13 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Bi Mkumbo: Na mifuko mbadala ya plastiki
 
2006-07-13 09:29:35
Na Sharon Sauwa

Hivi karibuni Serikali ilipandisha ushuru kwa mifuko ya plastiki ikiwa ni jitihada ya kutunza mazingira. Katika makala hii Mwandishi Wetu Sharon Sauwa anaelezea jitihada za Kituo cha Songela Wedding & Homecraft katika kupunguza matumizi ya mifuko hiyo kama anavyozungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho Bi. Sarah Mkumbo katika viwanja vya Maonyesho ya Kimataifa ya 30 ya Biashara katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam yaliyomalizika hivi karibuni

Ulipokuwa unaingia katika banda la Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo(SIDO) katika viwanja vya Mwalimu Nyerere kwenye Maonyesho ya Biashara Moja ya ulichokuwa unakiona ni mifuko ya nguo iliyonakshiwa kwa rangi mbalimbali.

Unaposogea karibu na kugusa mifuko hiyo unagundua tofauti iliyopo kati yake na mifuko mingine ya nguo ambayo umewahi kuiona nchini.

’’Nipo mbioni katika ubunifu wangu wa kutengeneza mifuko ya nguo ambayo itauzwa kwa bei rahisi na watu wa hali ya chini wanaweza kuimudu,’’Mkurugenzi Mtendaji wa Songela Wedding & Homecraft Center Bi. Sarah Mkumbo anasema unapotaka kujua nini mipango yake katika kuhakikisha kunakuwepo na mifuko mbadala wa mifuko ya plastiki.

Mbali na kuitengeneza katika kiwanda chake kilichopo Tegeta, anatarajia kutafuta sehemu ya kuuza mjini ili huduma hiyo iweze kusogea karibu na wahitaji.

Anasema kuwa mifuko hiyo itauzwa kwa kati ya Sh. 200 na Sh. 1000 ambapo mtumiaji ataweza kuifua na kisha kuitumia tena katika shughuli zake bila kuathiri ubora wake.

Bi. Mkumbo ambaye kitaaluma ni mwalimu wa sekondari, alianza kuchakarika na biashara rasmi mwaka 1996 mara alipoamua kuacha kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari ya Zanaki Jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, anasema alianza biashara hiyo, mwaka 1992 kama kazi ya ziada mara alipokuwa anatoka shuleni.

Anasema alikuwa akijishughulisha na utengenezaji wa batiki lakini alipoona kila mtu anaifanya biashara hiyo akaamua kubuni kitu kingine ambacho ni kutengeneza mifuko ya nguo.

Lakini kwa kawaida na mara nyingi mifuko inayouzwa ya nguo ambayo imenakshiwa kwa maua mbalimbali husinyaa na kuchuja rangi.

Hata hivyo, Bi. Mkumbo anasema ya kwake ni tofauti na mifuko hiyo kwa kuwa anatengenezea kitambaa kigumu na malighafi anazozitumia huwa hazichuji.

Anasema hata hivyo haikuwa rahisi hata kidogo kuiacha kazi ya ualimu na badala yake aliamua kuanzisha chuo cha mafunzo ya ushonaji, mapishi na mambo mengine.

Mwanamke huyo ambaye amewahi kuwakilisha nchi katika maonyesho ya kwanza ya wanawake ya dunia yaliyofanyika mwaka 1996 mara baada ya mkutano wa kimataifa wa Beijing, anasema haikuwa kazi rahisi hata kidogo kuisahau taaluma yake ya kufundisha.

Anasema mara baada ya kuacha kazi, aliamua kuanzisha chuo hicho ili aweze kuendeleza azma yake ya kuwamegea vijana ujuzi walionao.

Hivi sasa anasema anawanafunzi 15 ambao sasa wamekuwa wakisaidiana katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na kampuni yake.

’’Ili waweze kupata utaalamu wa biashara nimeamua kuwatafutia sehemu katika banda la Mama Mkapa ambapo wamekuwa wakikutana na wafanyabiashara wengine na kupata uzoefu, nataka nao waweze kuinuka na kuwa kama mimi, wanaweza,\”anasema Bi. Mkumbo.

Anasema chuo chake , mbali ya wanafunzi hao anao wataalamu wanne ambao amekuwa akiwasimamia na kusaidiana nao katika shughuli hizo.

Anasema tangu abuni biashara hiyo mwaka 2003, imekuwa na mafanikio makubwa kwani imeweza kukubalika katika soko la hapa nchini na kimataifa.

Anasema hivi karibuni alipeleka mikoba yenye thamani ya Sh. Milioni 2 , ambayo iliisha yote kwa kununuliwa na wafanyabiashara wa maduka ya watalii na wale wa rejareja.

Kuhusu mipango ya kuuza nje bidhaa zake, Bi. Mkumbo anasema wanatarajia kuanza Agosti baada ya kujipanga kwa kuhakikisha kuwa wanakuwa katika mkao wakuzalisha bidhaa zenye ubora sawa zinazotakiwa na wateja hao.

’’Kwa kawaida wateja wa nje ya nchi hawataki mali wanazoziagiza ziwe na tofauti katika utengenezaji ama ukubwa, na hili ndilo linatufanya tujipe muda wa kujipanga vizuri,’’ anasema.

Mbali na hilo anasema kunahitajika mashine ambazo zinauwezo wa kumalizia vizuri mikoba hiyo na pia kuwepo kwa usimamizi wa uhakika katika kila kitengo cha uzalishaji.

Anasema mashine ambayo inauwezo wa kumalizia kazi vizuri ya utengenezaji wa mikoba hiyo inauzwa kati ya Sh milioni 2 na Sh milioni 3.

Hata hivyo, anasema SIDO na moja ya benki hapa nchini imeshamuahidi kumsaidia baada ya kuvutiwa na ubunifu wake na hivyo Agosti mwaka huu wataanza kuliangalia soko la nje ya nchi.

Anasema wanawake wengi wafanyabiashara wanashindwa kuingia katika soko la kimataifa kwa kukosa ujuzi wa kufanya biashara hizo.

Pia analiona pia kama tatizo suala la kugawanya majukumu ya biashara na nyumbani hivyo anasema kunahitajika usimamizi wa ziada katika shughuli zake hizo ili aweze kufanikiwa kuuza nje ya nchi mifuko hiyo.

Hata hivyo, analiona suala la kuibiana mafundi ambao amewafundisha kwa gharama kubwa kama jambo ambalo linabughudhi katika biashara zake.

Pia analizungumzia suala la kuibiana kazi na kuweka katika mtandao, kama vile ni moja ya matatizo yaliyopo nchini.

Akizungumzia kuhusiana na maonyesho hayo anasema si mazuri sana kama mwaka jana kwa kuwa washiriki walikuwa wachache.

’’Nimeshauza karibu nusu ya mzigo niliokuja nao, ila idadi ya watu wanaoingia mwaka huu ni wachache katika dodosa dodosa ya huko mtaani wanasema kiingilio ni kikubwa,’’ anasema na kuiomba mamlaka husika kuangalia upya suala la viingilio.

Anawataka wanawake wengine kuwa wabunifu katika uzalishaji ili waweze kupata soko la uhakika ndani ya nchi na nje ya nchi.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.