|
TUKI yahifadhi nyaraka za kale za Kiswahili
2006-07-11 09:52:24
Na Jackson Kalindimya
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI),Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivi karibuni iliiaga Halmashauri yake, kuzindua vitabu, makavazi na kutoa tuzo kwa wafayakazi wake bora. Makala hii ya Mwandishi Wetu, Jackson Kalindimya yaelezea zaidi.
TAASISI ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam miongoni mwa majukumu yake ni kufanya utafiti katika nyanja zote za lugha ya Kiswahili, kuchapisha na kuyasambaza matokeo ya utafiti ili yatumiwe na walimu, wanafunzi, waandishi wa habari na wengine wote wanaohusika na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili.
TUKI hivi karibuni, ilizindua vitabu vinne na makavazi katika sherehe ya kuiaga Halmashauri ya TUKI iliyomaliza muda wake na kutoa tuzo kwa wafanyakazi wake bora kwa mwaka 2005. Mgeni rasmi katika sherehe hizo ni Afisa Mkuu Taaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof Mayunga, H.H.Nkunya.
Katika mfumo wa Chuo Kikuu, Halmashauri ya kitivo au taasisi ni chombo au kamati ya Seneti na ni asasi muhimu kabisa katika kusimamia shughuli za kitaaluma na kuhakikisha kuwa ubora na viwango vinadumishwa. Halmashauri hufanya kazi kwa kipindi cha miaka mitatu.
Profesa Nkunya alisema kuwa uzinduzi wa machapisho na makavazi ni hatua muhimu katika kukifanya Kiswahili kitambe na kutambaa katika nyanja anuwai za kitaaluma.
Bila shaka wananchi walio wengi ambao hawakuweza kuzipata taaluma hizi kwa lugha ya kigeni sasa, wataweza kufaidika nazo kwa lugha wanayoifahamu. Makavazi hayo ya TUKI ya kwanza ya aina yake nchini na pengine duniani kote kwa maana ya kwamba hakuna makavazi mengine popote pale ambayo ni mahsusi kwa hifadhi ya nyaraka zinazohusu lugha ya Kiswahili tu za tangu kale (kabla ya ukoloni) hadi leo na siku zijazo alisema.
Makavazi hayo ambayo yamezingatia dhana pana ya nyaraka sio za karatasi tu kwa namna yoyote ile yatakuwa ni kituo muhimu cha utafiti wa historia,maendeleo na mafanikio ya lugha ya Kiswahili hapo baadaye.
Uzinduzi huo wa vitabu na makavazi ( yaani hifadhi ya nyaraka) uliofanyika hivi karibuni Chuoni hapo ulihudhuriwa na wakuu wa vitivo na wakurugenzi, wajumbe wa Halmashauri ya TUKI, maprofesa, watafiti, wahadhiri na washiriki wengine.
Vitabu vilivyozinduliwa ni Nyimbo za Liongo zilizoimbwa katika karne ya 13(miongoni mwa nyimbo za zamani zaidi za Kiswahili), Jarida la Taasisi ya TUKI(2004), Utenzi wa Vita vya Majimaji na Jifunze Kompyuta kwa Kiswahili hatua ya kwanza(lengo kumsaidia wazungumzaji wa Kiswahili kuifahamu teknolojia ya kompyuta)
Mkuu huyo alieleza wasiwasi wake kwa baadhi ya wanataaluma ambao wakishapata ajira hapo Chuoni, huitumia nafasi hiyo kwa manufaa yao binafsi bila ya kujali maslahi ya Chuo. Tatizo limekuwa likijitokeza katika vitivo mbalimbali.
Sina budi kusisitiza kuwa uanataluma wa kweli si maarifa yaliyo kichwani tu, bali pia ni tabia ya mtu mwenye taaluma ambayo inapaswa kumtofautisha na yule asiyekuwa na taaluma.
Hapa nazungumzia suala itikeli (ethics) na masuala ya uadilifu na uaminifu kwa jumla.
Sisemi kwamba mwanataaluma asinufaike na taaluma yake, lakini kunufaika huko kusiwe ni adha kwa asasi iliyomwajiri, bali kunufaishe pande mbili aliwaambia.
Alipongeza mchango muhimu na mafanikio ya TUKI yaliyofanywa wakati Halmashauri hiyo ikiwa madarakani kuanzia mwaka 2003/2004 kwamba yasingewezekana bila ya usimamizi na ushauri wao, ikiwa pamoja na kutumia juhudi na raslimali zao kidogo katika kutengeneza makavazi.
Moyo huu wa kujitegemea ni jambo zuri linalofaa kuigwa na vitivo vyote hapo Chuoni, maana tutake tusitake, hakuna mhisani yeyote ambaye atatusaidia milele na kwa kila jambo aliwaasa.
Halmashauri ya TUKI ina uwakilishi toka,Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA),Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA), Kurugenzi ya Utamaduni ya Utamaduni ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo na Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Zanzibar (TAKILUKI).
Uwakilishi mwingine ni wa Idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwakilishi wa Seneti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Wakuu wa Sehemu katika TUKI.
Mgeni rasmi alimpongeza na kumshukuru Mkurugenzi wa Taasisi hiyo aliyemaliza muda wake,Profesa Mugyabuso Mulokozi ambaye ameitumikia taasisi hiyo katika nafasi hiyo kwa vipindi viwili,yaani miaka sita tangu mwaka 2001.
Nakupongeza Mkurugenzi kwa kumaliza vizuri muda wako wa uongozi na kwa kuifikisha TUKI katika hatua hii ya sasa ya kujivunia alisema.
Mgeni rasmi pia alimpongeza, kumkaribisha na kumtakia mafanikio katika wadhifa wake mpya wa Ukurugenzi wa TUKI, Dkt John G.Kiango.
Matarajio yangu ni kwamba utaisogeza TUKI mbele zaidi na kuiinua juu zaidi ya pale ambapo watangulizi wako wameifikisha alimwambia.
Mkurugenzi wa TUKI aliyemaliza muda wake, Prof Mulokozi, akimkaribisha mgeni rasmi, alisema kuwa bahati mbaya sana kuwa
Waafrika hawana utamaduni wa kutunza nyaraka hasa zile za maandishi kwani huzitupa bila ya kujali thamani ya kile kilichoandikwa humo.
Watu wengi tayari wamepoteza vyeti vya kuzaliwa,vyeti vya ndoa, vyeti vya kumaliza shule,achilia mbali madaftari yao na vitabu walivyotumia walipokuwa shule.
Wazazi wanapofariki watoto hupekua katika makabati na masanduku na kuchukua vitu wanavyoona vina thamani, ambavyo aghalabu ni ngyo na vifaa vya matumizi na kuchoma takataka ambazo aghalabu ni nyaraka na makaratasi alisema.
Tabia hiyo, alisema kuwa ipo pia katika asasi zetu za kiserikali na za binafsi na kwamba TUKI zipo nyaraka za tangu mwaka 1930 au hata kabla. Hata hivyo utunzaji wake ulikuwa hafifu na zinegweza kupotea wakati wowote kwa kutoithaminiwa.
Katika hali hiyo Prof Mulokozi alisema kuwa nyaraka nyingi zilizokuwepo wakati huo au ambazo walikuwa na nakala zake hapo zamani, sasa zinapatikana Ulaya tu, na kwamba hali isipoangaliwa itafika mahala kuanza kwenda Ulaya kununua nakala za nyaraka zetu wenyewe.
Makavazi haya tumeyaanzisha kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hili sugu na kuhakikisha kuwa nyaraka zote muhimu zinahifadhiwa vizuri kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Makavazi hayo yapo katika hatua ya mwanzo kabisa kwani uainishaji na ukatologi wa nyaraka hizo kimakavazi bado haujafanyika na uhiafdhi wa kikemikali wa nyaraka kuu ili zisiharibike haujaanza.
Makavazi yaliyozinduliwa yana nyaraka za kale za tunfo za washairi (kuanzia A.D.1600 hadi leo), kamusi za Kiswahili tangu 1882 hadi leo, tafsiri za Kiswahili (tangu 1652), machapisho ya Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki (1930 hadi leo), magazeti ya Kiswahili(kuanzia 1923).
Nyingine ni nyaraka za utafiti katika TUKI(1964 hadi leo),majarida yote ya Kamati na TUKI(1930-2005),kanda za sauti,video,disroma(CDs) na mengineyo.
Katika kumbukumbu hizo pia kuna taarifa za mikutano ya mwanzo ya Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki(1930 - 1944) zilizoandikwa kwa mkono zenye kuonyesha namna Kamati hiyo ilivyokuwa ikiunda Kiswahili sanifu.
Mkurugenzi huyo mstaafu, alielezea tatizo sugu linaloikabili TUKI na upungufu wa wanataluma ambapo kuna nafasi tupu zaidi ya 10 zinazohitajika kujazwa ambapo wanataaluma wa aina hiyo wenye sifa hawapatikani kwa urahisi.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na TUKI kukabili tatizo hilo ni kutafuta vijana wa kuajiri waliohitimu shahada ya uzamili kila mwaka na mwaka jana wameanzisha Mfuko wa Shaaban Robert wa Misaada ya Masomo ya Uzamili na Uzamivu.
|