14 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Twiga Stars ijiandae vizuri
 
2006-07-14 11:47:09
Na Mhariri

Timu ya taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars, kwa sasa inajiandaa kwa mchezo wa kwanza wa kutafuta nafasi ya kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika.

Twiga Stars inatarajia kucheza na timu ya taifa ya Afrika Kusini Julai 22 katika mchezo wa kwanza utakaofanyika ugenini kabla ya kurudiana jijini Dar es Salaam wiki mbili baadae.

Kocha wa timu hiyo Salum Gwaje alikaririwa na vyombo vya habari akitamba kuwa timu yake imejiandaa vizuri na itaibuka na ushindi katika mchezo huo ili ijiweke katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Hata hivyo, pamoja na matumaini hayo makubwa ya kocha Gwaje, kitu ambacho ni cha kawaida kwa kocha kutamba kushinda hata akijua kuwa timu yake ni dhaifu, lakini timu hiyo haijapata mechi za uhakika za majaribio.

Kukosekana kwa mechi nyingi za majaribio kunaweza kuwafanya wachezaji wa timu hiyo kushindwa kujiamini na kuwa na uoga wa mechi za kimataifa, lakini kama wangecheza mechi nyingi za kimataifa za majaribio, bila shaka wangekuwa na uzoefu fulani.

Tunapenda kuliomba benchi zima la ufundi la Twiga Stars kujitahidi kuiandaa vizuri timu hiyo kwani isije ikatokea kama huko nyuma timu hiyo ilipofungishwa virago na Zimbabwe baada ya kufungwa mabao kibao.

Afrika Kusini wamepiga hatua kubwa katika soka liwe na wanawake au wanaume, wako mbele yetu zaidi, hivyo timu yetu ipate maandalizi ya kutosha ili kuiwezesha kufanya vizuri katika mchezo huo wa kwanza.

Hakuna miujiza katika soka zaidi ya maandalizi mazuri tena yale ya kisayansi, yaani kuanzia vifaa vya mazoezi, mechi za majaribio, kambi nzuri, chakula kizuri, mafunzo mazuri pamoja na wachezaji kulipwa posho zao kwa wakati unaotakiwa.

Jukumu la posho ni la TFF, Shirikisho la Soka Tanzania, hivyo viongozi wa shirikisho hilo wahakikishe wachezaji wanapewa posho zao mapema tena itakuwa vizuri kama watalipwa sawa na wenzao wa timu ya wanaume, Taifa Stars.

Hakuna sababu ya kuibagua Twiga Stars katika viwango vya posho kwani wote hao ni wachezaji na wanamajukumu yanayolingana katika jamii (katika familia zao) na sio kuwaona wengine wako juu zaidi.

Kiongozi mmoja wa TFF alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa kuna tofauti ya vyanzo vya pesa kati ya Twiga Stars na Taifa Stars, .

Lakini hilo haliingii akilini kwani mzazi mmoja (TFF) na watoto (Stars na Twiga) wana majukumu sawa nje ya nchi, sasa iweje walipwe tofauti ?

Kama kanuni zenu ndizo zimeelekeza hivyo, basi mzibadilishe ili watoto wenu hao wapate maslahi sawa tofauti na sasa, ambapo wengine wanaonekana bora zaidi kuliko wenzao.

Ni matumaini yetu kuwa hii wiki moja iliyobaki, Twiga Stars mtaitumia vizuri kurekebisha makosa yenu ili muweze kujiweka sawa kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Afrika Kusini, na bila shaka mtashinda endapo mtaondoa kasoro ndogo ndogo zilizokuwepo.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Twiga Stars.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.