziheshimiwe.Lugha zinakufa kwa sababu hazitumiki ipasavyo,hasa zile ndogondogo za pwani zinamezwa na Kiswahili.

Sababu ya lugha hizo kutotumika ni kwamba hazina vifaa, maandishi kama vile vitabu na magazeti yanayoandikwa kwa lugha hizo watu wanakuwa hawajifunzi na wanaanza kusahau.

Au iliazimia kuwa ni bora kuwa na mfumo wa elimu uliojikita katika lugha mbili. Lugha ya mama ambayo mtoto anajifunza akiwa utotoni na nyingine anajifunza akiwa shule.

Hapa nchini labda elimu ingejikita katika matumizi ya lugha tatu. Lugha ya Kiswahili na Kiingereza, mfumo huu wanasiasa hawaukubali.Lugha ya mtoto ina gharama zake kama vile kuandaliwa vitabu na machapisho mengineyo Watanzania inawapa shida.

Njia nzuri na rahisi ni kuchapisha na kusambaza vitabu,magazeti katika lugha zao kama vile kisukuma,kigogo,kihaya na nyinginezo.Hii ni njia ya kudumisha lugha.

Inawezekana kabisa kama hatutaogopa kinachoitwa ukabila.Ukabila unaletwa na siasa kama unatumiwa na watu wanaopenda madaraka.

Kihaya, kichaga na nyinginezo kisiwe na ukabila.Ieleweke hakuna fursa ya kuingiza siasa katika lugha za watu. Wakati wa mkoloni makabila yalikuwepo.

Ni hasara lugha kupotea. Lugha zimebeba urithi wa falsafa, mapokeo na utamaduni zikipotea, zinapoteza mambo mengine kama vile majina ya miti, mimea yote yana maana na kukumbushia matumizi yake.

Jina likipotea likaitwa kwa Kiswahili hata maarifa yatapotea. Suala hili tuliangalie kwa makini sana. Zikiendelezwa tunapata maarifa na kutajirisha Kiswahili. Lugha zina sanaa iliyopevuka sana, hakuna aliyefanikiwa kuiua.

SWALI:Nini mtazamo wako kuhusu uandishi wa vitabu vya Kiswahili hapa nchini?

JIBU:Tuna washairi zaidi ya 5,000 wanaoandika magazetini na redioni.Wana athari fulani, mawazo, itikadi, siasa na mengneyo.

Kuna malengo ya kuhifadhi lugha ya Kiswahili.
Watunzi wa vitabu hatunao wengi, lakini wanasawiri maisha yetu katika kipindi chetu tuna matatizo na mapambano.

Riwaya na tamthiliya haya huwezi kuyapata katika taaluma.Vitabu vinabeba maarifa,sanaa na burudani. Maarifa ni vichocheo ikilinganishwa na sanaa na burudani.
Tatizo la waandishi kunakuwa na ile hali ya kudharauliwa na kuporwa haki zao. Hawapewi heshima na haki.

Sheria ya Hakimiliki haifuatwi.Wachapishaji hawawalipi kabisa waandishi wao na nakala zinazochapishwa waandishi hawaambiwi.Mimi ni muathirika vitabu vyangu vitano sipewi chochote vingine vimeuzwa sana.

Halikadhalkika tabia ya watu kutoa fotokopi hasa wanafunzi wa vyuo vikuu, hiyo inamnyima mwandishi na mchapishaj haki yao.Waandishi wana mchango.Waandishi wa vitabu wana mchango muhimu lakini haki zao haziheshimiwi.

SWALI:Wewe unastaafu nafasi yako ya Ukurugenzi.Unadhani TUKI itaendelea kuwa kama inavyotarajiwa?

JIBU:TUKI ina mifumo,utaratibu na mipango ya utafiti.Miradi iliyoanza inaendelea na ile bado Mkurugenzi mpya ataangalia namna gani ya kuianzisha.

Tumepeleka watu vyuoni wapate ujuzi zaidi hadi kiwango cha shahada ya udaktari ili waendeleze shughuli.

Tumeimarisha kitengo cha uchapishaji(mitambo na uwezo upo) na machapisho mbalimbali yanasambazwa.Nyenzo za kazi zimeimarishwa,wana kompyuta,viyoyozi na kama mtu anashindwa ni yeye mwenyewe.

Tumeanzisha makavazi (hifadhi ya nyaraka za kale) hata miaka mia yatadumu, kuna maktaba na mengineyo.

SWALI:Baada ya kustaafu unakusudia kufanya nini?

JIBU:Nastaafu nafasi ya ukurugenzi,lakini bado ni mwajiriwa wa TUKI.Nitaendelea na kazi ya fasihi(taaluma). Niliendelea kama mwana taaluma,sasa nitakuwa na muda mwingi wa taaluma.

Ninatarajia kuandaa chapisho la pili la Shaaban Robert,kazi za washairi wengine(historia ya ushairi) na miradi mingine, uchambuzi wa vitabu vya fasihi,vitabu vya kufundishia shuleni,fasihi simulizi,tenzi za nanga za kihaya.Taarifa nilizokusanya ni nyingi mno.

Kwa upande wa utamaduni (utafiti),na uendelezaji,uchapishaji vitabu,sanaa mbalimbali,mapokezi ya kihistoria yote nitayafanyia kazi.

Isimu,juu ya nafasi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia,lugha za makabila,Kiswahili nje ya Tanzania,Umoja wa Afrika(AU) na kwingineko.
SWALI:Una maoni gani mengine?

JIBU:Jamii itambue Kiswahili ndio lugha ya taifa,ndio utambulisho.Kiswahili kipewe aula.Wananchi wanahitaji kuhamasishwa wawe na mwamko wa lugha na utamaduni.Lugha yao ikikataliwa basi .

Hakuna mwamko wa kuamka na kuitetea.Vyama vya siasa ni muhimu kufikiria kuhusu lugha na utambulisho wake,vinginevyo ni rahisi kuifuta lugha yetu.

Wanataaluma, vyombo vya habari,wanasiasa na wananchi waungane kuitete,tuivalie njuga.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.