|
Michezo ya kompyuta na athari zake kwa watoto
2006-07-12 11:42:07
Na Moses Ismail
Kuingia kwa wingi teknolojia ya intaneti kumesababisha kufunguliwa kwa vituo vingi vinavyotoa huduma ya michezxo ya kompyuta kwa njia ya mtandao.
Lakini mbali ya watu wanaoingia kwenye huduma hiyo kuangalia masuala mbalimbali ya habari za kidunia, huduma hiyo pia inamwezesha mtu kushiriki michezo ambayo wataalamu kadhaa wamegundua kuwa ina matatizO Mwandishi Moses Ismail kwa msaada wa mashirika ya kimataifa anaangalia athari za michezo hiyo.
Katika kituo kimoja cha huduma za intaneti Sinza, jijini Dar es Salaam, karibu meza zote za kompyuta zimetawaliwa na watoto wadogo, ambao ama wamekaa wawili wawili au mtoto mmoja peke yake. Lakini wote wakiwa wamezama kwenye michezo ya kompyuta.
Hali hii huwa nakumbana nayo mara kadhaa ninapokuwa katika harakati zangu za kutaka kuangalia vitu fulani kwenye mitandao ya intaneti kwa kompyuta za vituo hivyo ambavyo hutoa huduma kwa kati ya sh. 500 mpaka sh. 800 kwa saa moja.
Kwa mtazamo wa haraka haraka unaweza kufikiri kuwa haya ndiyo maendeleo katika zama hizi za sayansi na teknolojia, kwamba watoto wa nchi hii wameacha kucheza michezo ya kidali, makida makida, kombolela na mingine ya kutumia misuli na sasa wanacheza michezo ya kompyuta.
Mambo haya ya michezo ya kisasa hayaishiii kwenye vituo hivyo vya huduma za intaneti tu, pia ni jambo la kawaida siku hizi kuona karibu katika kila nyumba za watu wenye vipato vya kati wanaoishi mijini, kuna seti maalumu ya aina ya michezo ya eletroniki ambayo huchezwa kwa njia ya video, kwa jina maarufu inaitwa video game.
Kama inavyoonekana ni kwamba ni michezo ya kisasa na ipo kwenye nyumba za kisasa na inachezwa na watoto ambao kwa kiwango fulani wazazi wao angalau wanayo pesa ya kuwawezesha kucheza michezo hiyo na kuachana na michezo ya kujichafua na mavumbi.
Kuenea kwa michezo hiyo kunaenda sambamba na maendeleo ya teknolojia na imetengenezwa kwa kuhusisha vitu kadhaa ikiwemo michezo ya mipira na michezo ya kivita ambayo ndiyo inayopendwa na wachezaji wengi.
Mie napenda kucheza game za vita, anasema Jumal Kuwinga, mtoto mwenye umri wa miaka 9, na kufafanua kuwa anapenda michezo hiyo ya kivita kwa sababu; kwenye vita unaua maadui, unau askari wako wakirudi nyuma.
Mtoto huyu ambaye ndio kwanza yupo darasa la tatu, anasema; ukiwaua askari wengi ndio unakuwa mshindi halafu unaendelea kwenye game nyingine... wanakuja wakali zaidi wakikuua unashindwa na game inaisha.
Bw. George Mlacha yeye ni mfanyakazi kwenye kituo cha huduma za intaneti cha Nakiete Internet Caffe, Mwenge jijini Dar es Salaam, nilipomuuliza ni wastani wa muda gani ambapo mtoto hucheza na kumaliza game mmoja kwa wakati alinieleza:
Hiyo inategemea na uwezo wake mwenyewe, akiwa shapu anashinda hata game tatu kwa saa moja, vinginevyo saa nzima inaweza kuisha hajashinda hata mchezo mmoja, inategemea na uzoefu wake na aina ya mchezo anaocheza.
Bw. Mlacha anasema wengi wa watoto wanakaa kwenye kompyuta moja kwa wastani wa saa moja hadi saa tatu, lakini hili tunaruhusu siku za Jumapili na Jumamosi tu, siku nyingine za masomo hatuwaruhusu kucheza, wanaweza wakaacha kwenda shule, hii michezo ina msahaulisha mtu mambo yake.
Lakini wakati michezo hii ya tenkonolojia inazidi kushamiri hapa nchini na kutapakaa kwa wingi, kuanzia ile ya kwenye kompyuta hadi ya video, tayari nchi za Ulaya na Marekani wameshaanza kutafuta mbinu za kuitokomeza au kuwashawishi watoto wasishiriki kwenye michezo hiyo.
Hili linatokana na tafiti mbalimbali kuonyesha kuwa ,wengi wa watu na watoto wanaoshiriki katika matukio mengi ya uhalifu hasa mauaji ya kutumia bunduki walijengwa moyo wa ujaisiri wa kufanya ghasia kutokana na michezo hiyo hasa ile ya kivita.
Hali hiyo inasababishwa na athari ya mifumo ya utengenezaji wa michezo hiyo ambayo imewekwa katika hali inayomchota mchezaji kisaikolojia na kumjenga katika hali ya kuwa katili.
Katika kitabu chake, On Killing, mtaalamu wa masuala ya saikolojia ya kivita, David Grossman, anasema michezo mingi ya kivita inayochezwa kwenye kompyuta imetengenezwa kwa mfumo ule ule wa kisaikolojia unaotumika kuwaandaa kiakili askari jeshi kupambana na kuua adui zao, ikizingatia kumtayarisha kuwa na kiwango cha juu cha kuua adui na kuwa na moyo wa kuua.
Mtaalamu huyo wa Jeshi la Marekani anasema kwa kuwa michezo hiyo mfumo huo, ni vigumu kuepuka hali ya kumfanya mchezaji asiwe na hulka hiyo kwa sababu anapocheza mchezo unamfunza kuwa katili kwa sababu lugha inayotumika kumuamrisha kuua imetengenezwa kwa mbinu za hali ya juu sana.
Mwishoni mwa mwaka jana nchini China, mtoto wa miaka 12 alimuua baba yake mzazi kwa kumsukuma kwenye dirisha la nyumba yao iliyopo kwenye ghorofa ya saba jijini Shanghai, baada ya baba huyo kufuta michezo yote ya kivita iliyokuwemo kwenye kompyuta yake.
Maoni ya wataalamu kama Bw. Grassman yamechochea taasisi mbalimbali kufanya utafiti juu ya suala hilo ambapo utafiti mwingi zaidi umeonyesha kuwa tatizo la kuwa na watoto wenye tabia za kikatili linalo zihangaisha nchi nyingi za Ulaya na Marekani limechangiwa kwa kiasi kikubwa na michezo hiyo ya kivita inayochezwa kwa eletroniki kwa njia ya kompyuta au video.
Kinyume na ilivyokuwa ikionekana zamani, kwamba sinema za kikatili na kivita zinanguvu za kumfanya mtoto kujifunza ukatili, utafiti mwingine uliofanywa na kuchapwa kwenye jarida la Journal of Personality and Social Psychology, michezo hiyo ya video na kompyuta ina uwezo mkubwa wa kumfanya mtoto kuwa katili kuliko sinema za kivita au za kikatili.
Sinema za kivita na za kikatili zinashawishi mtu kutaka kuwa katili, lakini michezo ya video na kompyuta inamfanya mchezaji ajihisi kuwa ni mshirika, inamjenga katika hali ya kuwa katili na si kufikiri kuwa katili, unasema utafiti huo.
Nilizungumza na daktari mmoja wa magonjwa ya akili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambaye hata hivyo hakutaka jina lake litajwe gazeti yeye alisema licha ya michezo hiyo kuwa na athari za kisaikolojia, pia ina athari nyingine nyingi kwa watoto.
Watoto wanaweza pia kupata athari ya afya ya mwili na kukumbwa na magonjwa mengine yanayotokana na kutotumika sawasawa kwa virutubisho vya chakula wanachokula kwa sababu hawashiriki michezo ya kutumia nguvu , alisema dokta huyo na kufafanua:
Hii alisema inatokana na mtoto akishakuwa muathirika wa michezo ya kukaa sehemu moja, sio ya kivita peke yake au hiyo ya teknolojia, hata kama itakuwa ni drafti, chakula anachokula kinakosa kutumika vizuri mwilini na kusabamsababishia aina fulani ya magonjwa yanayotokana na mwili kutofanya mazoezi.
Daktari huyo anasema hili likichanganyika na kufikiri mbinu za mchezo kwa muda mrefu, kukosa usingizi kwa kucheza mchezo karibu robo tatu ya usiku, linaweza kumsababishia mtoto matatizo ya kurukwa na akili ambayo huanza kwa kuonyesha dalili za mtoto kuwa na tabia ya ukali na kufoka kwa kila jambo asilokubaliana nalo.
Daktari huyo anasema pia kitendo cha kukaa mbele ya miali ya kompyuta au tv kwa muda mwingi nacho humsababishia mtu kupatwa na matatizo ya macho ambayo hutokana na mionzi mikali inayotokana na mwali wa mwanga wa kompyuta au televisheni.
Zipo athari nyingi, ila kwa sababu hizo za kisaikolojia ndio mbaya zaidi, ndio maana watafiti wengi wamezama kwenye upande huo, ila hizi game kweli zina athari kubwa kiafya kama hazitachezwa kwa mpangilio, na zikichezwa kwa mpangilio zinaweza kuwa ni sehemu nzuri ya kujenga uwezo wa akili ya mtu, anasema.
Wakati michezo hiyo ikionekana kuwashughulisha wazungu ambao wanatafuta kila aina ya mbinu za kupambana nayo, lakini barani Afrika inaonekana kuwa ni kitu ambacho kila mzazi wa kisasa angependa kuona mtoto wake anapata michezo hiyo.
Umasikini tu, lakini kama ningekuwa na pesa lazima ningehakikisha mtoto wangu anakuwa na zaidi ya play station (aina ya michezo) nne mpaka tano, bora mtoto acheze michezo hii aongeze akili kuliko kucheza michezo ya kujichafua, anasema Amiri Mnambenga mmachinga anayeuza vifaa vinavyotumika kuendesha michezo hiyo kwa njia ya video.
Tatizo linalojitokeza karibu katika ulimwengu wote ni kuwa kupambana na kusambaa kwa michezo hiyo duniani si jambo rahisi kwa sababu mingi ya michezo huuzwa kwenye masoko yaliyo kwenye mtandao wa intaneti, on line marketing, ambayo si rahisi kudhibitika.
Katika soko hilo mnunuzi huingia na kununua programu ya mchezo anaotaka kwa kutumia kadi yake ya malipo na papo hapo hutumiwa aina ya mchezo anaoutaka na kuingiza kwenye kompyuta yake na kuanza kucheza.
|