16 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Nilifungasha virago kwa wivu, mume anachekelea alete mwingine
 
2006-07-16 10:37:24
Na Anti Flora Wingia

Wivu kwa mwanadamu ni jambo la kawaida. Lakini wivu una faida na hasara zake. Yupo anayeona wivu kwa kufurahia mafanikio ya mwenzake.

Na yupo anayeona wivu kwa kuchukia maendeleo na mafanikio ya wengine.

Naam. Hebu mpenzi msomaji kabla sijafika mbali, sikia kituko hiki cha kusimuliwa toka Mpwapwa, kilicholenga kuonyesha hasara mojawapo ya wivu.

Yupo dada mmoja aliyeolewa miaka miwili iliyopita kwa ndoa Takatifu na sasa ana mtoto mmoja. Mumewe ni mfanyabiashara na mkamata maji(pombe) mzuri.

Kuna baa moja ambako bibie huyo na mumewe hupendelea kunywa pombe. Upo wakati wawili hawa huja pamoja na wakati mwingine mumewe huja peke yake.

Siku moja, kwa mujibu wa msimuliaji wa kituko hiki, bwana yule alikuja peke yake na kuamua kuketi eneo la kaunta katika baa ile. Mfanyakazi wa kaunta alikuwa mwanamama.

Siku hiyo mwanamama huyo akatoka nje ya kaunta na kuketi na bwana yule, tena kwa karibu sana.

Bila kutarajiwa, mwenye mume(mke) akaingia na moja kwa moja akamfuata mumewe kaunta. Kuona mkao wa mumewe na jinsi alivyokuwa amemkumbatia bibie wa kaunta, akawa ameduwaa kwa muda.

Kisha akamuuliza mumewe, ’’mbona mnapigana mabusu hadharani huku watu wakiwatizama? Mume akajibu, ’’najifurahisha tu mke wangu, ungetukuta kitandani ndiyo ungelalamika lakini hapa tunajifurahisha tu, hakuna ubaya’’.

Bibie kusikia vile kwa hasira akaondoka zake. Kumbe moja kwa moja usiku ule yapata saa tano alikwenda kulalamika kwa mshenga na pia kwa ndugu zake.

Nao ndugu kesho yake ikabidi wakamuulize mumewe kulikoni na yeye akajitetea vilivyo.

Hata hiyo, mke yule hakuridhika akaamua kufunga virago akaenda kijijini kwao alikozaliwa.

Huku nyuma mumewe akaamua kuwa sambamba na mwanamama yule wa kaunta tena kwa kasi kubwa.

Baada ya siku kupita, mume yule akamfuata mkewe kijijini kwa usuluhishi lakini ikasemekana alikataa kurejea. Mume akarudi mjini akabuni mbinu.

Akampigia simu na kumwambia kwamba kama amekataa kurudi basi mwanamama aliyemkuta naye baa ndiyo mkewe na ndiye aliyechukua nafasi yake nyumbani.

Bibie kusikia vile, kesho yake tu alifunga safari na kurudi kwa mumewe. Msimulizi wa kituko hiki anasema kuwa hivi sasa bibie ametulia, mpole na wala haendi kumsaka tena mumewe kwenye baa labda watoke pamoja kwa kinywaji. Ama kweli Maisha ndivyo Yalivyo.

Wivu mwingine ndio kama hivyo. Unadhani unamkomoa mwenzako kumbe unajiumiza mwenyewe.

Huu ni wivu wenye hasara. Kama bibie angeshikilia msimamo wake wa kubaki kijijini, siyo ajabu mumewe angeamua kuishi na mwanamama yule wa kaunta ambaye alikuwa free(aliyekuwa ameolewa lakini akaachana na mumewe).

Mpenzi msomaji, mwanamke kumuonea wivu mumewe ni jambo la kawaida. Lakini katika kufanya hivyo, kunahitaji tahadhari kubwa.

Yafaa mtu afikirie mara mbili kabla ya kurusha wivu wake hewani. Vinginevyo, waweza kujikuta unaamua jambo fulani, ukidhani unamkomoa mwenzako, kumbe yeye ndiyo kwanza anafurahia kutokana na sababu fulani fulani.

Wanaume wengine hawatabiriki. Waweza kumfumania na mwanamke mwingine yeye akawa cool.

Na wakati mwingine atadiriki hata kukuuliza ’’kwani una shida gani wakati nyumbani kila kitu nakutimizia’’.

Mwanaume wa aina hii anasahau kwamba suala siyo kutimiziwa kila kitu nyumbani.

Ni wivu wa kutotaka kushirikiana tunda ulipendalo na mtu mwingine. Si unajua ’mtu chake? Huo ndio ukweli.

Bibie aliyetimkia kijijini baada ya kumfuma mumewe akiwa na mwanamke mwingine katika mkao usiokuwa wa kawaida, hakika alikuwa na haki ya kulia wivu.

Ni kutokana na kutoamini macho yake kwa kile alichokiona. Na mbaya zaidi, mume yule hakuonyesha kushtuka.

Ndivyo wanaume wengine walivyo, hawajali na wengine hudiriki kumwambia mke ’’kama umechoka ondoka wapo wanaohitaji hifadhi’’.

Upo ule msemo kwamba ’hasira ni hasara’. Bibie alitimka kutokana na hasira pale mumewe alipomjibu mbofumbofu badala ya kuomba radhi.

Neno ’samahani’ laonekana jepesi, simple, lakini linabeba uzito mkubwa sana. Umekosea omba samahani yaishe. Au siyo?

Naam. Lakini kama nilivyosema awali, wanaume wengine ni jeuri hukejeli hata pale anapojua dhahiri kwamba amekosea jambo fulani. Wenzetu hawa ndivyo walivyo baadhi yao.

Kwa mantiki hiyo, wanawake wanaoangukia kwa waume wa aina hiyo, wapo wanaovumilia japo ’chozi’ rohoni na wengine ndio kama huyo aliyetimka lakini akarejea baada ya kuambia mwenzake aliyemlilia wivu ’kajaa tele’ nyumbani kwake. Ama kweli Maisha Ndivyo Yalivyo.
Wasalaam.

E-mail:fwingia@guardian.co.tz

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.