14 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Nafasi ya mazingira bora katika kuondoa umasikini
 
2006-07-14 11:46:34
Na Jackson Kalindimya

Kwa namna yoyote ile kuwekeza katika hifadhi bora ya mazingira endelevu ni hatua hasa ya kujikomboa kiuchumi na kuongeza fursa kwa watu kujinasua toka kwenye lindi la umasikini katika nchi zinazoendelea.

Makala hii ya Mwandishi Wetu, Jackson Kalindimya yazungumzia nafasi ya mazingira katika kuondoa umasikini.


Shughuli za kujiletea maendeleo zinazofanywa na binadamu kwa kiasi fulani zimefanikiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kimaisha kwa baadhi ya watu,lakini kwa upande mwingine zimeathiri sana mazingira na kuathiri maisha ya watu wengi hasa waishio vijijini ambao maisha yao yanafungamana na mazingira.

Mwaka 2000, viongozi wa nchi 189 wanachama wa Umoja wa Mataifa, walitia saini Tamko la Milenia. Miongoni mwa vipengele muhimu katika tamko hilo ni Malengo manane ambayo ni kupunguza hali ya umasikini uliokithiri duniani, kuhakikisha mazingira endelevu yaani kuingiza misingi ya maendeleo endelevu yanayojali hifadhi ya mazingira katika sera na mipango ya nchi.

Na kupunguza kwa nusu idadi ya watu wasio na uhakika wa maji safi na salama.

Hata hivyo, kumekuwa na tofauti kubwa kati ya matamshi ya makubaliano yanayofikiwa na utekelezaji wake.

Hali hii imesababisha kuwa vita ya kupambana na umasikini haijatoa matarajio yanayotarajiwa.

Wakati hali iko hivyo ni kwamba uharibifu wa mazingira unaendelea kwa kasi.

Tanzania imejaliwa kuwa na raslimali nyingi zikiwemo madini,misitu,ardhi nzuri kwa kilimo,mabonde kwa ajili ya kuhifadhi uoto wa asili, viumbe mbalimbali na kilimo,ufugaji,uvuvi ni miongoni mwa shughuli zinazochangia uchumi wa taifa.Hata hivyo, tatizo kubwa limekuwa likikabili hali hiyo ni hifadhi ya mazingira na matumizi endelevu.

Asilimia 80 ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo.Uharibifu wa mazingira unaoathiri kilimo ni kwamba unaathiri maisha ya watu wengi na kuchangia hali ya umasikini kujiimarisha.

Makamu wa Rais Dk Ali Mohammed Shein April mwaka huu, alitoa tangazo la serikali kuhusu hatua za haraka za kuhifadhi mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji, alisema nchi inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira hususan uharibifu wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji.

Uharibifu huu unatokana na shughuli za kilimo kisicho endelevu,unaofanywa katika maeneo ya vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kwenye vilele vya milima,kwenye miteremko ya milima na sehemu nyingine za milima.

Wachungaji nao huhamahama na makundi makubwa ya mifugo kutafuta malisho na maji,kwa ajili ya mifugo yao na hivyo,husababisha uharibifu mkubwa.

Dk. Shein alisema kuwa uharibifu huo wa mazingira ndio kiini kinachosababisha hali ya jangwa,ukame na kukauka kwa vyanzo vya maji nchini.Kwa wastani hekta za misitu zipatazo 91,300 hupotea kila mwaka.

Katika sekta ya nishati ya umeme, upungufu wa maji katika mabwawa,pamoja na sababu nyingine, umepunguza mchango wa vyanzo vya maji kutoka takriban asilimia 65 mwaka 2003 hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2005;hali ambayo imesababisha kuongezeka kwa matumzi ya umeme uzalishwao kwa mafuta,mgao wa umeme na kuathiri shughuli za uchumi,maendeleo ya jamii kwa ujumla ikiwa pamoja na kukwamisha juhudi za kupunguza kasi ya umasikini.

Hifadhi duni ya mazingira ni chanzo cha magonjwa ambayo yanachangia kupanuka kwa umasikini.Miaka ya karibuni tumeshuhudia milipuko ya magonjwa ya kipindupindu kutokana na uchafu wa mazingira.

Sensa ya mwaka 2002 imebainisha kuwa asilimia 33 ya watu waishio vijijini Tanzania Bara wanategemea visima visivyofunikwa na asilimia 34 ya Wazanzibar hawana vyoo
.Katika mazingira hayo ni rahisi sana uchafu wa aina yoyote, ukiwemo vinyesi kuingia visimani au mitoni na watu kunywa hata kupata madhara.

Watu masikini ndio ambao wako katika hatari kubwa ya kukumbwa na athari za mazingira na upungufu wa maji au ukame na mafuriko.Hii ni kutokana na ukweli kuwa maisha yao yanategemea sana hali nzuri ya mazingira kwa ajili ya kustawisha mazao yao, kulisha mifugo,kupata maji ya kunywa,dawa,miti na manyasi kwa ajili ya ujenzi na faida nyinginezo zitokanazo na mazingira.

Hata kama kutakuwa na mikakati ya aina gani ya kupiga vita umasikini endapo haitazingatia hifadhi ya mazingira na matumizi endelevu ni kwamba itakuwa vigumu sana kupunguza umasikini kwa watu wengi ambao sio rahisi kuwatenganisha na mazingira.

Mkakati wa Kupiga Vita Umasikini na Kuinua Uchumi (MKUKUTA) na Dira ya Taifa ya 2015,malengo yake ni mazuri yanayoainisha njia muafaka za kupunguza umasikini ikiwa pamoja na hifadhi ya mazingira endelevu.

Dk Shein akitangaza hatua za haraka kukabili hifadhi ya mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji alisema kuwa programu za hifadhi ya mazingira na mipango ya matumzi bora ni kwamba kila wilaya iandae programu ya hifadhi ya mazingira na mpango shirikishi wa matumzi bora ya ardhi,ifikapo Desemba 2006.

Halikadhalika kampeni ya elimu ya mazingira kwa umma inaanzishwa kwa kuzishirikisha serikali za mitaa na taasisi mbalimbali kwa kuwa ni suala muhimu.

Tatizo lipo kwenye utekelezaji ambao yawezekana ukachukua muda mrefu kupata matokeo yanayotarajiwa.

Uharibifu wa mazingira sio tu umechangia kuwepo kwa ukame na hata mvua inaponyesha, kumekuwa kukijitokeza tatizo la mafuriko kutokana na mikondo ya maji kuharibiwa na shughuli za binadamu.

Mlima Kilimanjaro, kwa miongo mingi kilele chake kilikuwa kinafunikwa na theluji katika eneo hili la Ikweta kutokana na kuzungukwa na misitu na uoto wa ya asili katika mazingira yake.

Uvunaji holela, uchomaji wa misitu na shughuli za binadamu katika eneo hilo ambayo ni makazi ya aina mbalimbali ya ndege,wanyama na mimea ya asili madhara yake sasa yanajidhihirisha.

Barafu imeanza kuyeyuka na kama hatua za makusudi hazitachukuliwa kudhibiti hali hiyo yawezekana baada ya miaka michache ijayo hali ikawa mbaya zaidi au barafu kuwa suala la kihistoria tu.

Athari za mafuriko katika eneo la Moshi vijijini mapema mwaka huu sio tu yalitishia maisha ya watu ni pamoja na kuimarisha hali ya umasikini wa mali na mifugo yao iliyozolewa na mafuriko hayo.Ni vigumu kutohusisha uharibifu wa mazingira unaofanywa na binadamu na matukio ya aina hiyo.

Watalaamu wa mazingira wanasema mabadiliko ya hali ya hewa,ongezeko la joto, upungufu wa mvua na maji ni matokeo ya kujitakia kwa binadamu kutokana na vitendo vyao vya uvunaji holela wa raslimali usiozingatia hifadhi ya mazingira endelevu zilizomo ardhini na majini.

Changamoto muhimu ni namna ya kuwawezesha watu masikini kuboresha maisha yao, hatua ambayo inatakiwa kuwa na mtazamo makini katika umiliki wa raslimali ya ardhi kwa wenyeji na ushiriki wao katika utawala wa raslimali na kudhibiti rushwa ambayo imekuwa ikitumiwa kuvuruga na kupora miliki toka kwa wenyeji na kupewa wageni ambao hawazingatii maendeleo ya mfumo wa mazingira endelevu zaidi ya kutilia mkazo uvunaji holela tu.

Katika utafiti uliofanywa na Taasisi ya Raslimali ya Dunia(WRI),na kutolewa ripoti ijulikanayo World Resources:The Wealth of Poor-Managing Ecosystems to Fight Poverty imebainishwa kuwa serikali ya Tanzania imemilikisha kwa wasukuma ekari 700,000 zilizokuwa katika hali ya jangwa mkoani Shinyanga na sasa umetunzwa kwa njia za asili (ngitiri) na kustawi vyema hata eneo hilo kuvikwa vazi la kijani baada ya mkakati maalum.

Sasa malisho kwa ajili ya mifugo yanapatikana na kuongeza upatikanaji maziwa,nyama,ngozi na hivyo kuboresha maisha yao ikiwa pamoja na upatikanaji wa dawa kutokana na ongezeko la miti, ndege na wanyama mbalimbali katika eneo hilo.

Ni muhimu sana mikakati ya serikali ikazingatia kuwa na mitaala ya ufundishaji elimu ya hifadhi ya mazingira katika ngazi zote ili watu wafahamu umuhimu wake na kuzingatia katika maisha yao yote.

Mshauri wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi (ESRF),Prof Ndalahwa.F.Maduhu katika mada yake inayochambua kama hatua za sasa za kudhibiti mazingira zinakinzana na juhudi za kupunguza umasikini, anapendekeza kuwa kuna haja kubwa ya kuwekeza kwa dhati katika elimu ya mazingira.

Halikadhalika jamii ihamasishwe na kuwezeshwa kutumia vyanzo vingine vya nishati.Serikali imetangza kupunguza gharama za vifaa vya nishati mbadala kwa ajili ya kupikia.Hatua hii ni ya kuiunga mkono kwa dhati.

Prof Maduhu alishauri kuwe na mipango mizuri ya ardhi kwa makundi yote nchi nzima yaani wafugaji,wakulima na watu wengine ili uwepo uwiano katika matumizi ya ardhi.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.