|
Serikali isibahatishe katika shauri la ulinzi
2006-07-13 09:28:44
Na Mhariri
Pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bi. Zabein Mhita kuyumba katika kuelezea ukweli kuhusu uwepo wa boti ya doria inayokwenda kasi katika Ziwa Tanganyika, mkoani Kigoma, suala hili nyeti la kitaifa linastahili kufanyiwa kazi hata kama bado limefunikwa.
HII inatokana na ukweli usiopingika kwamba ni lazima mali na mipaka ya nchi hii katika mapana yake vilindwe.
INGAWA wabunge wetu waliulizia masuala ya doria katika maeneo yao, serikali inawajibika kukusanya mashauri haya na kuyafanyia kazi kuhakikisha kwamba doria inafanyika ili kuhami mali ya taifa hili.
UKIANGALIA takwimu za waziri , doria za kutumia ndege zilifanyika katika kipindi cha Agosti 2005 hadi Februari 2006, ambapo jumla ya doria 69 za kutumia meli na sita za angani zilifanyika.Kimsingi, katika ulimwengu uliojaa faulo na vurugu za watu kutaka kuiba mali asili au kuvusha magendo, doria hizo hazitoshi hata kidogo iwe zimetumia meli au ndege.
KUTOKANA na umuhimu huo,tungependa kuungana na wabunge, Bw.Feteh Saad Mgeni (Bumbwini) na Bw. Manju Msambya (Kigoma Kusini) kuikumbusha serikali juu ya haja ya kuimarisha ulinzi na uchumi wa bahari na maziwa makuu.
WATANZANIA hawatapenda kusikia suala la kuwepo tu kwa mikakati mbalimbali ikiwemo kuanzisha vituo vya doria vya kanda katika kuhifadhi mali hizo, wakati inaonekana dhahiri kwamba wapo watu wanaondoka na mali hizo kwa sababu za ukosefu wa kuwepo kwa doria, mathalani meli zinazovua katika kina kikuu, sehemu ya Tanzania.
MAELEZO ya Naibu Waziri katika jibu lake kuhusu boti za doria yanatia shaka kuwa huenda nchi hii kubwa sana na iliyozungukwa na maji , haina doria popote pale, hasa ikizingatiwa kauli yake kwamba boti iendeyo kasi ipo ilihali akijua kwamba ni mbovu, hadi alipobanwa na kusema kwamba serikali inafadhiliwa na wananchi waliotoa meli zao kwa ajili ya doria.
UKIANGALIA majibu ya Naibu Waziri, mtu hatasita kusema kwamba serikali inafanya ajizi katika kuimarisha ulinzi wa mali asili za nchi hii kitu ambacho kinaweza kutumbukiza taifa katika aibu kubwa ya kuondokewa na maliasili bila kutambua.
INGAWA wabunge wamelisemea suala hili, sisi tunaamini kuwa nia ya kurekebisha hali hii ipo kwa hiyo ni lazima tuanze mara moja.
HAITOSHI mheshimiwa waziri kusema kuwa maeneo husika yamepewa vitendea kazi muhimu ikiwemo boti za doria zinazoenda kwa kasi, wakati hicho kitu hakipo na pengine kimekufa na hakiwezi hata kufufuka.
KAMA mbunge wa Kigoma asingepasua jipu ni wazi tungebaki na ukweli nusu na watu wasingetambua kwamba yapo masuala ambayo yanatakiwa kushirikiana na serikali kuyatatua kama shauri la doria.
Wananchi waliojitolea kufanya doria kwa kuwapa boti wanajeshi tunawapongeza na sasa kinachotakiwa ni serikali kufanya kila linalowezekana kupata boti zake mpya kwa ajili ya Kigoma na kwingineko badala ya kusubiri hadi kuazimwa vyombo hivyo vya ulinzi!
|